loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Changamoto ya tafsiri kwa waandishi wa habari

TAFSIRI ni uhawilishaji wa maarifa kutoka lugha moja hadi nyingine. Katika maisha ya kila siku tafsiri zinafanyika kwenye nyanja mbalimbali.

Nchini Tanzania tafsiri hufanyika sana katika ofisi nyingi, lakini inafanyika zaidi katika vyombo vya habari. Habari za lugha mbalimbali kutoka nje au hata ndani ya Tanzania zinawafikia wananchi baada ya kutafsiriwa katika lugha ambayo wanaielewa.

Kwa mfano, nchini Tanzania ili habari ziwafikie watu wengi zaidi, inabidi zitafsiriwe katika lugha ya Kiswahili. Ni kutokana na hilo kwamba watu wanaofanya tafsiri katika vyombo vya habari wanatakiwa kuwa makini sana wanapofanya kazi hiyo ili kuweza kufanikisha kazi yao na pia kuwafanya wanaoisoma au kuisikiliza kupata taarifa sahihi kwa lugha iliyotafsiriwa. Kwa sababu ya umuhimu mkubwa wa eneo hili la habari, tafsiri katika vyombo vya habari inatakiwa kufanyika kwa umakini mkubwa.

Ndiyo maana wataalamu wengi wa tafsiri wanasisitiza kwamba tafsiri inatakiwa isiwe na makosa ya dhana na uchapaji, ifanywe kwa umakini, iwe sahihi na ikiwezekana ijumuishe maelezo zaidi kwa madhumuni ya kufafanua kilichoelezwa katika lugha chanzi.

Makala haya yataangalia kwa kifupi matatizo ya tafsiri yanayowakabili waandishi wa habari wanapotafsiri habari za kimataifa kutoka katika lugha ya Kiingereza kwenda Kiswahili. Pia makala yataangalia sababu zinazowafanya waandishi wa habari kufanya tafsiri ambazo si sahihi.

Mafanikio ya vyombo vya habari, yaani magazeti, redio na televisheni katika tafsiri kwa kiasi kikubwa yanategemea uwezo wa wanahabari kutafsiri ujumbe kwa usahihi kutoka Lugha ya Kiingereza kwenda Kiswahili na kinyume chake.

Swali la kujiuliza ni kwamba, je, wanaotafsiri habari zinazotoka lugha ya Kiingereza wanao uwezo wa kufanya tafsiri zilizo sahihi? Waandishi wa habari walio wengi ambao wanafanya tafsiri kwenye vyombo vyao vya habari wanakabiliwa na matatizo mbalimbali wanapotafsiri habari hizo kutoka lugha ya Kiingereza kuwa katika lugha ya Kiswahili. Matatizo hayo ni pamoja na ukosefu wa mafunzo ya tafsiri, kutotumia kamusi na kutozimudu vizuri lugha zote mbili wanazozitumia katika kutafsiri.

Wanahabari wengi wanaofanya tafsiri wanaonekana kutomudu vema lugha ya Kiswahili na hivyo kujikuta wakitumia sarufi ya kigeni hasa ya Kiingereza wanapotafsiri kutoka lugha hiyo kwenda Kiswahili. Pia vyombo vingi vya habari huwapa wanahabari wao kazi ya kutafsiri wakiamini kwamba wanafahamu Kiingereza na Kiswahili kwa vile walisoma lugha hizo wakiwa shuleni.

Kwa hiyo, wanapoingia katika taaluma hiyo wanapewa kazi ya kutafsiri habari za kimataifa, jambo hili linapingwa na mwandishi mmoja wa kitabu kinachoitwa “Translating Law” ambaye anasema “tafsiri si kazi ambayo mtu yeyote anayezungumza lugha mbili anaweza kuwa na sifa ya kuifanya”, hii ina maana kwamba lazima upate mafunzo ya tafsiri ili uwe mfasiri mzuri.

Pia moja ya kanuni za kimataifa za maadili ya taaluma ya uandishi wa habari inasema kazi muhimu ya uandishi wa habari ni kuwapa watu haki yao ya kupata habari sahihi na za kweli ambapo taarifa zinaripotiwa kwa umakini katika muktadha wake unaofaa na bila ya kupotoshwa.

Wanahabari walio wengi hawaingii katika taaluma hiyo wakiwa na uelewa mdogo wa lugha tu, bali pia wanakuwa hawana mafunzo ya tafsiri. Tunapaswa kujiuliza maswali kadhaa kabla hatujawalaumu wanahabari. Je, wanafanya hivyo kwa makusudi? Kwa nini wanatumia maneno ya Kiingereza katika makala zao za Kiswahili? Kwa nini wanatumia maneno ambayo yana maana tofauti na ile ya Kiingereza? Kwa nini wanatumia sarufi ya Kiingereza? Je, hii inaweza kuwa sababu ya kutoimudu lugha? Wanaifahamu nadharia ya tafsiri? Kwa upande mmoja wanaweza kulaumiwa kwa sababu kuna makosa ya wazi kabisa katika tafsiri ambapo maana za maneno yaliyo katika Kiingereza zinapatikana kwenye kamusi.

Kwa mfano mwandishi anapotafsiri “rubber bullet” kama “virungu” badala ya “risasi za mpira”, au “to trust” kama “kuthamini” badala ya “kuamini” au “requested” kama “kulazimika” badala ya “kuombwa” au “students” kama “wananchi” badala ya “wanafunzi”.

Kwa upande mwingine lawama zinaelekezwa katika mfumo wa mafunzo ya uandishi wa habari. Mafunzo ya nadharia ya tafsiri na umilisi wa lugha haya- fundishwi kwa kina katika vyuo vya uandishi wa habari, kwa hali hiyo hatutegemei kupata tafsiri nzuri kutoka kwa mtu asiye na mafunzo ya tafsiri. Lakini kwa sababu zoezi la tafsiri inabidi liendelee licha ya matatizo yaliyotajwa hapo juu, mfasiri inabidi atafute namna ya kutatua matatizo anayokabiliana nayo wakati wa kutafsiri.

Mwisho tunatoa ushauri kwa wanahabari kwamba, kwa kuwa inabidi watafsiri habari wanazopokea kutoka lugha za kigeni ili wananchi wazielewe licha ya kutokuwa na mafunzo ya kutosha, matumizi ya kamusi ni muhimu sana ili kutatua matatizo ya maana za maneno ya kawaida ambayo yanapatikana kwenye kamusi. Kwa mfano hakuna namna ambayo unaweza kuhalalisha kosa la “student” kuitwa “wananchi”. Pia wanatakiwa kujenga utamaduni wa kujisomea ili kufahamu taarifa mbalimbali katika nyanja tofauti.

foto
Mwandishi: Vida Mutasa

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi