loader
Dstv Habarileo  Mobile
Majaliwa aagiza kuchunguzwa zilipo bilioni 40/- za korosho

Majaliwa aagiza kuchunguzwa zilipo bilioni 40/- za korosho

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amemuagiza Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Julius Mtatiro ahakikishe anaondoka na Mkurugenzi wa Bodi ya Korosho hadi Tunduru ili wakahakiki ni kwa nini wakulima hawajalipwa.

Alitoa agizo hilo jana mchana wakati akifungua kongamano la siku moja la wakandarasi na wazabuni wa mikoa ya Kusini, lilioandaliwa na benki ya CRBD, mjini Mtwara. “Nimefurahi kusikia minada ya korosho inakwenda vizuri. Lakini sijafurahia habari ya Tunduru. Mheshimiwa Rais aligiza Sh bilioni 40 zipelekwe kwa wakulima. Na ninajua kwamba zimeshalipwa.

Sasa ni kwa nini wakulima bado wanadai? “Ukitoka hapa kwenye mkutano nenda pale jengo la Bodi ya Korosho. Ondoka na Mtendaji Mkuu wake, mwende Tunduru akafuatilie ni kwa nini malipo ya mwaka jana hayajalipwa hadi sasa.

“Nataka ufuatilie fedha zimekwama kwa nani. Kaimu Mkuu wa Mkoa ukigundua wanaokwamisha ni viongozi wa Ushirika, shughulika nao hukohuko kama ambavyo umekuwa ukifanya,” alisisitiza.

Akizungumzia kuhusu kongamano hilo ambalo kaulimbiu yake ni “Pamoja nawe kukuza uchumi”, Majaliwa aliwataka wakandarasi hao baada ya kupata elimu kidogo kuhusu shughuli za benki hiyo, kwenda kwenye halmashauri zao na kutafuta kazi.

“Serikali inajenga miradi mikubwa kama vile Bwawa la kuzalisha umeme kwa nguvu ya maji la Mwalimu Nyerere, bomba la mafuta la kutoka Hoima hadi Tanga na miradi ya maendeleo kama ile ya barabara, reli, ujenzi wa hospitali, madarasa na nyumba za walimu. Miradi yote hii inawatarajia ninyi wakandarasi mkaijenge” alisema.

Alisema Serikali imeendelea kuimarisha na kusogeza karibu kwa wananchi huduma za jamii, ikiwemo ukarabati wa miundombinu ya kufundishia na kujifunzia katika ngazi zote za elimu.

“Katika kipindi cha Januari hadi Juni 2019, kwa shule za msingi, serikali imejenga madarasa 473, matundu ya vyoo 1,405, nyumba za walimu 24 na kukamilisha maboma ya madarasa 2,760. Kwa shule za sekondari, serikali ilijenga madarasa 465, matundu ya vyoo 736, nyumba za walimu 23 na kukamilisha maboma ya madarasa 2,392,” alisema.

Waziri Mkuu alitoa wito kwa viongozi na watendaji, wazingatie utekelezaji wa Sheria ya Ununuzi wa Umma, kwa kutenga zabuni zenye thamani ya chini ya Sh bilioni 10 kwa ajili ya wazabuni Watanzania ili kuwajengea uwezo na kushiriki katika zabuni.

Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na washiriki wa kongamano hilo, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Gelasius Byakanwa alisema hadi sasa jumla ya tani 67,000 za korosho, zimeuzwa mkoani humo kupitia minada mitatu.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/602a909906b28249d46f2081b6b5f2b7.jpg

ALIYEKUWA Mbunge Mteule wa Jimbo la Konde ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Maalumu, Mtwara

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi