loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Bei ya sukari yatarajiwa kupungua

DALILI za bei ya sukari kushuka nchini zimeanza kuonekana kutokana na mipango ya kuongeza uzalishaji iliyowekwa ikiwamo uanzishaji wa viwanda vipya.

Wakati sekta ya sukari ikiwa na viwanda vitano, vinavyoendelea na uzalishaji, uhamasishaji wa uwekezaji wa ndani, umezaa matunda kutokana na miradi mingine mipya kutarajiwa kuongeza uzalishaji.

Viwanda vikubwa vilivyopo ni Kilombero, Mtibwa, Kagera, TPC na cha kati ambacho ni Manyara, ambavyo msimu wa mwaka 2019/2020 tangu Juni hadi Septemba mwaka huu, jumla ya tani 143, 148.49 za sukari zilikuwa zimezalishwa.

Kiasi hicho ni sawa na asilimia 39 ya malengo ya uzalishaji wa tani 378,449.

Akizungumza na gazeti hili hivi karibuni katika mahojiano maalumu, Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Uwekezaji, Profesa Joseph Buchwashaija alisema kawaida bei ya bidhaa ikiwamo sukari, hutegemea hali ya ugavi na uhitaji wake.

“Kwa kuzingatia mipango ya kuongeza uzalishaji iliyowekwa na viwanda hapa nchini na kuanzishwa kwa viwanda vipya ugavi wa sukari sokoni utaongezeka hivyo kusababisha bei ya bidhaa kushuka,” alisema Profesa Buchwashaija.

Alisema mahitaji ya sukari mwaka 2019/20 yalikadiriwa kuwa tani 710,000. Kati ya hizo, tani 545,000 ni sukari ya matumizi ya nyumbani na tani 165,000 ni kwa matumizi ya viwandani.

Kutokana na uwiano hasi kati ya uzalishaji na mahitaji ya sukari nchini, serikali imeweka utaratibu wa kuingiza sukari baada ya mapitio ya uhitaji halisi na kutoa vibali vya kuingiza nchini.

Katibu mkuu alitaja miradi mbalimbali inayotarajiwa kutekelezwa nchini na kuongeza uzalishaji ikiwamo Mkulazi (I) na Mkulazi (II) chini ya Kampuni Hodhi ya Mkulazi iliyoanzishwa Septemba 2016.

Kwa pamoja, miradi hiyo miwili inatarajiwa kuzalisha tani za sukari 250,000 kwa mwaka.

Mradi wa Mkulazi I unatekelezwa katika shamba Na. 217 lililopo eneo la Mkulazi, Morogoro Vijijini na kiwanda kitazalisha tani 200,000 za sukari kwa mwaka.

Mkulazi II unatekelezwa katika shamba la Mbigiri, Kilosa na utazalisha tani za sukari 50,000 kwa mwaka. Mkulazi II una jumla ya hekta 60,103 ambazo kati yake, hekta 28,000 zimethibitika kufaa kwa kilimo cha miwa.

Mradi mwingine ni wa kiwanda cha sukari cha Bagamoyo mkoani Pwani ambacho mwaka 2021 kinategemewa kuzalisha tani 350,000 za miwa , kitasindika tani 35,000 za sukari kwa awamu ya kwanza.

Kiwanda kinamilikiwa na kampuni ya Sukari ya Bagamoyo inayomiliki eneo la hekta 10,000 kwa ajili ya kilimo cha miwa.

Eneo la hekta 50 limepandwa miwa ya mbegu, hekta 100 linaendelea kupandwa miwa ya mbegu itakayopandwa kwenye eneo la hekta 2,000 litakalotumika kuzalisha tani 350,000.

Vile vile Profesa Buchwashaija alisema kiwanda cha sukari cha Chamwino mkoani Dodoma, kinatarajiwa kuzalisha tani 4000 za sukari kwa mwaka.

Mkoani Geita, uainishaji wa mashamba ulifanyika katika Tarafa ya Butundwe na Bugando na kubainika takribani hekta 508 zinafaa kwa kilimo cha miwa kwa ajili ya kiwanda cha sukari cha Geita.

Kampuni ya Kigoma Sugar ilisajiliwa na kuanza taaribu za kuomba ardhi kwa ajili ya uwekezaji wa kilimo cha miwa na kiwanda cha sukari wilayani Kasulu na hekta 37,000 zinafaa kwa uwekezaji.

IKIWA fomu moja ya kuomba ridhaa ...

foto
Mwandishi: Stella Nyemenohi

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi