loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Hakuna mfanyakazi wa iliyokuwa EAC anayedai - Kabudi

WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi amesema hakuna mfanyakazi wa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), anayeidai kiasi chochote cha fedha na kwamba wote walishalipwa.

Pia amesema Sh bilioni 117 walizokuwa wakidai wafanyakazi 31,831 wa jumuiya hiyo walioingia makubaliano na serikali, walilipwa tangu mwaka 1977. Profesa Kabudi aliyasema hayo jana mjini hapa wakati akihitimisha hoja ya Azimio la Bunge la Kuridhia Itifaki ya Kinga na Maslahi ya Kidiplomasia ya Jumuiya ya Afrika Mashariki. Alisema ndani ya kipindi cha miaka 20, wamejenga jumuiya imara na ili iendelee kuwa imara, lazima ibebwe na misingi miwili.

Alibainisha kuwa fedha za wafanyakazi 31,831 wa jumuiya hiyo walioingia makubaliano na serikali walipwe Sh bilioni 117, walilipwa wote.

“Orodha ya wafanyakazi wote ipo, walio hai na waliokufa na waliochukua haki yao mahakamani. Hakuna mfanyakazi wa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki anayeidai serikali fedha yoyote” alisema.

Awali, Profesa Kabudi alisema kuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki ilivunjika mwaka 1977 na mpaka inavunjika Uganda iliendelea kutoa michango yake yote chini ya uongozi wa Idd Amin.

“Ukweli wa kihistoria nchi ambayo haikutoa michango yake kabla ya hapo inafahamika na kwamba baada ya kuvunjika na Tanzania ililazimika kufunga mpaka na Kenya” alisema.

Alisema jitihada zilifanyika chini ya aliyechaguliwa kuwa msuluhishi na Benki ya Dunia na Shirika la Fedha Duniani mwaka 1984 Cairo nchini Misri. Profesa Kabudi alisema katika makubalianao hayo, waliangalia mambo mbalimbali kuwa ni mali gani zinakuwa za pamoja licha ya jumuiya kuvunjika, ambapo Benki ya Maendeleo ya Afrika Mashariki iliendelea kuwa mali ya pamoja ambayo ilikuwa Uganda. Alisema pia walikubaliana kuwa daima Mwenyekiti na Mkurugenzi Mtendaji, anatakiwa atoke hapa nchini Tanzania.

Profesa Kabudi alisema nchi ambayo haikufaidika ni Uganda na ndio maana ndani ya mkataba huo, ilikubaliwa wawe na viwango ambapo Kenya na Tanzania walipewa viwango vya kuifidia Uganda na ikishindikana watalipa riba ya asilimia saba.

“Mara baada ya mkataba huo kusainiwa 1984 nchi iliyotoa ushirikiano mkubwa ni Uganda, ndipo kila nchi mwanachama ilipeleka katika mabunge yake sheria ya kuridhia mkataba wa Afrika Mashariki,”alisema Profesa Kabudi.

Alisema kuwa hakuna ombwe panapotokea mgogoro, hata kama mkataba na sheria hiyo haijatamka ; na kwamba kila jambo linalofanyika lazima wajadiliane kiitifaki. Awali, akiwasilisha mapendekezo ya azimio hilo, Profesa Kabudi alisema kuridhiwa kwa Itifaki hiyo kutawezesha kuwawekea kinga watumishi wa EAC na kulinda mali za jumuiya mahali popote zilipo katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Alisema pia itasaidia kuwepo kwa kinga ya mali na fedha za jumuiya dhidi ya athari yoyote ya mahusiano ya kidiplomasia, au pale nchi moja au zaidi zitaamua kujitoa katika jumuiya.

“Pia itatasaidia kuwa na mfumo wa misamaha ya kodi unaowiana baina ya nchi wanachama hususan kwa wataalam, washauri elekezi na vitendea kazi, kuwianisha utoaji wa kinga na maslahi ya kidiplomasia kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki na taasisi zake.

Aidha, alisema itawezesha wafanyakazi wa EAC na taasisi zake, kupewa kinga na maslahi sawa bila kujali nchi waliyopo na hivyo kuongeza ari ya utendaji, kujenga imani kwa nchi wanachama kuwa nchi yetu ina nia ya dhati ya kuendelea kuwa mwenyeji wa taasisi za Jumuiya zilizopo na zitakazoanishwa.

Profesa Kabidu aliainisha pia kuwa itifaki hiyo pia itasaidia nchi kunufaika kiuchumi kutokana na kuwa mwenyeji wa taasisi za jumuiya kupitia matumizi yasiyoepukika kama vile pango la ofisi, makazi ya watumishi wa jumuiya, chakula, malazi, mafuta ya magari, huduma za mtandao wa intaneti, bima, shajara, huduma za hoteli na chakula, kuitangaza nchi yetu kimataifa kupitia utalii wa mikutano.

Bunge pia limepitisha Azimio la Kuridhia Itifaki ya Jumiya ya Afrika Mashariki ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, ambayo itaweka mazingira wezeshi yatakayoleta utatuzi wa changamoto zilizopo katika sekta ya Mawasiliano. Changamoto hizo ni pamoja na gharama kubwa za huduma za mawasiliano, huduma za “roaming”, changamoto katika maunganisho ya miundombinu, mwingiliano wa masafa hususan katika maeneo ya mipakani, na changamoto za usalama wa mitandao.

foto
Mwandishi: Anastazia Anyimike, Dodoma

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi