loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

‘Msitu umetutoa kwenye mapato sifuri hadi mamilioni’

“MPAKA mwaka 2016 kabla ya kupokea mradi huu kijiji chetu kilikuwa kina mapato sifuri. Lakini mwaka jana tulipoanza uzalishaji, tukapata zaidi ya shilingi milioni 63,” anasema Redemptor Matola, Mtendaji wa kijiji cha Diguzi kilichoko kata ya Matuli, Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi ya kijiji hicho, Chilunda Imani anasema: “Maendeleo ambayo tumepata kwa mwaka mmoja kupitia mradi huu wala hatuhitaji shilingi milioni 50 zilizoahidiwa kupewa kila kijiji na Rais John Magufuli.”

Mhasibu wa Kamati ya Maliasili ya kijiji hicho, Angelina Mugasa anasema: “Kwa kweli mwanzoni hatukuupenda kabisa huu mradi, lakini kwa sasa kila mtu anaona manufaa yake.”

Mradi gani unaozungumzwa? Mradi wa Kuleta Mageuzi katika Sekta ya Mkaa nchini (TTCS) maarufu kama ‘Mkaa endelevu’ unatekelezwa kama shamba darasa katika vijiji 30 katika wilaya za Morogoro, Kilosa na Mvomero mkoani Morogoro. Mradi huu umejengwa katika dhana kwamba Watanzania wengi wataendelea kutumia mkaa kama nishati ya kupikia kwa miongo kadhaa na hivyo ni muhimu kuwa na uzalishaji endelevu wa nishati hiyo.

Mradi unaendeshwa na asasi zisizo za kiserikali za Shirika la Kuhifadhi Misitu ya Asili Tanzania (TFCG), Mtandao wa Jamii wa Usimamizi wa Misitu Tanzania (MJUMITA) na Shirika la Kuendeleza Nishati Asilia (TaTEDO) kwa ufadhiliwa na Shirika la Maendeleo na Ushirikiano la Uswisi.

Wiki iliopita mashirika hayo yalitoa semina kwa waandishi wa habari na wahariri kuhusu mradi huo, mafanikio pamoja na changamoto. Baada ya semina, waandishi na wahariri wakatembelea kijiji cha Diguzi ambacho ni moja ya vijiji vinavyotekeleza mradi huo ili kujionea hali halisi.

Ofisa Mawasiliano wa TFCG, Bettie Luwuge, anasema hiyo ni semina ya tatu kutolewa kwa waandishi wa habari, ikilenga kuwawezesha kujua na kuona namna wanakijiji wanavyonufaika na rasilimali za misitu pale inaposimamiwa vyema. Nini kinafanyika katika mradi? Kupita mada alioiwasilisha kwa waandishi wa habari na wahariri, Ofisa Ujengaji Uwezo wa TFCG, Simon Lugazo, anasema mradi wa TTCS unaanza kwa kijiji kuanzisha mpango bora wa matumizi ya ardhi.

“Katika hatua hii ardhi ya kijiji hupimwa, na kisha kutenga eneo kwa ajili ya makazi, eneo la kilimo, eneo la malisho na eneo la msitu wa kijiji,” anasema.

Anasema ndani ya eneo la msitu lililotengwa, asilimia 10 hadi 30 ya msitu wa kijiji ndiyo inayotengwa kwa ajili ya kuvuna mkaa kwa miaka yote kwa njia endelevu. Kinachofanyika ndani ya eneo lililotengwa kwa ajili ya uvunaji mkaa huku asilimia 70 ya msitu ikiwa haiguswi, anasema ni kutenga tena vitalu vya ukubwa wa mita 50 kwa 50 kwa njia ya picha za satellite na kupimwa kwa teknolojia ya GPS.

Anasema vitalu huvunwa kwa njia ya kuruka kitalu kimoja kwenda kingine kwa usimamizi wa Kamati ya Maliasili ya kijiji. “Kikivunwa kitalu A, kinarukwa kitalu B bila kuvunwa hadi C na hivyo kitalu kinachorukwa huja kuvunwa tena baada ya miaka 24 ambapo unakuta vile visiki vilivyokatwa vimechipuka na kuwa miti mikubwa kwa ajili ya kuvunwa tena na hivyo uvunaji unakuwa endelevu.

Miti hukatwa kwa kuacha shina ili liweze kuchupua. “Miti inayofaa kwa mbao, miti yenye viota vya ndege au mapango ya wanyama na iliyo katika vyanzo vya maji ndani ya kitalu haivunwi. Halikadhalika kwenye kitalu kinachovunwa miti michache huachwa ili kutoharibu ikolojia ya kitalu,” anasema. Lugazo anasema pia uchomaji mkaa unafanywa kwa kutumia tanuri kichuguu lililoboreshwa ambalo hutoa mkaa mwingi na bora.

Kilimo chaongoza kumaliza miti Mkurugenzi Msaidizi wa TFCG, Emmanuel Lyimo, aliwasilisha kwa waandishi wa habari na wahariri kuhusuuchunguzi uliofanyika hivi karibuni na kuonesha kwamba kilimo, hususani cha kuhamahama, ndicho kinamaliza misitu ya Tanzania. Anasema takwimu zilizopo zinaonesha kwamba kila mwaka hekta zipatazo 469,000 za misitu Tanzania zinafyekwa kila mwaka sawa na mara tatu ya eneo la Mji wa Unguja.

Kwa mujibu wa utafiti huo ambaye yeye alishiriki pia, Lyimo anasema asilimia 89 ya upotevu wa misitu nchini inatokana na shughuli za kilimo. Anasema kwa mujibu wa utafiti huo, uvunaji mkaa huchangia uharibifu wa misitu kwa asilimia saba, ufugaji na moto kwa asilimia tatu huku ufyekaji misitu kwa ajili ya uanzishwaji wa mashamba mapya ya miti ukichangia kwa asilimia moja.

Anasema utafiti wao uliofadhiliwa na Mfuko wa Critical Ecosystem Partnership Fund (CEPF) ulihusisha mahojiano na wananachi katika kujibu swali la nini kinasababisha uharibifu wa misitu sambamba na utumiaji wa picha za satellite na upigaji wa picha za kawaida katika maeneo 120 yanayohusisha wilaya 62 na mikoa 22 tofauti tofauti nchini.

Diguzi wanavyonufaika na msitu wao Akitoa taarifa ya mradi kwa waandishi wa habari, Mwenyekiti wa Kamati ya Maliasili ya Kijiji cha Diguzi, Jonathan Biko, anasema kupitia kipato walichopata kutokana na mkaa endelevu wameweza kujenga choo katika ofisi ya kijiji na kuweka umeme jua kwenye zahanati ya kijiji. Mengine yaliyofanywa na mapato hayo anasema ni ukarabati wa tangi la maji, ujenzi wa nyumba ya mwalimu na pia kulipa posho kwa kamati ya ulinzi kwa ajili ya kufanya doria kwenye msitu.

Anasema mwaka huu wa 2019, kijiji kinatarajia kupata zaidi ya Sh milioni 60 kutokana na mradi huo wa mkaa endelevu. Anafafanua kwamba kijiji kinapata pesa hizo kutokana na ushuru wanaotoza wafanyabiashara wanaokwenda kununua mkaa uliozalishwa kwa njia endelevu kijijini hapo.

“Zamani, kabla ya mradi huu kuja tulikuwa tunajivunia tu holela tena kwa njia ya wizi. Kwanza mapato yalikuwa madogo kwa sisi wenyewe wavunaji na kijiji kilikuwa hakipati manufaa yoyote,” anasema Biko ambaye pia ni mchoma mkaa.

Biko anasema baada ya wananchi kuona faida ya mradi, sasa ndio walinzi wakubwa wa raslimali za misitu katika kijiji chao. Kwa upande wake, Mtendaji wa kijiji, Redemtor, anasema: “Maisha ya kabla ya mradi yalikuwa magumu kwani ofisi ya kijiji ilikuwa haina akiba yoyote hata fedha ya kununulia karatasi. Kwa ujumla mkaa endelevu umetutoa kwenye utegemezi,” anasema.

Mtendaji huyo amesema kutokana na mradi huo kuonesha matokeo chanya anaomba Serikali kusaidia katika kuuendeleza pale wafadhili watakapofikia kikomo. Kuhusu changamoto, Mwenyekiti wa Kamati ya Maliasili ya Kijiji, Biko, anasema ni pamoja na kutumia vifaa duni vya ulinzi na nyingine ni wafugaji kuingiza mifugo yao kwenye misitu.

“Lakini bado pia kuna changamoto ya watu ambao bado hawajaelewa vizuri kuhusu huu mradi,” anasema.

Mkaa endelevu ni mali Takwimu za Msingi za Hewa Ukaa (Forest Reference Emission Level-FREL)’ za mwaka 2016 zinaonesha kwamba zaidi ya tani milioni 2.3 za mkaa zinatumika kwa mwaka hapa nchini. Kwa mujibu wa takwimu hizo, mchango wa sekta ya mkaa kwenye uchumi wa nchi ni takribani ni Sh trilioni 2.2 lakini mapato yanayopotea kwa mwaka ni Sh bilioni 220.

Inaelezwa kwamba, pamoja na mkaa kupuuzwa, kipato kinachotokana na uvunaji wa raslimali hiyo kinazidi kiasi kinachopatikana kutoka kwenye mazao yotete makuu nchini kama korosho, mahindi, mpunga na kadhalika.

Takwimu hizo zinaonesha pia kwamba mpaka sasa asilimia 96 ya kaya zote hapa nchini zinatumia nishati ya kuni na mkaa kwa ajili ya kupikia huku katika jiji la Dar es Salaam pekee asilimia 91 ya kaya zote zikitegemea mkaa kwa ajili ya kupikia. Waandishi na wahariri walioshiriki semina, wengi wao wakitokea Dar es Salaam na Morogoro, hakuna aliyesema anatumia umeme kwa kupikia. Lakini takribani wote walisema majumbani mwao wanatumia mkaa na gesi kama nishati ya kupikia.

Meneja wa Mradi wa TTCS, Charles Leonard anasema: “Pamoja na juhudi tulizonazo kama nchi za kutaka nishati mbadala ya kupikia ndiyo itumike, bado itatuchukua takribani miongo kadhaa kuweza kuwafanya Watanzania wengi kuachana kabisa na mkaa pamoja na kuni.”

Anaendelea: “Ndio maana sisi tumekuja na mradi huu wa kuleta mageuzi katika sekta ya mkaa ambao unahakikisha mkaa unazalishwa kwa njia endelevu, misitu inalindwa na wakati huo huo kijiji, halmashauri hadi serikali inapata mapato yake.”

Anafafanua kwamba kwa sasa asilimia zaidi ya 90 ya mkaa wote nchini unazalishwa kwa njia holela na kuchangia katika kuharibu mazingira.

IKIWA fomu moja ya kuomba ridhaa ...

foto
Mwandishi: Hamisi Kibari

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi