loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Uchumi unakua kwa asilimia 7.1

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein, ametimiza miaka tisa ya uongozi wake akijivunia mafanikio mbalimbali katika uchumi, afya, elimu na sekta nyingine mbalimbali.

Katika sekta ya fedha ambayo ndio makala haya yatajikita zaidi, Rais Shein amefanikiwa kujenga nidhamu ya matumizi na makusanyo ya kodi yaliyosaidia kuvuka malengo. Akizungumzia mafanikio hayo, Waziri wa Fedha na Mipango, Balozi Mohamed Ramia anasema bajeti ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na matumizi yake yote yamejikita katika ukusanyaji wa mapato na kujenga nidhamu nzuri ya matumizi ya fedha.

Anasema matokeo ya hatua hiyo ni kukua kwa kasi ya uchumi hadi kufikia asilimia 7.1 kutoka asilimia 4.1 wakati anaingia madarakani mwaka 2010, hatua ambayo inatoa nafasi ya kuiwezesha Zanzibar kufikia uchumi wa kati muda si mrefu. Anasema matarajio makubwa ni kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi hadi kufikia asilimia 7.5 ifikapo mwezi Juni mwakani.

Balozi Ramia anasema mfumuko wa bei umepungua kwani wakati Dk Shein anaingia madarakani ulikuwa asilimia 6.1 na sasa umeshuka hadi 3.9, jambo ambalo limeleta utulivu wa hali ya juu katika mwenendo wa biashara. Aidha anasema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea na mikakati yake ya kuhakikisha miradi ya kimkakati ikiwemo ujenzi wa bandari ya Mpiga Duri na jengo la abiria la uwanja wa ndege wa Abeid Amani Karume inatekelezwa kwa kutumia fedha za ndani.

Anasema miradi hiyo ya kimkakati ambayo imetajwa katika utekelezaji wa ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2015-2020, inalenga kukuza uchumi na pato la taifa na kutoa ajira kwa vijana.

“Nilipokuwa katika Baraza la Wawakilishi nikiwasilisha bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha 2019-2020 nilisisitiza kwamba miradi miwili ya ujenzi; Bandari ya Mpiga Duri na jengo la abiria la uwanja wa ndege wa Abeid Amani Karume tutaitekeleza kwa kutumia fedha za ndani,” anasema.

Anafafanua kwamba ujenzi wa jengo la abiria la uwanja wa ndege wa Abeid Amani Karume ni muhimu kwa sababu utaiwezesha Zanzibar kuongeza idadi ya watalii kwa mwaka. Jengo jipya la abiria likikamilika litawezesha uwanja huo kupokea wageni wapatao milioni 1.6 kwa mwaka kutoka wageni milioni 1.3 wa sasa. Anasema tayari serikali imelipa asilimia 30 ya fedha kwa ajili ya malipo ya awali kwa mkandarasi atakayeshughulikia mradi huo.

Kwa upande wa mradi wa bandari mpya ya Mpiga Duri huko Maruhubi, Balozi Ramia anasema upembuzi yakinifu umefanyika ambapo hata hivyo serikali haikuridhika na imeitisha tena kazi ya kufanya upembuzi mwingine yakinifu kwa ajili ya mradi huo ili kupata gharama kamili.

“Tunataka kujenga bandari nyingine kwa sababu iliyopo sasa imezidiwa na shughuli za mizigo na makontena na kufanya baadhi ya kazi kudorora na hivyo kuzusha malalamiko kutoka kwa wafanyabiashara,” anasema.

Balozi Ramia anasema katika kipindi cha miaka tisa ya uongozi wa Dk Shein amefanikiwa kwa kiasi kikubwa katika kudhibiti matumizi ya fedha na nidhamu ya matumizi ambapo mapato yameongezeka katika taasisi za ukusanyaji mapato. Kwa mfano, anasema bodi ya mapato nchini (ZRB) imevuka malengo ya ukusanyaji wa kodi kutoka Sh bilioni 32 katika mwaka 2010 hadi kufikia Sh bilioni 36 kwa mwaka 2019.

Anasema hatua hiyo imesaidia na kuiwezesha wizara ya fedha kulipa mishahara kwa wafanyakazi wake kwa wakati pamoja na kulipa pensheni kwa wastaafu kwa wakati. Hatua hiyo pia anasema imeiwezesha serikali kulipa viinua mgongo kwa wafanyakazi wanaotarajiwa kustaafu baada ya kupokea taarifa kutoka kwa Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.

Aidha anasema Wizara ya Fedha imefanikiwa pia kutekeleza agizo la Rais Shein la kulipa pensheni jamii kwa wazee waliofikisha umri wa miaka 70 bila ya kujali kama walipata kuajiriwa Serikali ama la.

‘’Wizara ya fedha tunalipa jumla ya Sh milioni 600 kwa mwezi kwa wazee wanaolipwa pensheni jamii kila mwezi,’’ anasema.

Anasema makusanyo mazuri ya kodi yameiwezesha serikali pia kununua meli mbili katika kipindi cha urais wa Dk Shein ikiwemo meli ya abiria iliyopewa jina Mv Mapinduzi pamoja na meli ya mafuta ya MT Ukombozi.

Anasema meli ya Mv Mapinduzi II imenunuliwa mwaka 2015 kwa shilingi bilioni 69.6 zilizotokana na serikali kubana matumizi na kwamba meli hiyo kubwa sasa inatoa huduma katika visiwa vya Unguja na Pemba. Aidha anasema Serikali imenunua meli ya mafuta mwaka huu ya MT Ukombozi kwa shilingi bilioni 36 na kwamba ina uwezo wa kubeba tani za mafuta 3,500.

“Hayo ni mafanikio katika kubana matumizi na kutumia vizuri fedha za walipa kodi kwa kununua meli zitakazotoa huduma kwa wananchi wetu na kupunguza tatizo la usafiri wa abiria na usafirishaji mafuta katika visiwa hivi,” anasema.

Hata hivyo, Balozi Ramia anasema mafanikio yaliyopatikana katika wizara ya fedha kwa kiasi kikubwa yamechangiwa na ushupavu na usimamizi makini wa Rais Shein. Kwa mfano, anasema ziara za Rais Shein nje ya nchi kwa kiasi kikubwa zimeleta tija na mafanikio makubwa ambapo Zanzibar imepata misaada mikubwa ya kifedha.

Anataja ziara ya Rais Shein ya hivi karibuni katika nchi za Umoja wa Nchi za Falme za Kiarabu (UAE) ilisaidia Zanzibar kupatiwa Sh bilioni 23 kwa ajili ya kusaidia vijana kujenga uwezo wa kazi za ujasiriamali.

Anasema fedha hizo zimetolewa kupitia mfuko wa Khalifa Fund ambapo utiaji saini wa fedha hizo ulishuhudiwa na Rais Shein pamoja na Shehe Mohamed bin Zayed Al-Nahyan ambaye ni mrithi wa mtawala wa Abudhabi.

‘’Fedha zitakazopatikana katika makubaliano yale ni kwa ajili ya vijana wa Zanzibar kuelekea kujitegemea kimaisha kupitia uanzishwaji wa shughuli za miradi midogo midogo ya ujasiriamali,” anasema Balozi Ramia.

Akizungumza katika ziara ya kukagua vifaa vya matengenezo ya barabara vilivyonunuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa fedha za ndani, Rais Shein alisema Serikali inatekeleza mpango wake wa matumizi mazuri ya fedha na hivyo kumudu kununua vifaa vya matengenezo ya barabara kwa Sh bilioni 14.

Aidha alisema serikali pia inatoa asilimia 75 ya fedha za ndani kwa ajili ya kununua vifaa vya kilimo na ruzuku pamoja na pembejeo ili kusaidia wakulima kupiga hatua kubwa ya maendeleo na kilimo.

Uzoefu wa kazi na utumishi uliotukuka unatajwa sehemu kubwa ya mafanikio ya Wizara ya Fedha ambapo Balozi Ramia katika miaka ya 1981-84 alikuwa Waziri wa Fedha katika awamu ya pili ya Rais mstaafu, Hayati Aboud Jumbe. Balozi Ramia anasema atatumia uzoefu wake kuona mafanikio makubwa katika sekta ya fedha yanafikiwa kwa ushirikiano na watendaji wa wizara hiyo.

foto
Mwandishi: Khatib Suleiman

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi