loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Miradi inayotarajiwa kukabili upungufu wa sukari nchini

WIKI iliyopita, kulikuwa na makala inayoonesha juhudi za serikali za kuongeza uzalishaji wa sukari kwa lengo la kukabili nakisi iliyopo nchini. Makala haya ni mwendelezo, yakiainisha miradi na hatua zilizofi kiwa kuelekea katika uzalishaji wa sukari inayotosheleza mahitaji nchini.

Katika mahojiano maalumu na Katibu Mkuu, Wizara ya Viwanda na Uwekezaji, Profesa Joseph Buchwashaija, inabainika viwanda vitano vilivyopo nchini havitoshelezi mahitaji ya sukari. Mahitaji ya sukari yamekuwa yakibadilika mwaka hadi mwaka kulingana na hali halisi ya mahitaji kwa mwaka husika.

Kwa mfano, mwaka 2019/20 mahitaji ya sukari yanakadiriwa kuwa tani 710,000. Kati ya hizo, tani 545,000 ni sukari ya matumizi ya nyumbani na tani 165,000 ni kwa matumizi ya viwandani. Makadirio ya uzalishaji wa sukari kwa viwanda vyote kwa mwaka 2019/20 ni tani 378,449 sawa na asilimia 67.7 ya sukari inayokadiriwa kwa matumizi ya nyumbani.

Viwanda vikubwa vilivyopo nchini ni Kilombero Sugar Ltd na Mtibwa Sugar Ltd vilivyopo Morogoro, Kagera Sugar Ltd kilichopo Kagera, TPC Ltd kilichopo Kilimanjaro. Kidogo ni cha Manyara Sugar Company kilichopo mkoani Manyara.

Profesa Buchwashaija anaeleza mikakati ya serikali kuhakikisha nchi inajitosheleza katika uzalishaji wa sukari na kupunguza matumizi ya fedha za kigeni katika kuagiza sukari kutoka nje ya nchi. Kwa kuzingatia fursa zilizopo za kuzalisha sukari ikiwamo ardhi nzuri na soko, serikali imekuwa ikihamasisha uwekezaji wa mitaji katika tasnia ya sukari. Jitihada zinajumuisha uhamasishaji wa uwekezaji wa ndani. Katibu Mkuu anataja miradi ya uwekezaji ambayo ikikamilika, itasaidia nchi kuondokana na upungufu wa sukari.

Morogoro Mradi wa Mkulazi I na II ulianzishwa mwaka 2016 kwa ubia wa Mifuko ya Hifadhi za Jamii (NSSF na PPF/ PSSSF) chini ya Kampuni Hodhi ya Mkulazi. Kampuni hii ilianzishwa Septemba 2016 kwa lengo la kuanzisha kiwanda cha sukari nchini. Inatekeleza miradi hiyo miwili ya Mkulazi ambayo kwa pamoja inatarajia kuzalisha tani za sukari 250,000 kwa mwaka. Mradi wa Mkulazi I unatekelezwa katika shamba Namba. 217 lililopo eneo la Mkulazi, Morogoro Vijijini.

Kiwanda kinatarajiwa kuzalisha tani 200,000 za sukari kwa mwaka. Mradi una jumla ya hekta 60,103 na hekta 28,000 zimethibitika kufaa kwa kilimo cha miwa. Mradi wa Mkulazi II unatekelezwa katika shamba la Mbigiri, Kilosa. Utazalisha tani za sukari 50,000 kwa mwaka. Bagamoyo Kampuni ya Sukari ya Bagamoyo Ltd inamiliki eneo la hekta 10,000 tangu Februari, 2016 ili kuanzisha kilimo cha miwa na kiwanda cha sukari.

Imefanya utafiti wa udongo, maji, hali ya hewa, mbegu na athari za mazingira. Aidha, eneo la hekta 50 limepandwa miwa ya mbegu na eneo lingine la hekta 100 linaendelea kupandwa miwa ya mbegu itakayopandwa kwenye eneo la hekta 2,000 litakalotumika kuzalisha tani 350,000 za miwa zitakazosindika tani 35,000 za sukari kwa awamu ya kwanza inayotarajiwa kukamilika mwaka 2021.

Chamwino Wilaya ya Chamwino ilianza mikakati ya kuhamasisha uendelezaji wa zao la miwa na kuanzisha kiwanda kidogo cha sukari katika kijiji cha Dabalo, Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino. Uainishaji wa mashamba umefanyika, mafunzo ya kilimo bora cha miwa yametolewa na mashamba ya miwa ya mfano ya takribani hekta 24 yameanzishwa.

Mwaka 2016, jitihadi zilifanyika kumpata mwekezaji Purandare Industries Tanzania Ltd na akapata eneo la kusimika kiwanda cha kati kitakachozalisha wastani wa tani 4000 za sukari kwa mwaka. Hali ilivyo sasa katika kijiji cha Dabalo, wakulima wameshaanzisha chama cha ushirika na mashamba ya wakulima takribani hekta 720 yameainishwa kwa ajili ya kilimo cha miwa.

Mwekezaji ameshapata hati miliki isiyo ya asili kwa ajili ya eneo la kusimika kiwanda kutoka katika Kituo cha Uwekezaji Tanzania. Hivyo matarajio ni kwamba usimikaji wa kiwanda utakamilika Juni mwakani.

Geita Katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita, uainishaji wa mashamba ulifanyika katika Tarafa ya Butundwe na Bungando. Ilibainika kuwapo kwa takribani hekta 508 zinazofaa kwa kilimo cha miwa. Mafunzo yalitolewa kwa wakulima wa miwa na uanzishaji wa mashamba ya mfano na ilibainika kuwa maeneo hayo yanafaa kwa ajili ya kilimo cha miwa. Hatua inayofuata ni utekelezaji wa mradi kwa kufanya upembuzi yakinifu. Kasulu Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma, ina shamba lenye ukubwa wa hekta 38,000 lililopo karibu na mto Malagarasi katika vijiji vya Kigadie, Makere, Kitanga, Nyarugusu na Mvungwe.

Kampuni ya Kigoma Sugar ilisajiliwa na kuanza taratibu za kuomba ardhi hiyo kwa ajili ya uwekezaji wa kilimo cha miwa na kiwanda cha sukari. Mwekezaji wa kampuni hiyo alitoa Sh milioni 66 kwa halmashauri kuwezesha uthamini na tathmini kufanyika. Kazi hiyo imeshakamilika na kugundulika kuwa zipo hekta 37,000 kwa ajili ya uwekezaji huo.

Rufiji Kampuni ya Agroforest Plantation (MTEL) ilitoa fedha kwa ajili ya kuandaa mpango wa matumizi bora ya ardhi katika eneo la mradi na kufuata taratibu za uhaulishaji wa ardhi. Ilishawasilisha maombi ya uhaulishaji wa takribani hekta 25,000 kwa ajii ya kuwekeza katika kilimo cha miwa na kiwanda cha sukari. Maombi hayo hayajatolewa uamuzi.

Songea Kampuni ya Nkusu Theo Sugar iliwasilisha maombi ya uhaulishaji wa ardhi takribani hekta 14,000 katika Halmashauri ya Wilaya ya Songea. Maombi hayo yalikubaliwa kwa sababu yalifuata hatua zote za awali na kuwasilishwa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa hatua zaidi za uhaulishaji. Manyara Kampuni ya Suba Agro ilipewa usajili wa muda na Bodi ya Sukari Tanzania wa kusimika kiwanda cha kati cha sukari.

Mwekezaji wa kampuni hiyo ana wastani wa hekta 102.8 za shamba la miwa na uwezo wa kiwanda uliopo ni kuchakata wastani wa tani 100 za miwa kwa siku. Kiwanda kilifanya kazi kwa msimu wa 2018/19 na kuzalisha tani 20 za sukari. Vile vile kampuni ya Rift Valley Sugar iliwasilisha maombi ya kupewa usajili wa muda wa uwekezaji wa kiwanda cha kati katika kijiji cha Matufa - Manyara.

Mwekezaji huyo alipewa usajili wa muda na matarajio yake ni kusimika kiwanda chenye uwezo wa kuchakata tani 500 za miwa kwa siku. Kiwanda kina eneo la hekta 1,200 na pia kuna wakulima wadogo wenye hekta 740 kwa ajili ya uanzishwaji wa mashamba ya miwa. Kilosa Kiwanda cha Sukari cha Kilosa kinatarajiwa kuendeshwa chini ya kampuni ya Geoman Cane Estate.

Mwekezaji huyo mzawa alipewa usajili wa muda na Bodi ya Sukari Tanzania kwa ajili ya kuanzisha kiwanda cha kati chenye uwezo wa kuchakata tani 150 za miwa kwa siku. Mwekezaji anamiliki eneo lenye ukubwa wa hekta 1000. Pia wapo wakulima wadogo wanaomiliki eneo la hekta 450. Mwekezaji huyo anaendelea na utaratibu wa kupata fedha kutoka benki za nchini kwa ajili ya ununuzi wa mitambo.

Akizungumzia miradi hii na uwezekano wa bei ya sukari kushuka, Profesa Buchwashaija anasema: “Kimsingi bei ya bidhaa hutegemea hali ya ugavi na uhitaji wa bidhaa husika. Kwa kuzingatia mipango ya kuongeza uzalishaji iliyowekwa na viwanda hapa nchini na kuanzishwa kwa viwanda vipya ugavi wa sukari sokoni utaongezeka hivyo kufanya bei ya bidhaa kushuka.”

FIGO ambayo jukumu lake kubwa ni kuchuja damu na kutoa ...

foto
Mwandishi: Stella Nyemenohi

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi