loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Serikali yaokoa bil 51/- tiba ya moyo

Serikali imeokoa Sh bilioni 51.2 baada ya kuboresha Taasisi ya Moyo ya Jakaya (JKCI) kwa kipindi cha miaka minne.

Takwimu za mwaka 2015 za Shirika la Afya Dunia (WHO), zinaeleza zaidi ya watu milioni 17.7 walifariki kutokana na magonjwa ya moyo na mfumo wa damu.

Hii ni sawa na theluthi ya vifo vyote, vinavyotokana na ugonjwa wa moyo na mishipa ya damu, vinavyotokea kwenye nchi zenye uchumi wa chini na ule wa kati.

Mara nyingi magonjwa ya moyo yanaambatana na mishipa ya damu kuwa na tatizo, ambapo moyo hushindwa kufanya kazi, moyo hutegemea damu ambayo hubeba oxygen, madini, vitamin, kinga ya mwili, joto, homoni na vingine vingi.

Kufuatia hali hiyo, HabariLeo ilifanya mahojiano maalum na Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Profesa Mohamed Janabi ambaye amesema kuanzishwa kwa taasisi hiyo, wameweza kuokoa maisha ya watu wengi ndani na nje ya nchi.

Hali hiyo ni tofauti na siku za nyuma ambapoo serikali ilipeleka nje wagonjwa 200 kila mwaka kwa ajili ya matibabu ya moyo.

“Magonjwa ya moyo ndio ilikuwa namba moja kwa kupeleka wagonjwa nje, serikali ilikuwa ikipeleka wagonjwa 400 kwa mwaka, kati yao wagonjwa 200 ni wa moyo… wakati Rais Magufuli anaingia madarakani alikuta kuna deni la mabilioni kwa sababu ya kupeleka watu India,” alisema.

Profesa Janabi amesema mgonjwa mmoja, alikuwa anapelekwa nje na kutibiwa kwa gharama ya dola 30,000 sawa na shilingi milioni 60.

Kwa maana hiyo, kwa wagonjwa 200 kwa kipindi cha miaka minne, wangetibiwa kwa gharama ya shilingi bilioni 51.2.

Alisema kabla ya 2015, Tanzania iliongoza kwa kupeleka wagonjwa nchini India kwa asilimia 90, idadi ambayo ni kubwa. Hata hivyo, tangu kipindi hicho mpaka mwaka huu, wamepunguza idadi ya wagonjwa kuwapeleka wagonjwa nje kwa asilimia 90.

“Tuna namba kubwa ya watu tunaowafanyia upasuaji humu ndani, kwa miaka mitatu kuanzia mwaka 2015 mwishoni mpaka mwaka jana wa 2018 tumepasua wagonjwa 3,000. Kama serikali bado ingekuwa na utaratubu wa kupeleka wagonjwa 200 kwa mwaka wa moyo kwa miaka mitano ilikuwa ni wagonjwa 1,000 sasa kwa wagonjwa 3,000 ingetuchukua miaka 15 kuwamaliza wagonjwa wote. Wagonjwa 8,000 hatujawafanyia upasuaji, wanatibiwa kwa vidonge na dripu, wangeweza kupelekwa India na kufika kule wangeambiwa ni wa vidonge, na dripu mgonjwa mmoja tulikuwa tunampeleka kwa dola 30,000 sawa na shilingi milioni 60,” amesema Profesa Janabi.

Alisema taasisi hiyo inamilikiwa na serikali kwa asilimia 100 na ilianzishwa Septemba 5, mwaka 2015 kwa thamani ya Sh bilioni 26, huku serikali ya China ikitoa Sh bilion 16 na serikali ya Tanzania Sh bilioni 10.

Kwamba kwa miaka minne wameweza kuwaona wagonjwa 291,800 kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara na Tanzania Visiwani pamoja na nchi jirani, ikiwemo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Malawi, Ethiopia, Zambia, Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda na Visiwa vya Comoro.

Alisema tangu taasisi ya JKCI ilipoanzishwa, wana mkataba na Malawi na Rwanda, ambapo wamewaokoa wagonjwa 25 baada ya watalaamu wa JKCI kuweka kambi Kigali, Rwanda. Awali awali Rwanda walikuwa wakipeleka wagonjwa India.

Pia alisema taasisi hiyo imeweza kuokoa maisha ya watanzania ambao wametibiwa na hivi sasa wanaendelea na majukumu yao ya kazi za kila siku.

Kwa kwa kipindi cha miaka minne, walilazwa wagonjwa 14,645, upasuaji wa bila kufungua kifua kwa kutumia tundu dogo kwa mtambo wa Cathlab umefanyika kwa wagonjwa 3,180 na upasuaji wa kufungua kifua na kusimamisha moyo kwa wagonjwa 1,627. Janabi alisema kama wagonjwa wote hao, waliofanyiwa upasuaji wangetibiwa nje ya nchi serikali ingetumia zaidi ya Sh bilioni 144.

Kwa wagonjwa hao kutibiwa hapa nchini, matibabu yao yamegharimu Sh bilioni 72, fedha ambazo zimelipwa kupitia bima zao mbalimbali za matibu, misaada ya wafadhili mbalimbali wa nje, wagonjwa wenyewe kujilipia na Serikali kugharamia matibabu ya wagonjwa wasiokuwa na uwezo wa kumudu gharama za matibabu. Gharama ya kumtibu mgonjwa mmoja nchini ni zaidi ya Sh milioni 29.

Vifaa vya Kisasa

Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Ununuzi na Ugavi wa JKCI, Melkiory Sallema alisema kwa kipindi cha miaka minne taasisi hiyo imeweza kununua mashine za kisasa za matibabu ya moyo, zikiwemo mashine za kuchunguza jinsi moyo unavyofanya kazi (Echocardiograph - ECHO), mashine ya kuchunguza umeme wa moyo unavyofanya kazi (Electrocardiogram-ECG), mashine za Ventilators, Cardiac monitor, Test gears, mashine ya X - Ray.

Thamani ya mashine zote hizo ni Sh 2,178,863,009. Alisema wadau wao kutoka taasisi ya Okoa Moyo wa Mtoto (Save a Child’s Heart - SACH) ya Israel, iliwapatia mashine ya kuchunguza jinsi moyo unavyofanya kazi yenye thamani ya Sh 110,898,000 kwa ajili ya watoto wenye magonjwa ya moyo wanaotibiwa JKCI.

Alisema ndani ya miaka minne, taasisi hiyo imefanikiwa pia kufungua maabara ya kisasa kwa ajili ya kuchunguza magonjwa mbalimbali yanayoambatana na magonjwa ya moyo kama vile uchunguzi wa ini, figo, malaria, sukari, homoni na uchunguzi wa damu mwilini.

Paja/Mkono kuzibua mishipa

Profesa Janabi akifafanua kuhusu mtambo wa Cath lab ambao umenunuliwa kwa gharama ya Sh bilioni tano, alisema matibabu yake wanatumia mshipa wa paja au mkono kuangalia kama moyo umeziba.

“Tunatumia waya zetu mpaka kwenye moyo kujua umeziba kwa asilimia ngapi, tunaingia kitu kama vyuma lakini sio vyuma hasa vyetu ambayo kimoja ni gharama shilingi 3,000,000, tunaingiza na kuzibua kupitia mshipa wa paja au mkono… kuna tunaowawekea betri, tunapasua juu ya ziwa na tunaweka mashine karibu na bega, tunaingia na waya, zile waya ndio zinakuwa zinatuongoza, upasuaji huu wa tundu ndogo unakuja saa 12 asubuhi, jioni tunakuruhusu kuondoka,”alisema

Mfumo wa umeme

Profesa Janabi alisema moyo una mfumo, ambao kama haufanyi kazi sawa sawa, ndio wanamuwekewa ‘pacemaker’ ambao ni mfumo wa umeme uliotengenezwa na binadamu ili kupeleka umeme kwenye moyo.

Wodi Maalum ya Watoto

Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya Moyo kwa Watoto, Dk Sulende Kubhoja alisema kuwepo kwa Chumba cha Uangalizi Maalum (ICU) kwa watoto, kumeongeza idadi ya watoto wanaofanyiwa upasuaji kutoka 20 hadi 40 kwa mwezi, hivyo kupunguza muda wa kusubiri kupata matibabu ya upasuaji wa moyo. “Jengo hili lina vyumba vya kliniki vinne, chumba cha wagonjwa waliopo ICU chenye vitanda nane na wodi yenye vitanda 33.

Tumeweza kutimiza mkakati wetu wa kupunguza msongamano wa wagonjwa na kuwafikia kimatibabu watoto wengi zaidi,” alisema Dk Kubhoja.

Viongozi waikimbilia

Profesa Janabi alisema uwekezaji uliofanywa na serikali ndani ya taasisi hiyo umelipa; na viongozi kutoka ndani na nje ya nchi, wanaenda kutibiwa hapo.

“Viongozi mbali mbali wa serikali na dini wanatibiwa hapa,” alisema

Changamoto

Alisema licha ya Rais John Magufuli kuwapa ghorofa moja Muhimbili, ambayo imefanyiwa matengenezo na ndio imekuwa wodi maalum ya watoto, bado wana changamoto ya vitanda.

Profesa Janabi alisema mpaka sasa wana vitanda 140, ambapo vitanda 100 vipo jengo la JKCI na 40 vipo jengo la watoto kwenye wadi maalum ya watoto wenye matatizo ya moyo.

“Nchi yetu na nchi za jirani zote zinategemea hapa, hii ndio hospitali pekee kubwa ya moyo Afrika Mashariki na Kati, nyingine zote zina vitengo vya moyo, licha ya hatua kubwa tuliopiga kama taasisi lakini bado tunahitaji kuongeza vitanda zaidi,” alisema.

JKCI nyingine Mloganzila

Alisema wapo mbioni kuongeza jengo la pili la taasisi hiyo ya moyo Muhimbili Mloganzila, ambalo litakuwa kubwa kuliko lililopo sasa.

Alisema tayari wamechagua eneo Mloganzila, lenye ukubwa wa mita za mraba 30,000 na litaanza kujengwa rasmi mwaka 2020 na China na serikali watanunua vifaa.

Alisema tayari wamewapeleka mafunzo ya moyo wauguzi na madaktari 36 nje ya nchi na watakaporeja tayari jengo hilo la JKCI Mloganzila litakuwa limekamilika.

Wagonjwa waipa tano

Benedictor Maina ambaye ana umri wa miaka 101, aliyefanyiwa upasuaji na kuwekewa kifaa maalum cha kurekebisha mapigo ya moyo ili yawe sawa, alikuwa akipata maumivu makali sehemu za moyo, kuanguka, kupoteza fahamu na kushindwa kutembea.

Lakini, baada ya kufanyiwa upasuaji huo, hali yake imebadilika na maumivu yamekwisha. Mkazi wa DRC, Nura Babu alisema alipata rufaa kutoka Burundi ya kwenda kutibiwa Uganda na baada ya kufika Uganda, hakuridhika na huduma ya matibabu ya moyo, iliyokuwa inatolewa huko. Alipewa ushauri na daktari wa kuja nchini Tanzania.

foto
Mwandishi: Vicky Kimaro

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi