loader
Picha

Mikoa 3 kutopiga kura serikali za mitaa

Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) imesema mikoa mitatu haitafanya uchaguzi wa serikali za mitaa kwa kuwa wagombea kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) wamepita bila kupingwa.

Naibu Waziri wa wizara hiyo, Mwita Waitara amesema leo jijini Dar es Salaam kuwa, kati ya halmashauri za wilaya 184 nchini, 90 hazifanyi uchaguzi huo Novemba 24 mwaka huu kwa kuwa wagombea wamepita bila kupingwa.

“Katika mikoa 26 ya hapa bara, kwa taarifa ambazo tumeshapokea mpaka leo asubuhi mikoa mitatu inaonekana kwamba wagombea wa Chama Cha Mapinduzi wamepita bila kupingwa kwa hiyo kuanzia siku ya uteuzi wao ni viongozi halali na wasimamizi wameshawateua, hakuna haja ya kampeni katika eneo hilo” ameyasema hayo wakati anazungumza kwenye kipindi cha Asubuhi Hii kinachorushwa na kituo cha redio cha TBC Taifa cha Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC).

Wakati akizungumza na Habarileo leo mchana Waitara ameitaja mikoa ambayo haitafanya uchaguzi kabisa kuwa ni Katavi, Tanga, na Ruvuma.

“Mahalali ambako mgombea alikuwa peke yake na amepita bila kupingwa kazi ya msimamizi ni kumtangaza na baada ya hapo atasubiri baada ya tarehe 24 ataapishwa na ataanza majukumu yake kwa hiyo hakuna habari ya kampeni lakini mikoa 23 itakuwa na mchakato wa uchaguzi”amesema Waitara.

Kwa mujibu wa kiongozi huyo hata katika mikoa hiyo 23 uchaguzi utafanyika kwenye baadhi ya maeneo.

Amesema, kuna vitongoji 64,000 lakini 3,432 tu vitafanya uchaguzi na kuna mitaa zaidi ya 4,000 lakini mchakato wa uchaguzi utakuwa kwenye mitaa 188 tu. Waitara amesema, Tanzania bara kuna vijiji 12,000 lakini mchakato wa uchaguzi utakuwa kwenye vijiji 1,000.

Amevituhumu baadhi ya vyama kuwa vimewatisha wanachama wao wakilazimisha wajitoe kwa kuwatishia kuwafukuza uanachama.

Amesema Serikali haiingili michakato ndani ya vyama, na kwamba, vyama havitoi maagizo kwa Serikali bali kwa wanachama wake.

Waitara amesema, kwa mujibu wa kanuni anayestahili kujitoa ni mgombea na si chama cha siasa, na kwamba, vyama hivyo vilipewa kanuni hizo Aprili mwaka huu jijini Dodoma hivyo ama hawataki kuzisoma au havisemi ukweli.

“Katika mikoa hii mitatu ambayo haifanyi uchaguzi kabisa, naposema mkoa ninamaanisha kwamba yaani hakuna mahali popote uchaguzi utafanyika isipokuwa mgombea wa Chama Cha Mapinduzi wamepita bila kupingwa maana yake hakuna kitongoji wala mtaa wala kijiji ambacho watakuwa na uchaguzi maana yake hawa wameandika barua wagombea wenyewe”amesema.

WAKURUGENZI wawili wa Kampuni ya Tanzanite One Mining Ltd ya ...

foto
Mwandishi: Basil Msongo

1 Comments

  • avatar
    Fenance Paulo
    18/11/2019

    Comment Inadhihirisha wazi kuwa Chama Cha mapinduzi CCM Ni Chama kinachokubalika na chenye sets nzuri na ilani inayotekelezeka kwa wananchi na pia kimekidhi matarajio, matamanio na shauku kubwa Sana ya wananchi wengi wa Tanzania

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi