loader
Picha

Tanzania kuondolewa orodha ya nchi maskini

SHIRIKA la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Maendeleo ya Biashara (UNCTAD), limezindua ripoti ya mwaka 2019 kuhusu nchi maskini zaidi duniani.

Shirika hilo limebainisha kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizo katika hali chanya kwa kufanya vizuri, kuweza kuondoka katika orodha ya nchi maskini. Imebainisha kuwa Tanzania inafanya vizuri, ikiwa na taasisi imara, uongozi imara na mapambano dhidi ya rushwa.

Akiwasilisha ripoti hiyo jana jijini Dar es Salaam, Mchumi kwa Nchi Zinazoendelea (LDC), Benjamin Banda alisema Tanzania ipo katika nafasi nzuri ya kuondoka katika kundi la nchi maskini. Alisema Tanzania ina uongozi imara, lakini pia ikielekeza usimamizi imara hata fedha za misaada kutoka nje ya nchi, zinaelekezwa sehemu zinazofaa, lengo likiwa ni kutoka kwenye kundi la nchi maskini.

Kuhusu ripoti, alisema nchi itastahili kuondoka kwenye kundi la nchi maskini, ikiwa itakidhi viwango vya juu vya kutoka, angalau kwa vigezo viwili kati ya vitatu na katika uhakiki. Alisema miongoni mwa vigezo ni ikiwa wastani wa pato la kila mtu la kitaifa la miaka mitatu la nchi maskini, limeongezeka kwa kiwango angalau mara mbili ya kiwango cha juu, yaani dola za Marekani 2,460.

“Hii ina maana kwamba mpaka mwaka 2018 kulikuwa na nchi 12 zinazostahili au kukaribia kuondoka kwenye kundi la nchi maskini,” alisema Banda.

Alisema kutoka na ripoti hiyo, UNCTAD inazitaka nchi maskini duniani, kuchukua jukumu kubwa la kuelekeza msaada wa nje katika maendeleo. Alisema mataifa yaliyo masikini zaidi duniani, yanapaswa kuhakikisha fedha kutoka vyanzo vyote vya nje, vinaelekezwa kwenye vipaumbele vya maendeleo ya taifa, mbinu hii ni njia bora ya kusimamia utegemezi wao wa msaada na hatimaye kuuepuka.

Alisema ili nchi hizo zifikie Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs), lazima zichukue umiliki wa ajenda yao ya maendeleo na kusimamia mgawo wa fedha za maendeleo ya nje katika mpangilio na vipaumbele vyao vya maendeleo ya taifa.

“Jumuiya ya kimataifa pia inahitaji kutoa msaada wake kwenye lengo hilo la kawaida,” alisema.

Akitoa neno la shukrani, Kaimu Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa (UN), Michael Dunford alisema ripoti hiyo inatoa fursa kwa uchambuzi kijamii na kiuchumi na kupata data zitakazoboresha nchi.

Alisema ni ripoti inayotoa taarifa zinazotakiwa, ikitaka pia fedha kutoka nje kuelekezwa katika uwekezaji stahiki jambo litakalokuza uchumi. Alisema mashirika ya UN yaliyoko nchini Tanzania, yako mbele kusaidia serikali kufikia malengo enddlevu ya maendeleo na kutekeleza program mbalimbali za maendeleo. Nchi maskini zinahusisha nchi 15 kati ya 20, zinazotegemea zaidi msaada duniani kutokana na upungufu wa mara kwa mara katika akiba zao za nyumbani.

WAKURUGENZI wawili wa Kampuni ya Tanzanite One Mining Ltd ya ...

foto
Mwandishi: Lucy Lyatuu

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi