loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

China: Kutoka kiwanda cha dunia kuelekea kuwa soko la dunia

MAONESHO ya kimataifa ya uagizaji bidhaa yamefungwa Novemba 10, mwaaka huu mjini Shanghai hapa China, baada ya kufanyika kwa muda wa siku sita.

Nchi na sehemu 181 duniani ambazo kupitia makampuni zaidi ya 3,800 waliweza kuonesha bidhaa na huduma kwenye maonesho hayo, na wafanyabiashara 500,000 walitazama maonesho hayo.

Maonesho haya yaliyoanzishwa mwaka jana yanafanyika katika kipindi ambacho mazingira ya biashara duniani yanaendelea kukumbwa na changamoto nyingi, ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa vitendo vya kujilinda kibiashara, na nchi ambazo zamani zilizoelekea kuwa vinara wa biashara huria duniani, sasa zinaonesha kuanza kufunga milango yao na kuweka vizuizi vya kikodi na visivyo kwa kodi.

Hali hii si kama tu imekuwa ni changamoto kwa uchumi wa dunia kwa sasa, bali pia inaleta hatari kwa maendeleo ya siku za baadaye ya uchumi na biashara duniani. Ukubwa wa maonesho hayo na ushiriki wa makampuni mengi ya kimataifa, vinaonesha kuwa China inaendelea kuwa na mvuto mkubwa kwa makampuni yanayotaka kutafuta faida kutokana na maendeleo ya China.

Lakini pia yanaonesha moyo wa dhati wa China wa kutaka maendeleo yake ya kiuchumi kunufaisha nchi nyingine duniani. Hii ni ahadi ambayo imekuwa ikitolewa mara kwa mara na China, na maonesho haya ni sehemu ya utekelezaji wake.Kwani umaalum wa maonesho hayo ni kuagiza bidhaa na huduma kutoka nje. Mbali na hayo, kupitia maonesho hayo China imetoa jukwaa kwa nchi na makampuni mengine kufanya biashara kati yao.

Kwa mujibu wa takwimu, mwaka huu makubaliano ya uagizaji wa bidhaa yenye thamani ya dola za kimarekani bilioni 71.13 yalisainiwa, kiasi ambacho ni ongezeko la asilimia 23 kuliko mwaka jana. Hali hii inaonesha kuwa umuhimu wa maonesho haya miongoni mwa watu kwenye sekta za viwanda na biashara unazidi kuongezeka.

Lakini pia maonesho haya yameonesha matokeo ya juhudi za China katika kubadilisha muundo wake kutokana na changamoto za uchumi wa dunia kwa hivi sasa. Tangu mazingira ya biashara duniani yaanze kubadilika, kama vile kudorora kwa uchumi wa dunia, kuongezeka kwa vitendo vya kujilinda kibiashara na makampuni ya China kulengwa na baadhi ya nchi za Magharibi ili kuepusha ushindani, China ilianza kuimarisha matumizi ya ndani na kutumia ipasavyo soko lake kubwa lenye watu bilioni 1.4 kama injini mpya ya kuhimiza ongezeko la uchumi wake, na si kutegemea uuzaji wa bidhaa nje peke yake kama ilivyokuwa mwanzoni. Kutokana na kupanuka kwa tabaka la kati la China, uwezo wa manunuzi wa wachina wa kawaida umeongozeka.

Hali hii si tu inafanya China iwe kivutio kikubwa kwa makampuni yanayotaka kuwekeza vitega uchumi hapa China, bali pia kwa makampuni na nchi zinazotaka kuuza bidhaa zake kwenye soko la China.

Kwa nchi zetu za Afrika kuongezeka kwa uwezo wa manununzi wa wachina wa kawaida, imekuwa ni faraja kubwa kutokana na kuwa hali hii imepanua mahitaji ya bidhaa za kilimo kutoka kwenye nchi zetu. Kwenye maonesho hayo Tanzania iliweza kutangaza bidhaa zake za kilimo ikiwa ni pamoja na korosho, kahawa, mkonge, chai ufuta na kazi mbalimbali za mikono. Bidhaa ambazo hata Rais Xi Jinping alipotembelea banda la Tanzania kwenye maonesho hayo, alisema kuwa China ingependa kuagiza bidhaa zaidi kama hizo kutoka kwenye nchi za Afrika.

Hamu ya kununua bidhaa za kilimo kutoka kwa nchi za Afrika miongoni mwa wachina inaendelea kuongezeka, hasa kutokana na wachina kuitambua kuwa Afrika ni eneo ambalo bado lina mazingira safi na hali ya hewa nzuri ya kitropiki inayofanya bidhaa zake za kilimo kuwa bora. Hata hivyo changamoto imeonekana kwenye upande wa kuzalisha bidhaa za kilimo na kuzifanya zifikie vigezo vya karantini vya Idara ya Forodha ya China. Imefahamika kuwa asali ya Zambia na maparachini ya Kenya zimeanza kuuzwa kwenye soko la China baada ya kufuata utaratibu huo.

Pamoja na kuwa kwa sasa soko la China linaonekana kuwa endelevu na China imeruhusu bidhaa nyingi za kilimo kutoka nchi za Afrika kuingia kwenye soko lake bila kutozwa ushuru, ruhusa hiyo kwanza inategemea makubaliano kuhusu vigezo vya karantini kati ya serikali ya China na serikali za nchi za Afrika. Jambo la muhimu linalotakiwa kufanywa na wazalishaji na wafanyabiashara wa nchi za Afrika, ni kujua ni bidhaa gani kutoka nchi zao zimekidhi vigezo vya karantini, na ni mchakato gani unatakiwa kufuatwa ili kuweza kuleta bidhaa za kilimo katika soko la China.

Pia inatakiwa kukumbukwa kuwa China ni soko kubwa, na wafanyabiashara wa rejareja wanakuwa na mahitaji makubwa sana. Kwa hiyo kabla ya kufikiria kutumia soko la China, suala la uwezo wa kukidhi kiasi cha mahitaji pia linatakiwa kufikiriwa. Hata hivyo maonesho hayo yameanza kuleta sura mpya ya China duniani. Zamani China ilifahamika kama karakana ya dunia, kwa kuwa vitu vingi vinavyouzwa madukani karibu katika nchi zote duniani vinatoka China. Lakini kupanuka kwa tabaka la kati nchini na utekelezaji madhubuti wa sera ya kufungua milango, kumeifanya China iwe ni soko kubwa duniani kwa bidhaa na huduma.

Kwenye maonesho hayo ya Shanghai, karibu kila nchi duniani ilikaribishwa kushiriki kutokana na uwezo wake, na bidhaa inazoweza kuonesha iwe ni za teknolojia za hali ya juu, malighafi hata mazao ya kilimo. Hali hii inaanza kuipa China sifa ya kuwa soko la dunia na kuchangia maendeleo ya nchi nyingine. Maonesho haya pia yanaonesha sura ya China kuwa mkombozi kwa makampuni mengi ambayo kwa sasa yanasumbuliwa na changamoto za uchumi wa dunia.

Marekani kwa mfano ambayo imeonekana kuendesha kampeni hasi kuhusu China na kuiwekea vizuizi vingi kibiashara, inaonekana kuwa ni moja ya nchi ambazo makampuni yake yanashiriki kwa hamasa kubwa kwenye maonesho hayo. Wizara ya Biashara ya China imetangaza kuwa mwaka huu makampuni 192 ya Marekani yalishiriki kwenye maonesho hayo, yakiwa yameongezeka kutoka makampuni 174 ya mwaka jana.

Kinachotia moyo zaidi ni kuwa maonesho haya sasa yanakuwa ni fursa endelevu kwa nchi mbalimbali zenye mtazamo wazi kuhusu biashara. Kwa nchi za Afrika ambazo uwezo wa kiviwanda bado uko chini, na ambazo zinakabiliwa na vizuizi mbalimbali katika kuuza bidhaa zao za kilimo kwenye mabara mengine duniani, sasa zitakuwa na uhakika wa kuwa na jukwaa kubwa na endelevu kwa ajili ya biashara ya bidhaa za kilimo. Hii ni kutokana na kuwa China imetangaza maonesho hayo yatafanyika kila mwaka kuanzia Novemba 5 hadi Novemba 10.

Kabla ya kumalizika kwa maonesho ya mwaka huu, makampuni 115 ya nchi mbalimbali yalisaini makubaliano ya kushiriki kwenye maonesho hayo ya mwaka kesho. Kama Rais Xi Jinping alivyosema kwenye hotuba ya kuyafungua maonesho hayo, “Soko la China ni kubwa mno, na watu wa nchi zote wanakaribishwa.”

foto
Mwandishi: Fadhili Mpunji

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi