loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Utafiti wabaini dawa ya kuua mbu sugu wa malaria

TAASISI ya Utafi ti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) kituo cha Amani, wilayani Muheza, kimefanya utafi ti wa vyandarua vilivyopuliziwa dawa mseto za viuatilifu na viuadudu kwa pamoja na kuonesha ufanisi wa kuzuia usugu wa mbu wanaoeneza malaria na kupunguza maambukizi ya ugonjwa huo.

Utafiti huo wa miaka mitatu umefanyika Benin kwa nchi za Magharibi mwa Afrika na kwa upande wa Afrika Mashariki ulifanyika nchini chini ya NIMR kituo cha Amani na kuratibiwa na Shirika la Afya Duniani (WHO).

Akizungumza na Habari- Leo mjini hapa juzi, mkuu wa utafiti huo, Dk Patrick Tungu wa NIMR-Amani, alisema ulifanyika kwa vyandarua vyenye mseto wa viuatilifu aina ya pyrethroid pamoja na kiuadudu aina ya piperonyl butoxide kuangalia ufanisi wa vyandarua hivyo katika kudhibiti mbu waenezao malaria hasa wenye usugu dhidi ya viuatilifu. Vyandarua hivyo vilijaribiwa kwenye vibanda vya majaribio na kwenye nyumba za wakazi wa maeneo hayo kama njia ya udhibiti wa malaria.

Dk Tungu alisema matokeo ya utafiti huo yameonesha kwamba, katika kuangamiza mbu wenye usugu, vyandarua vyenye mseto wa viuatilifu vilionekana kuwa na ufanisi mkubwa kwa asilimia 36 zaidi ya vyandarua ambavyo vina viuatilifu vya aina ya pyrethroid pekee.

Pia matokeo ya utafiti huo yameonesha kuwa, piperonyl butoxide inapunguza maambukizo ya ugonjwa wa malaria kwa asilimia 44 kwa mwaka wa kwanza wa majaribio, ikilinganishwa na vyandarua vilivyonyunyiziwa pyrethroid pekee. Alitoa wito wa kuongezwa kwa wigo wa matumizi ya vyandarua vyenye piperonyl butoxide katika maeneo ambayo yana mbu sugu ambao wanaeneza malaria.

Alisema kuwa awali kabla ya utafiti huo walikuwa wanatumia njia mbalimbali za kudhibiti malaria, ikiwamo kupuliza dawa kwenye nyumba pamoja na kusambaza vyandarua vyenye viuatilifu kwa muda mrefu hali iliyosababisha usugu kwa mbu waenezao malaria. Kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, kiwango cha malaria nchini kimepungua kwa asilimia 10, ambapo mwaka 2008 kiwango cha ugonjwa huo kilikuwa asilimia 18.1 hadi asilimia 7.3 mwaka 2017.

Malengo ya taifa ni kupunguza kiwango cha maambukizi hadi kufikia asilimia moja mwaka 2020. Ili kufikia lengo hilo, Dk Tungu alitoa wito kwa Watanzania kutumia vyandarua hivyo vilivyopuliziwa dawa mseto za viuatilifu na viuadudu kwa pamoja ili kupunguza na kutokomeza kabisa malaria nchini.

foto
Mwandishi: Cheji Bakari, Muheza

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi