loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Wanafunzi milioni 3 wasajiliwa mpango wa elimu bure

KATIKA kipindi cha miaka minne tangu kuanzishwa kwake, mpango wa elimu bure nchini umezaaa matunda baada ya wanafunzi milioni tatu kusajiliwa. Kati ya hao, kwa upande wa shule za msingi waliosajiliwa ni wanafunzi milioni 2.4 na sekondari 600,000.

Pia, serikali imeanza kuifanyia mapitio Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014, ambayo wadau mbalimbali wakiwamo wabunge watapata fursa ya kutoa maoni yao. Hayo yamebainishwa bungeni jana na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, William Ole Nasha wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalumu, Suzan Lyimo (Chadema).

Katika swali lake, Lyimo alisema walimu wa shule za msingi, wanafundisha mitaala sawa na awali, wakati awali ni za msingi sana na ndipo mtoto anapata elimu ya muhimu sana hivyo wanapaswa kufundishwa namna ya kulea watoto, je, serikali haioni umuhimu wa kuwapa kipaumbele walimu hao wa shule za awali. Akijibu swali hilo, Ole Nasha alisema katika kipindi cha miaka minne, serikali imeongeza upatikanaji wa elimu mfano kwa shule za msingi kutoka wanafunzi milioni 8.2 kwa mwaka 2015 hadi milioni 10.6 kwa mwaka 2019.

“Hivyo ndani ya miaka minne tumeongeza wanafunzi milioni 2.4 kwa shule za msingi miaka hiyo,” alisema.

Aidha, alisema kwa upande wa shule za sekondari, wameongeza wanafunzi milioni 1.7 kwa mwaka 2015 hadi wanafunzi milioni 3.3 mwaka mwaka 2019..

“Hivyo ndani ya miaka minne tuna ongezeko la wanafunzi wapya zaidi ya 600,000 na ni matunda ya elimu bila malipo,” alisema Ole Nasha.

Alifafanua kuwa kwa sasa wanarejea mitaala ili iendane na elimu ya sasa na mifumo inafanyiwa kazi na kwenye sera maoni yatakayotokewa, ndio yatafanyiwa kazi ili kuwepo mitaala bora zaidi. Awali katika swali la msingi, Lyimo alisema mfumo wa elimu umekuwa ukilalamikiwa na kukosolewa, na kuhoji kama serikali imefanya utafiti wowote kuona kama lawama hizi zina mashiko au la.

Akijibu swali hilo, Ole Nasha alisema serikali imeanza kuifanyia mapitio Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014, ambapo katika mchakato huo wadau mbalimbali wakiwemo wabunge watapata fursa ya kutoa maoni yao.

Alifafanua kuwa serikali imekuwa ikipokea maoni mbalimbali ya wadau kuhusu Mfumo wa Elimu nchini na kuyafanyia kazi. Pamoja na hivyo, kupitia Mpango wa Maendeleo ya Sekta ya Elimu 2016/17 – 2020/21, wizara kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa elimu imekuwa ikifanya ufuatiliaji na kupokea mrejesho juu ya Mfumo wa Elimu nchini.

Alifafanua kuwa kufuatia mrejesho huo hatua mbalimbali zimekuwa zikichukuliwa kwa lengo la kuboresha Elimu.

foto
Mwandishi: Mgaya Kingoba, Dodoma

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi