loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Mambo manne anayofanya JPM tofauti na wengine

VYOVYOTE vile ilivyo kuna mambo manne ambayo naweza kuyasema kwa ufupi tu ambayo Rais John Magufuli anayafanya tofauti sana na viongozi wengine.

Bila shaka kuna mengine anayafanya ambayo yanafanana na watangulizi wake na kubwa katika hayo ni ile hali ya kutukuza chama chake ili kiendelee kubaki madarakani kwa miongo mingi ijayo.

Sidhani kama kuna kiongozi atakayekuja kutoka CCM ambaye atafanya kinyume cha hilo. Hata hivyo, kwa maoni yangu, ningependa kudokeza mambo ya kiutendaji ambayo Rais Magufuli anayafanya kwa namna tofauti na viongozi waliomtangulia.

Kujitegemea kumepata magurudumu Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kusisitiza maneno haya: “Mnaweza kuamua kuachana na siasa ya ujamaa, lakini hamuwezi kuacha sera ya kujitegemea.”

‘Kujitegemea’ ni miongoni mwa dhana ambazo bila kueleweka zinaweza kumfanya mtu awe duni mbele ya wengine. Mtu ambaye ni ‘tegemezi’ au Nyerere aliita ‘ombaomba’ kwa kiasi fulani anajidunisha mbele ya wengine.

Kwa muda mrefu nchi zetu hizi za Kiafrika zilifika mahali pa kuomba hadi misaada ya kujenga vyoo! Na bado hata leo kuna watu ambao wanasubiria serikali iwafanyie vitu hata vilivyo ndani ya uwezo wao. Kurudi kwenye ‘kujitegemea’ ni kurudi kwenye kuuheshimu na kuulinda utu wetu kama binadamu.

Hivi ni kweli, tunahitaji msaada wa kigeni kupanda bustani ya maua shuleni au kwenye ofisi? Je, ni kweli tunahitaji msaada kutoka SIDA, USAID, EU, JICA, DANIDA, NORAD ili kufanya ukarabati shule zetu kongwe, kujenga shule mpya, kutengeneza madawati kwa ajili ya shule za watoto wetu au kujenga viwanja vya kuchezea watoto? Magufuli anaposema ‘tunaweza’ anataka kutuambia kuwa tumechelewa kujitegemea! Rais Magufuli tangu aingie madarakani ameamua kulishikilia hili vyema akijitahidi kulifanya taifa liwe na fikra za kujitegemea.

Na hapa ni katika kutumia rasilimali zake, uwezo wake, watu wake na mipango yake katika kujiletea maendeleo. Hakuna jambo linalotishia uhuru na utu wetu kama taifa kama kutegemea watu wa nje kwa ajili ya mafanikio yetu.

Jambo hili la kulazimisha taifa kujitegemea naamini litakuwa ni mafanikio makubwa kwa Rais Magufuli kuliko mambo mengi. Binafsi sitoshangaa kwa mwaka unaokuja Magufuli akaagiza wizara na idara zote kuandaa bajeti zao za 2020/2021 bila kuweka ndani au kusubiri misaada ya kigeni.

Sitoshangaa kabisa akaamua kutukatisha kunyonya (weaning) kutoka kwa wajomba zetu wa Ulaya na kulazimisha taifa kupanga bajeti yake kwa kutumia mapato na vyanzo vyake vya ndani. Misaada ya kigeni ikawa siyo tena ya moja kwa moja kwenye bajeti (Nondirect budgetary support).

Akiamua kufanya jambo hili nawahakikishia dunia nzima itashtuka na hawatoamini na siyo hivyo tu wapo wenzetu humu humu (wapingaji) ambao watatuambia kwa nini wanaamini hatuwezi kujitegemea kwenye bajeti! Amekataa kuangalia sura ya mtu Kwa muda mrefu watu walipokuwa wakishika madaraka walikuwa wanajiona wamefika. Watu walipoapishwa kushika ofisi yoyote walijisikia wako salama na wengine walifanya sherehe kwa kuamini ‘wameula’.

Magufuli amewafanya watu sasa hivi kutokuwa salama kwenye vyeo vyao. Hakuna jambo muhimu kama watu kutambua dhana ya ‘cheo ni dhamana’ na hivyo kujua hayuko salama kwenye kiti chake kama atashindwa kutimiza vyema majukumu yake.

Huko nyuma watu walitegemea ‘Rais kuwalinda’ lakini sasa hakuna anayeweza kuishi akiamini analindwa. Unaweza hata kuwaonea huruma wateule wa Rais. Rais amethibitisha kwamba haoni aibu au kigugumizi kumwondoa hata mchezaji nyota kwenye mechi! Kulikuwepo na baadhi ya ‘wachezaji nyota’ lakini wakajikuta wanaondolewa na mechi inaendelea kupigwa na watu wakashinda vile vile.

Sasa hivi, hakuna kujali sura, tunajali utendaji wa kazi. Sasa hivi ukipewa madaraka katika ofisi ya umma, sherehekea huku unatokwa machozi. Wale wale watakaokuletea maua ya pongezi ndio watakaomletea mwingine maua ya pongezi! Matokeo ya hili ni kuwa tunaona watendaji wengi, hasa mawaziri, wakiwa wanyenyekevu, wenye kujituma na kila mmoja akijitahidi ‘kuwa kazini’.

Amekuwa muwazi mno Kwa muda mrefu tulikuwa hatujui mambo yanayoendelea ndani ya serikali yetu. Mambo mengi tulikuwa tunayasikia kama uvumi au majungu kwenye vijiwe lakini sasa ni kama tumefunguliwa mlango na madirisha tuchungulie kinachoendelea ndani. Sisi ambao tumemfuatilia kwa muda mrefu tunajua JPM huwa hana tabia ya kufichaficha. Hata ile kauli yake maarufu ya ‘Msema kweli ni mpenzi wa Mungu’ kimsingi inatuambia tu kuwa haoni sababu ya kwa nini Watanzania wafichwefichwe.

Kile anachoamini ni ukweli atakisema hadharani na wazi kabisa na wakati mwingine kutoificha aibu ndani ya serikali yake mwenyewe. Kuna mambo ya siri lakini ukiaangalia sana mambo mengi ambayo watu wangependa kuwa ya siri hayana usiri wa maana kivile zaidi ya kufichiana tu siri zisizo na maana. Uwazi huu umewasaidia wananchi kuona nini kilikuwa kinafanyika na nini kinafanyika sasa hivi.

Kwa vile Rais ameamua kuwa muwazi kwa wananchi ni vyema wananchi pia waachwe wawe wawazi kwa serikali yao. Hakuna haja ya kufichana. Ujenzi mpya wa taifa Mojawapo ya mambo ambayo labda ni kubwa zaidi (linaloendana na lile la kwanza) ni uamuzi wake wa kufanya ujenzi mpya wa taifa. Magufuli ni kama amedakia alipoachia Nyerere.

Ni kama ameichukua nchi mwaka 1985 kutoka kwenye janga la wahujumu uchumi (mafisadi), viongozi ambao wameshaonja ubepari na sasa kila mtu anataka kula kwa raha zake. Ni kama amelikuta taifa ambalo wananchi wake wanatafuta maisha bora lakini wanakwazwa na viongozi wao. Magufuli anaingia na kuamua kuendeleza mambo yale ya kujenga misingi kwa maana ya masuala ya ardhi na makazi, miundombinu, elimu, maji, umeme na nishati, kilimo, madini na afya. Katika haya Rais Magufuli anajaribu kupalilia nchi na kupanda mbegu ili wengine waje kuvuna.

Na anachofanya – na labda wakati mwingine wengi hawasikii – ni kuwa katika nchi nzima, na kwa wakati ule ule miradi mbalimbali inatekelezwa. Anachokifanya ni kuhakikisha hakuna sehemu kubwa ya nchi ambayo inaweza kujihisi inapitwa. Ukiwasikiliza watu wenye kukosoa kinachofanyika Chato unaweza ukadhania Magufuli amegoma kufanya jambo lolote sehemu nyingine ya nchi.

Hili linaweza kuwa ni udhaifu wa taasisi zenyewe kujieleza lakini kwa tunaofuatilia tunajua jinsi gani matanki ya maji, njia za umeme, hospitali, vituo vya afya, barabara na miradi mingine lukuki inayoendelea kujengwa au ilikwishajengwa ndani ya miaka hii minne kulinganisha na miaka mingine yote. Hitimisho Mambo haya manne mbali na mengine mengi, Magufuli anayafanya kwa namna ya tofauti sana.

Lakini tofauti hiyo naweza kuielezea inatokana na mambo makubwa mawili ambayo hayakuwepo huko nyuma. Moja ni kuwa amekataa kufuata kilichoandikwa vitabuni. Kwamba, namna ya kufanya mambo ni a, b, na c kama watu walivyosoma shuleni.

Badala yake anawalazimisha watendaji walio chini yake kufikiria nje ya sanduku na kujaribu vitu tofauti. Matokeo yake baadhi ya mambo ambayo yangechukua muda zaidi au raslimali zaidi yanaweza kufanyika kwa ubora na uharaka kuliko huko nyuma.

Chukulia mfano wa jambo moja tu kati ya mengi la masoko ya madini. Hili halikutangaliwa na vikao virefu vya sera na mipango; ni mambo ambayo yaliamriwa na watu wakapewa kazi kwenda kuyatekeleza.

Jambo la pili ni kuwa Rais Magufuli hana hofu ya kukosea au kuonekana amekosea. Kwa wanaomjua vyema hili wala si jambo jipya. Toka zamani Magufuli amekuwa ni mtu wa kufikiria kitu na kukitenda labda wakati mwingine kwa gharama ya serikali au hata hadhi yake; lakini hofu ya matokeo ya kisheria (legal ramification) haijamzuia Magufuli kufanya kitu anachoamini ni sahihi kwa Watanzania.

Tuliona hili wakati wa suala la Makanikia na jinsi gani baadhi ya watu waliona kama Magufuli amegusa wakubwa na hatokuwa salama tena. Lakini alisimamia kile anachoamini hadi dakika ya mwisho.

Hata hili suala la ujenzi wa Bwawa la kufua umeme la Nyerere; kwa wengine liliwatia hofu kuwa wakubwa watetezi wa ‘mazingira’ wangemkwamisha; lakini kama huwaombi dola zao watakukwamisha kwa lipi? Miye nasubiria watakapoanza kutengeneza zile ‘cable cars’ kuruka Ngorongoro na kutengeneza viewing platforms kama zilizoko kwenye vivutio vingi kwenye nchi za wenzetu (nenda pale Grand Canyon utaona).

Sitoshangaa kuna watu watapiga kelele kweli. Wakati wenzetu wana barabara za lami zikikatisha Yosemite Parks na Parks nyingine huko majuu sisi kwetu tunaambiwa eti zinatishia wanyama kuvuka kwa waya kana kwamba hakuna namna ya kushughulikia hilo.

Hili la pili ndio linaweza au limeweza kumtengenezea Magufuli maadui wengi wa nje ikiwemo kitendo chake cha kutokwenda kwao “kujionesha onesha au kujitambulisha”.

Magufuli anaendelea kubaki Rais wa Afrika asiyeona kama ni ufahari kushikana mikono huko New York, Geneva, Paris na London. Ameendelea kuwa mtu wa tofauti sana. Makala haya yalichapishwa kwa mara ya kwanza kwa kirefu katika Jamii Forum, Novemba 18, 2019. Hii ni sehemu ya makala hayo ambayo imefanyiwa uhariri kidogo.

foto
Mwandishi: M. M. Mwanakijiji

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi