loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Chama kujisafisha msingi kupambana na ufisadi China

MWAKA 1945 wakati hayati Mwenyekiti Mao Zedong na wenzake wa Chama cha Kikomunisti cha China hawajapata mafanikio ya mapinduzi ya China na kuingia madarakani, msomi mmoja wa China alimwuliza swali Mwenyekiti Mao akisema,

“Kwenye historia ya China tunaona kila utawala wa enzi ya kifalme ulipita njia ya namna moja ya kukua, kustawi, kushuka, kuzorota hadi kufa, inaonekana hii ni historia ya mzunguko wa utawala. Je, chama chako kinaweza kuvunja mzunguko huu?”

Hayati Mao alimjibu, “Ndiyo, tumepata njia tofauti ambayo ni demokrasia, kwamba serikali iliyo chini ya usimamizi wa wananchi haifanyi uzembe, na utawala unaoshirikisha kila mwananchi hautakufa.”

Miaka minne baada ya mazungumzo hayo, Chama cha Kikomunisti kilipata ushindi wa mapinduzi na kuanzisha Jamhuri ya Watu wa China.

Hadi sasa ni miaka 70 tangu chama hicho kingie madarakani nchini China, na katika muda wote wa utawala wake kazi ya kupambana na ufisadi imepewa uzito mkubwa.

Kama alivyosema hayati Mao Zedong, nia na hatua za chama tawala kujisafisha ni msingi wa kuhakikisha mafanikio katika mapambano hayo.

Kesi ya kwanza ya ufisadi iliyotokea muda mfupi baada ya Jamhuri ya Watu wa China kuanzishwa, ilihusisha makada wawili waandamizi wa Chama waliogunduliwa kufanya ubadhirifu wa fedha ambazo thamani yake ni sawa na dola za kimarekani laki 2.5 za hivi leo.

Wawili hao waliokuwa viongozi wa mji walijiunga na chama katika miaka ya 1930 na kutoa mchango mkubwa katika vita dhidi ya uvamizi wa Japan na ukombozi wa taifa.

Wakati kesi yao inasikilizwa, kulikuwa na ombi la kuwasamehe kutokana na nafasi yao muhimu katika chama na mchango mkubwa kwa taifa. Hata hivyo utetezi huo haukukubaliwa na walifukuzwa uanachama na kuhukumiwa adhabu ya kifo.

Hayati Mao alisema hiyo ni adhabu inayostahili kwa kuwa inaweza kuokoa maelfu ya makada ambao wanaweza kufanya makosa kama hayo.

Licha ya hatua kali kama hiyo kupunguza sana ufisadi, vitendo vya ufisadi vilianza kujitokeza tena katika miaka ya 1980 katika ngazi mbalimbali za jamii baada ya China kuanza kutekeleza sera ya mageuzi na kufungua mlango, na uchumi kuanza kukua kwa kasi.

Katika juhudi za kupata maendeleo ya kiuchumi, baadhi ya maofisa wa serikali walisahau miiko na nia ya kutumikia umma, na kuanza kujichotea pesa kwa kutumia madaraka yao.

Chama cha Kikomunisti kilitumia mbinu mbalimbali kupambana na ufisadi, lakini matokeo yake hayakuwaridhisha wananchi. Ingawa hatuwezi kusema ufisadi ulifikia hatua ya kukithiri, lakini ulifikia hali ya kuwafanya watu wawe na malalamiko makali na kutaka hatua kali zichukuliwe ili kurudisha miiko na maadili ya uongozi.

Malalamiko hayo yaliwafanya viongozi wa China kutafakari kwa makini, ili kupata njia ya kuondoa tatizo hilo kutoka kwenye mzizi wake.

Lakini kazi ya kung’oa mzizi wa ufisadi sio rahisi nchini China, kwa sababu mafisadi ni wajanja kiasi kwamba serikali inatakiwa kuwa hatua moja mbele kuwatambua, kuwakamata na kuwashughulikia.

Kuna ufisadi unaofichika kiasi kwamba uchunguzi wa kawaida hauwezi kuugundua. Ufisadi unafanyika kiasi kwamba jina la fisadi halionekani popote, kwa kuwa unafanyika kupitia mtu wa tatu iwe ni mwanafamilia, rafiki au kimada.

Ufisadi kama huu inakuwa vigumu kuutambua kwa njia za kiuhasibu na kufuatilia akaunti. Kuna wengine waliotorosha mabilioni ya pesa nje ya nchi, wakiamini kuwa idara za uhasibu za China haziwezi kwenda kuwakagua nje ya nchi, na mkono wa sheria za China hauwezi kuwafikia kama wakitoroka nje ya nchi.

Kuna ofisa mmoja wa mkoa wa Mongolia ya Ndani, alipokea rushwa iliyofikia thamani ya zaidi ya dola za Kimarekani milioni 20, na kuficha pesa taslimu kwenye ndoo za kunyweshea maji kuku.

Hali kama hizi zilifanya mapambano dhidi ya ufisadi yawe magumu na kuhitaji mbinu mpya. Mwaka 2012 Chama cha Kikomunisti cha China kiliitisha Mkutano Mkuu wa 18 uliowachagua Katibu Mkuu Xi Jinping na kundi jipya la viongozi.

Katika mikutano ya ngazi mbalimbali, Xi Jinping alisisitiza umuhimu wa chama tawala kujisafisha na kujiendesha kwa nidhamu kali katika mapambano dhidi ya ufisadi.

Alitaja umuhimu wa kusimamia na kuweka mpaka wa utekelezaji madaraka, na kudhibiti madaraka ndani ya utaratibu, kuanzisha na kukamilisha taratibu za adhabu zinazowafanya maofisa wasithubutu kufanya ufisadi, taratibu za udhibiti zinazowafanya wasiweze kufanya ufisadi, na taratibu za uhakikisho zinazowafanya wasitake kufanya ufisadi.

Na alisisitiza kuwa wote wanaokiuka nidhamu ya chama kutoka ngazi ya taifa hadi ngazi ya chini kabisa wanachukuliwa hatua. Xi Jinping alipotaja kupambana na mapapa na vidagaa wa ufisadi, alisema “chui” na “nzi” (akiwa na maana) wote hawatapona.

Na kauli yake ilitekelezwa kivitendo. Moja ya hatua hizo ni kuwataka maofisa wa serikali katika ngazi zote kutangaza mali zao na za familia zao kila mwaka.

Mali hizo ni pamoja na akiba za benki, hisa, nyumba n.k. Hata kama mke au mume na watoto wa maofisa wanafanya biashara pia inatakiwa kuripotiwa. Na ni mwiko kwa ofisa mwenyewe kuendesha kampuni au kufanya biashara yoyote.

Ripoti hizo zinakaguliwa na idara ya nidhamu, na maofisa waliodanganya au kuficha habari kuhusu mali zao wanachukuliwa hatua za kinidhamu, na kunyimwa fursa za kupandishwa cheo.

Wale walitambulika kuwa wabadhirifu walifukuzwa na chama na kesi zao kukabidhiwa kwa idara za sheria.

Katika juhudi za kujisafisha, maofisa kadhaa waandamizi wa Chama cha Kikomunisti, maofisa waandamizi wa idara za serikali na hata wa jeshi wamekamatwa na kuchukuliwa adhabu kali.

Takwimu zinaonesha kuwa, toka mwaka 2017, maofisa waandamizi wa ngazi ya mawaziri zaidi ya 70 walifanyiwa uchunguzi, huku kesi zaidi ya laki 2.3 kuhusu matumizi mabaya ya madaraka zilichunguzwa na watu laki 3 walichukuliwa hatua.

Kutokana na kwamba ni vigumu kufanya uchunguzi, kupata ushahidi na kushirikisha idara za sheria za nchi tofauti, awali mafisadi wengi wa China walitumia ujanja wa kukimbilia nje ya nchi ili kukwepa adhabu.

Kutokana na hali hii, China ilianzisha kampeni maalum inayoitwa “Operesheni wavu wa angani” (Operation skynet) ili kuwasaka na kuwaadhibu mafisadi waliokimbia nchi za nje.

Operesheni hii iliyoanza mwaka 2015 inashirikisha nguvu za idara mbalimbali zikiwemo Polisi, Idara ya Uendeshaji Mashtaka, Wizara ya Mambo ya Nje, na taasisi za fedha. Hadi hivi sasa imesaidia kuwarudisha mafisadi 6,690 pamoja na dola za kimarekani bilioni 2.2.

Zaidi ya hayo, China na nchi nyingine 77 zimesaini makubaliano 55 ya kurudisha wahalifu na makubalino 64 ya kusaidiana kisheria.

Hatua hizo zenye mafanikio zinaungwa mkono na kukaribishwa na wananchi wa China, na zimerudisha imani ya wananchi kwa chama tawala. Hata hivyo kama Rais Xi Jinping wa China alivyosema, kazi ya Chama kujiendesha kwa nidhamu kali na kupambana na ufisadi haina mwisho.

foto
Mwandishi: Fadhili Mpunji

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi