loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

‘Namwandaa mwanangu arithi kilimo hai’

“KAMA unavyoona mimi nimerithi shamba hili (kihamba) kutoka kwa baba yangu miaka mingi iliyopita na sasa ninamwandaa mwanangu aliyeko kidato cha tatu kurithi hili shamba,” anasema Remmy Temba, baba wa watoto tisa.

Temba (57) ni mkulima ambaye pia anajihusisha na ufugaji katika kijiji cha Uru Shimbwe, Halmashauri ya Wilaya ya Moshi anayeendesha maisha yake kwa kutegemea, pamoja na vyanzo vingine, shamba la ekari tatu la kahawa pamoja na matunda mbalimbali. Anabainisha kuwa alirithi shamba hilo mwaka 1979 kutoka kwa baba yake na mpaka sasa anaendelea kula matunda ya shamba hilo.

Baba huyo wa watoto tisa anasema wakati anaendeleza shamba hilo, ameanza kumwandaa mtoto wake wa mwisho, James, aliyepo kidato cha tatu katika sekondari ya Shimbwe Juu ili aje kurithi shamba hilo na kuendeleza kilimo hai.

Akizungumza na waandishi wa habari waliomtembelea shambani kwake ili kujionea manufaa ya kuendesha kilimo hai, Temba anasema anashukuru kuendesha kilimo hai ambacho hakina madhara kwa watumiaji na kinampa faida. Ni kwa mantiki hiyo, anawataka watanzania kupenda kutumia mazao yatokanayo na kilimo hai ili kulinda afya zao.

Kilimo mseto Mkulima huyo anayeendesha kilimo mseto, anawaonesha pia waandishi wa habari mifugo iliyopo katika shamba lake ambayo ni pamoja na kuku, nguruwe, mbuzi, sungura pamoja na ng’ombe na kwamba mifugo hiyo ndio pia humpa mbolea kwa ajili ya mazao yake. Temba anasema ndani ya shamba lake la miti ya kahawa, pia kuna magimbi na miti mbalimbali ya asili inayotumika kama kivuli ndani ya shamba lakini pia mingine ni dawa za magonjwa mbalimbali ya binadamu, mifugo na mimea.

Temba anabainisha kuwa katika shamba lake amepanda mimea ya aina mbalimbali, ikiwamo parachichi, matunda damu, peach, ndizi, kakao, viazi vikuu na mengineyo. Vingine alivyopanda ni miti mbalimbali ambayo inatumika kama dawa za asili yenye uwezo wa kutibu magonjwa mbalimbali.

Miaka 15 ya kilimo hai Anasema sasa ana miaka 15 tangu alipoanza kuendesha kilimo hai baada ya kupata elimu kutoka kwa wataalamu wa Shirika la Chakula Duniani (FAO) na kuachana na kilimo cha matumizi ya dawa alichokuwa anatumia baada ya kurithi shamba hilo.

Kilimo hai (organic farming) ni kile ambacho hakitumii mbolea na dawa zenye kemikali sanisi. Halikadhalika mifugo ya kilimo hai haitumii viongezwa wala homoni na kilimo kinachoongeza rutuba ya udongo. Kilimo hai pia kinahusisha matumizi asilia ya virutubisho, kinazuia na kudhibiti wadudu na magonjwa, hakihusishi ubadilishwaji wa vinasaba (GMO) na pia kinatumia mbinu nzuri za asili za kilimo na za kitaalamu.

Temba anabainisha kuwa katika kilimo hicho amekuwa akitumia mbolea za wanyama huku dawa anazoweka katika mimea na wanyama wake anaofuga zikiwa siyo zinazotokana na kemikali isipokuwa dawa za asili ambazo anasema zinamaliza kabisa matatizo yaliyopo.

“Kwa mifugo yangu natumia dawa za miti iliyopo na mizizi yake kutokana na maelekezo niliyopata kutoka kwa wazazi pamoja na mlonge, ambayo ni dawa nzuri kwa kuku,” anasema.

Temba anasema kwa kuendesha kilimo hai hakuna gharama ya kununua dawa za kupuliza au dawa za mifugo kama alivyokuwa akifanya awali kabla ya kupata elimu kuhusu kilimo hai, bali anatumia vitu mbalimbali vinavyotokana pia katika shamba lake au mifugo yake. Katika kupambana na wadudu anasema anatumia bangi mwitu, mkojo wa ng’ombe au sungura pamoja na maua maarufu mashona nguo.

“Kila kiumbe katika ardhi kina kazi yake hivyo dawa hizi zinatumika kufukuza wadudu,” anasema Temba.

Anasema mdudu aina ya ‘bungua’ anayetafuna miti ya mikahawa hupambana naye kwa njia ifuatayo: Anachukua mafuta ya kula na kuyaweka kwenye shimo ili kuvutia siafu waje kwa ajili ya kufuata wadudu wanaokuja kula mafuta, hivyo siafu hao ndio wanaowamaliza bungua.

Kuhusu matumizi ya mkojo wa wanyama kama dawa ya kuondoa wadudu kwenye mimea, anafafanua kwamba anachukua mkojo huo na kuuhifadhi sehemu kwa siku 21 kisha huwa tayari kupulizia kwenye mimea na kuua wadudu. Mti mwingine anaoutumia kama dawa ni ule wanaouita mfurufuru ambao anasema anautumia kama dawa ya mbuzi wanapougua.

“Katika kukabiliana na wadudu wanaoharibu mazao ninatumia dawa za asili ili kuwafukuza wakati mwingine bila kuwaua,” anasema na kuongeza kwamba matumizi ya kemikali huua hadi minyoo kwenye udongo ambao kimsingi wana faida zake shambani.

Halikadhalika anasema kuna mti wanaouita mnuka ambao wakati wa kiangazi una tabia ya kupandisha maji kwenye matawi na baadaye mvua zikiisha hudondosha maji kwa kutumia wadudu wanaokuwa katika mti huo hivyo kuleta unyevu shambani.

Kilimo na afya njema Temba anaamini kwamba umri wa kuishi ni mrefu katika kijiji hicho huku wengi wakiwa pia hawaugui mara kwa mara kutokana na kula chakula kisichotokana na mazao yaliyolimwa kwa kemikali. Huku akiwaonesha waandishi wa habari kaburi la mama yake, Temba anasema watu katika kijiji hicho wanaishi kwa miaka zaidi ya 100 na kwamba mama yake mzazi alifariki dunia mwaka 2017 akiwa na umri wa miaka 112.

“Mimi nina miaka 57 lakini kutokana na kula vyakula vya asili sikumbuki mara ya mwisho nilienda lini hospitali kutibiwa,” anasema.

Mbali na afya njema, Temba anasema kilimo hicho kumemwezesha kusomesha watoto wake na wengine hadi chuo kikuu huku wengine wawili wakiwa kidato cha tatu. Kwa nini anamwandaa mwanawe wa mwisho, James kurithi shamba hilo na siyo wengine? Temba anajibu kwamba kutokana na ‘dogo’ huyo kupenda kuwa mkulima mbali na kuwa na ndoto pia za kusoma hadi kupata shahada.

Kuhusu hali ya mavuno katika shamba lake, Temba anasema katika msimu uliopita alipata kilo 700 za kahawa zilizompa Sh milioni tatu. Temba analiomba Shirika la Kuendeleza Kilimo Hai Tanzania (Toam) kusaidia katika kuweka bei elekezi ya kahawa zinazolimwa kwa kutumia kilimo hai tofauti na kahawa inayolimwa kwa kemikali kutokana na kuwa na soko kimataifa.

Kuhusu changamoto, anasema kubwa ni mabadiliko ya hali ya hewa hususan pale kunapotokea mvua nyingi na hivyo kahawa kuchelewa kukauka. Changamoto nyingine anasema kwa sasa bei ya kahawa wanayolima kwa njia hai ni karibu sawa na bei ya kahawa zinazolimwa kwa dawa. Mwito kwa jamii “Naishauri jamii ijikite zaidi katika kutumia mazao yanayotokana na kilimo hai kwa kuwa hayana madhara na yana faida nyingi mwilini,” anasema Temba na kuwashauri wakulima wengine kuachana na kilimo cha kemikali.

Kwa upande wa serikali, Temba anaiomba iendelee kutoa elimu kwa jamii ili itumie kilimo hai ambacho kwa sasa baadhi ya mikoa wakulima wameanza kukikimbia kwa madai kwamba uzalishaji wake huchukua muda mrefu. Kahawa hai bado chache Wafanyabiashara kutoka Uingereza na Afrika Kusini wanaojihusisha na biashara ya kahawa hai (inayolimwa bila kemikali) walifika shambani kwa Temba wakitafuta kahawa hai kwa ajili ya viwanda vyao, hali inayoonesha jinsi ambavyo kuna mahitaji makubwa duniani ya mazao yatokanayo na kilimo hai.

Wakati wafanyabiashara hao wanafika katika shamba la Temba walikuwa katika juhudi za kukamilisha ujazaji wa makontena makubwa 16 ya kahawa hai huku hadi muda huo wakiwa wamepata makontena manane pekee kutoka Rungwe mkoani Mbeya. Paul Cooker wa kampuni ya CTCS ya Uingereza anakiri kwamba kutokana na mahitaji ya kahawa hai, walifika Tanzania wakilenga kupata makontena 16 lakini hadi waandishi wakiwa shambani kwa Temba walikuwa wameambulia makontena hayo manane tu.

“Tumefika huku kuangalia kama tutapata kiasi kilichobaki kwani mahitaji ni makubwa,” anasema na kuongeza kwamba bei ya kahawa hai ni kubwa tofauti na inayolimwa kwa kutumia kemikali.

Mzungu huyo anaamini kwamba kahawa hai ni tiba ya kumwondolea mtu msongo wa mawazo na maumivu ya kichwa. Kwa upande wake, mfanyabiashara, Mart Carter kutoka kampuni ya Tribeca Coffee ya Afrika Kusini anasema mazingira ya mashamba ya asili yanapendeza huku yakitoa mazao bora ambayo ni muhimu kwa afya. Naye anawahimiza wakulima wa Tanzania kujikita zaidi katika kilimo hai ili kukamata soko duniani lililopo ambalo anasema ni kubwa.

Kifo cha Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamini Mkapa ...

foto
Mwandishi: Theopista Nsanzugwanko

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi