loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Kilimo cha chikichi kupanuliwa nchini

TAASISI ya Utafi ti wa Kilimo Tanzania (TARI) imepanga kuendeleza zao la chikichi katika maeneo mengine yanayostawi zao hilo, ikiwamo wilaya ya Kyela (Mbeya), Mkuranga na Bagamoyo (Pwani), Tanga na Zanzibar.

Mkurugenzi Mkuu wa TARI, Dk Geofrey Mkamilo, alisema hayo juzi wakati akiwa kwenye ziara yake ya kuangalia uzalishaji wa mbegu bora za chikichi mkoani Kigoma. Alisema maeneo hayo tayari yamefanyiwa utafiti na kuonekana yana uwezo mkubwa wa kustawi zao hilo, hali ambayo itasaidia kuzalisha mafuta kwa wingi na hivyo kupunguza tatizo la uhaba wa bidhaa hiyo nchini.

“Ipo mikoa ambayo ina fursa ya kulima zao la chikichi ukiachilia mbali mkoa wa Kigoma, sasa tumepanga kuongeza nguvu katika mikoa hiyo kwa kupeleka mbegu za kisasa na zenye tija kwa ajili ya kuhakikisha tunazalisha mafuta ya chikichi kwa wingi ili kumaliza tatizo la uhaba wa mafuta nchini,” alisema.

Iwapo Tanzania itafanikiwa kuongeza uzalishaji wa mafuta na ziada inaweza kuiuzia Kenya ambayo inaagiza asilimia 80 ya mafuta ya kula kutoka nje ya nchi pamoja na nchi za Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Sudan.

Naye Mkurugenzi wa TARI kituo cha Kihinga, mkoani Kigoma, Dk Filson Kagimbo, alisema taasisi hiyo ina mkakati wa kufufua zao la chikichi kwa sababu linatoa mafuta mengi kwa ekari moja ikilinganishwa na mengine ambayo yanazalisha mafuta nchini, likiwamo alizeti.

Akizungumzia kilimo cha chikichi mkoani Kigoma, alisema TARI inafanya utafiti ili kuongeza tija kutoka kutoa tani 1.6 kwa hekta moja ili kufikia nchi nyingine zinazolima zao hilo ambao zinazalisha hadi tani nane au tisa kwa hekta moja.

Alisema mkakati wa TARI ndani ya miaka mitatu ni kusambaza miche milioni 15 kwa wastani wa miche milioni tano kwa kila mwaka, hatua ambayo itapunguza gharama za serikali za kuagiza mafuta ya kula kutoka nje ya nchi.

Kwa upande wake, mshauri wa kilimo sekretarieti ya mkoa wa Kigoma, Joseph Lubuye, alisema kwa kuzingatia agizo la Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, halmashauri zote zinazolima chikichi katika mkoa huo zimeitikia wito wa kuanzisha vitalu vya miche ya zao hilo.

foto
Mwandishi: Lucy Ngowi, Kigoma

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi