loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Mamilioni ya dola aliyowekeza Magufuli yatoa ajira 30,000

UWEKEZAJI wa mamilioni ya dola uliokuwa moja ya vipaumbele vya Rais John Magufuli alipoingia madarakani mwaka 2015, umewezesha kuanzishwa kwa miradi mikubwa mitano ya kimkakati iliyowezesha ajira zaidi ya 30,000 kwa Watanzania.

Alipohutubia Bunge Novemba 25 mwaka 2015 baada ya kuchaguliwa na kuapishwa kuwa Rais wa Awamu ya Tano wa Tanzania, Rais Magufuli alieleza malengo ya kuifikisha Tanzania katika uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025 kupitia sekta ua viwanda ili pia kulinda bidhaa za ndani na kuongeza ajira hasa kwa vijana nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari juzi, jijini Dar es Salaam kuhusu mafanikio ya Serikali kwa miaka minne ya uongozi wa Rais Magufuli, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) Geoffrey Mwambe, alisema miradi ya kimkakati kulingana na sheria na kanuni za uwekezaji zimegawanyika katika uwekezaji wa ndani wa Dola za Marekani 100,000 (TSh 223) na nje Dola 500,000.

Alisema nje ya hiyo, kuna uwekezaji mkubwa wa mamilioni ya dola ulioelezwa na Rais Magufuli kuutekeleza kwa kipindi chake na kwa miaka minne, mapinduzi makubwa yaliyotokana na kuhamasisha na kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji nchini.

“Uwekezaji wa aina hii viashiria vyake ni pamoja na nchi kuaminika kiuchumi na wawekezaji, imani inayowaondolea hofu ya kupoteza fedha wanazowekeza na namna serikali inavyopambana na rushwa na kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji,” alisema.

Mwambe alisema kwa miaka minne, Serikali ya Magufuli kupitia uwekezaji mahiri, imewezesha miradi mikubwa mitano ya mabilioni kuanzishwa kupitia TIC. Miradi hiyo ni wa kuzalisha vigae wa kampuni ya Twyford (KEDA), Chalinze; na kiwanda cha matunda cha Sayona cha kampuni ya Motisun Group kijiji cha Mboga, Chalinze. Mingine ni kiwanda cha kutengeneza sabuni ya unga cha KEDS kilichopo Chalinze; Kiwanda cha Nondo cha Kiluwa group cha Mlandizi, Kibaha na kiwanda cha Goodwill cha kutengeneza vigae (marumaru) cha Mkuranga.

Vyote vikiwa mkoani Pwani. Mwambe alisema Twyford kinazalisha mita za mraba za vigae 50,000 kwa mwaka huku asilimia 90 ya malighafi wakitoa nchini na asilimia 10 nje ya nchi.

Alisema mradi huu wa Dola za Marekani milioni 56 (Tsh bilioni 130) umeajiri maelfu ya vijana. “Mradi mwingine ni kiwanda cha Sayona cha juisi. Hiki kinazalisha tani 300 za matunda kwa siku na kimeajiri Watanzania zaidi ya 800 wa moja kwa moja na 3,000 wasio wa moja kwa moja.

Uwekezaji wake ni Dola za Marekani milioni 55,” alisema. Kwa mujibu wa Mwambe, uwekezaji wa kiwanda cha KEDS wenye thamani ya Dola milioni 11.8 wa kiwanda cha sabuni cha pili kwa ukubwa Afrika umetoa ajira zaidi ya 2000 za moja kwa moja huku maelfu wakipata ajira zisizo za moja kwa moja.

Alisema Kilua kinachozalisha tani 10,000 za nondo kwa siku ni moja yab uwekezaji mahiri uliotoa maelfu ya ajira huku Goodwill cha vigae cha thamani ya Dola milioni 53 kikitoa ajira zaidi ya 1,500 za moja kwa moja na zaidi ya 3,000 zisizo za moja kwa moja.

foto
Mwandishi: Gloria Tesha

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi