loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Nyasa ni benki ya vivutio lukuki vya utalii

WILAYA ya Nyasa iliyopo mkoani Ruvuma bado ina fursa za maliasili ya kutosha zikiwemo misitu, wanyamapori, samaki, mito, ziwa, fukwe na mali kale ambazo hazijaharibiwa lakini ambazo wengi hawazijui na ndiyo maana tunasema wilaya ya Nyasa ni benki ya vivutio vya utalii na uwekezaji.

Fursa hizo zinaweza kutoa mchango mkubwa kwenye pato la Taifa na wananchi wa wilaya ya Nyasa, mkoa wa Ruvuma na Taifa kwa ujumla kupitia utalii wa kiutamaduni na ikolojia.

Makao makuu ya Wilaya ya Nyasa yapo katika Mji wa Mbambabay. Ofisa Maliasili na Utalii wa wilaya ya Nyasa, Bugingo Bugingo, anasema wilaya hiyo ina sifa ya kuwepo kwenye bonde la ufa, ambapo bonde hilo huanza kuonekana kutoka katika maeneo ya Buruma, unaposhuka milima katika kona zinazoitwa Ambrosi.

Kivutio adimu cha utalii katika wilaya ya Nyasa ni uwepo wa Ziwa Nyasa ambalo linapatikana Kusini Magharibi mwa Tanzania. Ziwa Nyasa ni la tisa kwa ukubwa duniani na la tatu kwa ukubwa barani Afrika.

Ziwa hilo lina kina cha kati ya mita 426 na 758 na hii ni kutokana na kupitiwa na bonde la ufa. Kwa upande wa Tanzania mito mingi inapatikana ikitokea wilaya ya Nyasa katika safu za milima ya Livingstone, mito hiyo ni Ruhuhu, Lumeme, Ruhekei, Lwika, Mbamba Bay, Likumbo na Chiwindi ambayo huingiza maji ndani ya Ziwa Nyasa.

Kwa mujibu wa Bugingo, ziwa Nyasa ni kuvutio kikubwa cha utalii kanda ya kusini kwa kuwa limesheheni vitu vingi ndani yake na tabia tofauti ukilinganisha na maziwa mengine ya hapa nchini na duniani kote.

“Baadhi ya tabia za ziwa hili ni uwepo wa maji meupe na maangavu eneo lote la ziwa na mawe marefu ambayo yanajulikana kwa majina ya hia na mala yanayobeba sifa tofauti,’’ anasema Bugingo.

Tabia nyingine za ziwa hilo anazitaja kuwa ni mawimbi makubwa, fukwe nzuri na zenye sifa tofauti, mawe kuonekana kama sakafu eneo la Chiwindi, fukwe zenye udongo wa mfinyanzi, kina cha maji kuwa kifupi kwa umbali mrefu na mchanga mdogo ambao watu wa kale walitumia kusugulia meno ili yawe meupe hasa katika fukwe za Mtipwili.

Bugingo anayataja maeneo mengine ambayo ni kivutio katika wilaya hiyo kuwa ni yale ambayo huota nyasi ambazo zinaonekana kama zimefyekwa kwa ustadi, na fukwe za eneo la Mhalo zina mapango ambayo kuta zake ni kama zimesakafiwa.

Kulingana na ripoti ya utafiti wa mwaka 2011, asilimia 15 ya aina za samaki wa maji baridi duniani wanapatikana ziwa Nyasa ambapo kuna aina ya samaki tofauti zaidi ya 600, huku kukiwa aina ya samaki wa mapambo zaidi ya 400 na viumbe wengineo ambao hawapatikani katika ziwa lolote duniani isipokuwa katika maeneo tofauti ndani ya ziwa Nyasa kutegemeana na aina na usalama wa maisha yao.

Jonathan Ruanda, Mtaalamu wa kuzamia samaki wa mapambo katika ziwa Nyasa na mfanyabiashara wa samaki hao anasema tangu mwaka 1960 samaki hai wa mapambo walianza kuuzwa katika nchi za Ulaya na Marekani. Hata hivyo, anasema nchi nyingi kama vile Japan, Sweden, Uturuki, Denmark, Canada, Ufaransa, Uingereza na Ujerumani zilivutiwa na samaki wa mapambo kutoka ziwa Nyasa kutokana na kuwa na sifa ya kipekee yaani rangi nzuri za kupendeza na hakuna sehemu nyingine wanapatikana samaki wa mapambo wa aina hii. Ofisa Maliasili wa Mkoa wa Ruvuma, Afrikanus Challe, anabainisha kuwa Ziwa Nyasa pia limesheheni utajiri mkubwa wa viumbe hai wakiwemo fisimaji, mamba, nyoka na viboko ambao ni kivutio kikubwa cha utalii.

“Ndege wanaohamia kutoka Ulaya na baadhi ya nchi za Afrika wanapatikana maeneo ya mwambao mwa ziwa Nyasa ambao ni kivutio kikubwa cha utalii. Ndege hao huja kwa ajili ya kujipatia chakula cha aina mbalimbali katika mwambao wa ziwa Nyasa wakiwa kwenye misafara yao,’’ anasisitiza Challe. Akizungumzia jina la Mji wa Mbambabay ambao ni makao makuu ya wilaya ya Nyasa, Challe anabainisha jina la “Mbamba bay,” kwamba Mbamba ikiwa na maana ya radi na bay ikimaanisha ghuba na kwamba vyote hivyo ni vivutio vyenye historia ya kupendeza na kuvutia kwa wageni.

“Tafsiri hizi ambazo zilitolewa na wenyeji zinaonesha kwamba kutokana na radi kali za mara kwa mara kupiga kwenye rasi iliyopo karibu na ghuba hiyo na ndipo eneo likaitwa Mbamba bay,’’ anasisitiza Challe. Challe anabainisha kuwa ghuba hiyo ni kubwa na imefunikwa na uoto wa asili wa miti na nyasi, baadhi ya miti hiyo inatumika kama dawa za asili hadi sasa. Anasema watu pia hutumia msitu wa Mbamba kwa matambiko ya kupiga ngoma za kufukuza au kuita majini kwa imani zao na kwamba katika msitu huo kuna wanyama kama chui wanaotokea milima ya Nangombo, Ukuli na Chinyemba ambao wanapatikana katika ghuba hiyo, wakiwafuata wanyama aina ya ngedere waliopo kwa wingi katika msitu huo.

Kulingana na Challe, maeneo mengine ya vivutio vya utalii kwa Wilaya hiyo ni visiwa vya Mbamba, Lundo, Hongi na jiwe la Pomonda ambavyo vyote vimekuwa na sifa na historia nyingi ambazo zikitangazwa vizuri zitachangia kukuza utalii kwa kuvutia watalii wa ndani na nje. “Visiwa hivi kila kimoja kimekuwa na sifa ya pekee; kisiwa cha Mbamba kina sifa ya kuwa na mapango ambayo wavuvi hujihifadhi wakati wa dhoruba kali, samaki wa mapambo pia wanapatikana katika kisiwa hicho.

“Kisiwa cha Lundo kina historia ya kuishi wagonjwa wa ukoma waliotengwa na jamii na makaburi ya wagonjwa hao ambao walizikwa kwenye tope au kwa kugandikwa tope kwa imani kwamba wakifanya hivyo wangetokomeza ugonjwa huo. Kituo hicho baadaye kilihamishiwa kijiji cha Ngehe kata ya Kihagara wilayani Nyasa ambacho kipo hata sasa,’’ anasema Challe.

Kivutio kingine maarufu katika Wilaya ya Nyasa ni uwepo wa jiwe la Pomonda ambalo lina pango kubwa ambalo linaweza kuhifadhi watu zaidi ya 100. Jiwe hilo wakati huo lilitumika kujificha wakati wa vita na wavuvi kujihifadhi dhoruba inapozidi. Jiwe hili pia ni eneo zuri ambalo hutumiwa na waogeleaji kwa ajili ya kujirusha wakati wa mchezo wa kuogelea.

Itaendelea

Mwandishi ni mchangiaji wa gazeti hili mawasiliano ni baruapepe: albano.midelo@ gmail.com, simu 0784765917

IJUMAA iliyopita, tulianza kuangalia manufaa ambayo nchi inaweza kuyapata kupitia ...

foto
Mwandishi: Albano Midelo

1 Comments

  • avatar
    Petro
    22/11/2019

    Asante Bwana Midelu kwa taarifa, kuhusu neno Mbamba lina maana ya mti unaomkinga mtu dhidi ya radi pia inasemekana waanzilishi wa neno Mbamba ni Wayao. Wakipita hapo walipaita mbamba

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi