loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Uvinza yapata mwekezaji kiwanda cha mawese

HALMASHAURI ya Wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma, imepata mwekezaji wa kiwanda cha mawese ambaye tayari amewasilisha barua ya kuanza kununua malighafi za zao hilo.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Masumbuko Kichego amesema hayo wakati wa ziara ya Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), Dk. Geoffrey Mkamilo aliyoifanya katika Mkoa wa Kigoma ikiwa ni ufuatiliaji wa agizo la Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kuhusu upandaji wa mbegu bora za zao hilo.

Amesema kupatikana kwa mwekezaji huyo kutaongeza tija kwa wakulima wa zao hilo kwa kuwa watakuwa na sehemu ya kupeleka mazao yao baada ya kuvuna.

“Kupatikana kwa mwekezaji huyu wilaya itakuwa na connection nzuri kwa kuwa tayari tuna mbegu za kisasa, kuna mkulima anazalisha mbegu za kisasa, kuna mnunuzi anayenunua hapahapa ambaye ataipeleka ku process hiyo product kwa hiyo chain itakuwa imekamilika,” amesema.

Kichego ameiomba TARI iongeze kasi ya kuzalisha mbegu kwa kuwa wana maeneo mengi ya kupanda michikichi.

Amesema mbali na kupata miche 35,000 kutoka TARI kabla ya hapo walinunua miche 3,000 kutoka taasisi binafsi ya Seed Change inayozalisha mbegu bora ya Tenera ya michikichi iliwagharimu zaidi ya sh. milioni 10/- na kwamba, gharama hiyo ilikuwa ni kubwa kwao.

Kwa mujibu wa Kichego wanajipanga kuwapa wakulima miche ya michikichi itakapokuwa tayari kwa lengo la kuinua uchumi wa mkoa huo kwa kupunguza uagizaji mafuta ya kula nje ya nchi.

Kaimu Mkurugenzi wa Kituo cha Utafiti wa Michikiki Kihinga mkoani Kigoma, Dk. Filson Kagimbo amesema kituo hicho kinafanya utafiti wa zao la mchikichi kwa kuwa kilimo hicho nchini kina changamoto mbalimbali ikiwemo upungufu wa mbegu za kisasa aina ya Tenera.

“Wakulima zaidi ya asilimia 90 wanalima mbegu ya kienyeji inayoitwa dura ambayo inatoa mafuta kidogo kulinganisha na mbegu ya kisasa aina ya tenera.

“Hizi mbegu za kisasa aina ya tenera upatikanaji wake ni kama asilimia 10 na za kienyeji ni asilimia 90 hivyo kituo kimeweka kipaumbele cha kuzalisha mbegu nyingi za kisasa ili kisambaze kwa wakulima waweze kuzilima,” amesema.

Ametaja changamoto nyingine ni kuzeeka kwa miti ya zao hilo kwani mingi ina zaidi ya miaka 50, lakini uzalishaji wenye tija unatakiwa miti iwe na miaka minne mpaka 30.

“Sasa miche mingi ina zaidi ya miaka 50 na mingine mpaka miaka 100 inapofikia umri huo uzalishaji unakuwa mdogo sana kinachotakiwa hivi sasa wakulima waing’oe hiyo ya zamani na kuipanda mipya,” amesema.

Amesema jitihada za kufufua zao hilo zinafanyika ili kupunguza uagizwaji wa mafuta ya kula nje ya nchi kwa kuwa michikichi inatoa mafuta mengi kwa eka ikilinganisha na mazao mengi yanayozalisha mafuta.

Mkurugenzi Mkuu wa TARI, Dk. Mkamilo anafanya ziara mkoani Kigoma kuangalia uzalishaji wa zao hilo umefikia hatua gani tangu Waziri Mkuu Majaliwa alipotoa agizo la kupanda mbegu za kisasa.

Kwa mujibu wa Dk. Mkamilo awali kulikuwa na upotevu mkubwa wa fedha za serikali kutokana na mafuta ya kula kuagizwa nje ya nchi, na kwamba, TARI imeanza kuzalisha kwa wingi mbegu hizo wakisaidiana na kampuni binafsi ili kuondoa changamoto hiyo kwa taifa.

SHIRIKA  la Madini Nchini (Stamico) litaanza ...

foto
Mwandishi: Lucy Ngowi, Kigoma

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi