loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Majaliwa- Fanyeni mazoezi, kuleni mboga, matunda

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa ametaka wananchi kubadili tabia, kwa kufanya mazoezi na kuongeza ulaji wa mboga, matunda na kupunguza mafuta, chumvi na sukari.

Ametoa kauli hiyo jijini Dodoma alipokuwa akizindua Mpango Mkakati wa Kukabiliana na Magonjwa Yasiyoambukiza nchini.

“Tujenge utamaduni wa kufanya mazoezi angalau dakika 30 mara tatu kwa kila wiki, sekretarieti za mikoa na mamlaka za serikali za mitaa ziendeleze utaratibu wa ufanyaji mazoezi uliozinduliwa na Makamu wa Rais,” alisema.

Alisema kwa bahati mbaya, watu wameanza kusahau mpango wa kufanya mazoezi na kuwataka kurudisha utaratibu.

“Wananchi wahamasishwe kufanya mazoezi kila Jumamosi, watu waache kutumia magari kwa saa tatu hadi tano kila siku, hata ukiwa nyumbani fanya mazoezi chumbani, ruka kichura, zunguka coffee table dakika 20 hadi 30,”alisema.

Aliagiza halmashauri nchini kutenga na kuendeleza na maeneo ya wazi kwa kila kata au mitaa ili wananchi watumie kufanya mazoezi. Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alisema watanzania wengi wanaugua magonjwa hayo wanaishia kwa waganga wa kienyeji.

“Wizara imeweka mikakati madhubuti ya kukabiliana na vichocheo vya magonjwa hayo, kuna changamoto ya kuwapata wanaume kwenye huduma za afya sio kwenye Ukimwi bali na magonjwa mengine,” alisema.

Takwimu zinaonesha kuwa tatizo la magonjwa hayo, linaongezeka kwa kiwango kikubwa nchini ambapo kwa kipindi cha miaka miwili kuna ongezeko la asilimia 24 la watu wanaoumwa maradhi hayo.

Pia takwimu za Shirika la Afya Duniani(WHO) kwa mwaka 2016, zinaonesha kwamba magonjwa hayo, yanachangia zaidi vifo takribani milioni 41 sawa na asilimia 71 kwa mwaka.

Makadirio yanaonesha kwamba gharama za makadirio ya huduma kwa wagonjwa yasiyoambukiza, itafikia asilimia 75 ya mzigo wote wa bajeti ya afya hapa nchini, ambapo ugonjwa wa kisukari pekee utagharimu dola za Marekani bilioni 465, sawa na asilimia 11 ya bajeti yote ya afya.

Ugonjwa wa figo ndani ya wiki moja, mgonjwa itamgharimu zaidi ya Sh 900,000 na hivyo kutumia Sh milioni 3.6 kila mwezi, sawa na wastani wa Sh milioni 43 kwa mwaka mzima, ambazo Mtanzania wa kawaida hana uwezo wa kumudu.

foto
Mwandishi: Magnus Mahenge, Dodoma

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi