loader
Dstv Habarileo Mobile
Picha

Benki ya Maendeleo ya Kilimo ilivyoleta neema kwa wakulima

ILI kuunga mkono juhudi za Rais John Magufuli katika kuijenga Tanzania ya viwanda na kutimiza ndoto zake za uchumi wa kati ifi kapo mwaka 2025, Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) kupitia Mfuko wa Dhamana kwa Wakulima Wadogo (SCGS) imekuwa ikitoa huduma za ubunifu katika maendeleo ya kilimo.

Ni katika muktadha huo, TADB inamwezesha mkulima mdogo ambaye yupo nje ya mfumo wa kifedha aweze kukopesheka. Hadi Novemba 21, mwaka wa 2019 jumla ya wakulima wadogo wapatao 108,545 kutoka mikoa 24 ya Tanzania bara na Zanzibar walikuwa wamenufaika na mikopo hiyo inayodhaminiwa na TADB pamoja na mabenki washirika ambayo tangu kuanzishwa kwa Mfuko wa Dhamana kwa Wakulima Wadogo yamejipanga kukuza mitaji ya wakulima ili kuongeza tija.

Akizungumzia mafanikio hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania, Japhet Justine, anasema kati ya wanufaika hao, zaidi ya wakulima wapatao 5,417 wamefaidika na mikopo ya moja kwa moja au kupitia vyama vya ushiriki na vikundi. Anasema wakulima wengine wapatao 103,128 waliwezeshwa kupata fursa za masoko na mitaji kupitia wanufaika wa mfuko huo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na TADB, hadi kufika Novemba 2019 kati ya Sh bilioni 36.3 ambazo zimekwishatolewa, asilimia 48 ya mikopo hiyo imewekezwa katika kukuza mnyororo wa thamani wa mazao ikiwemo ununuzi na usindikaji wa mazao na asilimia 52 iliyobaki ni mikopo iliyolenga katika uzalishaji wa mazao. Kati ya mikoa 24 ya Tanzania bara na visiwani, mikoa 10 iliyotajwa kuongoza katika kuchangamkia fursa ya mikopo hiyo imetajwa kuwa ni Mtwara, Morogoro, Simiyu, Kilimanjaro, Lindi, Dar es Salaam, Pwani, Shinyanga, Ruvuma na Mbeya.

Mafanikio hayo yanatokana na kuanzishwa kwa Mfuko wa Dhamana wa Wakulima Wadogo Wadogo ambao umerahisisha upatikanaji mikopo kwa wakulima ambao wamekuwa hawakopesheki kwa kushindwa kukidhi vigezo na masharti vinavyowekwa na mabenki ya kibiashara. Kwa kutambua changamoto hii na ili kuchagiza upatikanaji wa huduma za kifedha kwa wakulima wadogo, mwishoni mwa mwaka 2018, TADB ilianzisha mfumo mpya wa mfuko wa dhamana kwa wakulima wadogo kwa lengo la kuondoa vikwazo vya mikopo kwa wakulima wadogo.

Kupitia Mfuko huo wa SCGS, TADB imeingia makubaliano na taasisi za kifedha washirika ambapo yenyewe inadhamini asilimia 50 ya mkopo ili kuwezesha benki washirika kukopesha wakulima wadogo kwa masharti nafuu. Benki hizo washirika ni pamoja na benki za biashara za NMB, CRDB, TPB na Stanbic.

Washirika wengine ni taasisi za kifedha ikiwemo FINCA na benki za jamii zikiwemo MUCOBA, TACOBA, na Benki ya Uchumi. Tangu kuanzishwa kwake, mfumo huu umeleta chachu katika maendeleo ya kilimo kwa makundi ya vijana na wanawake. Katika kipindi cha mwaka mmoja, jumla ya wanawake 939 na vijana takribani 4478 chini ya umri wa miaka 35 wamenufaika na mfumo huu wa dhamana kwa wakulima wadogo wanaolima mazao ya mpunga, alizeti, chai, mboga na matunda, korosho, mahindi, miwa, kahawa na ufugaji wa kuku.

Mkakati wa TADB ni kuwafikia vijana na wanawake wengi zaidi na kuwapatia elimu na hamasa ili waweze kuchangamkia mikopo ya kuendeleza kilimo siku za usoni. Mapinduzi haya ya TADB ya huduma za kifedha kwa wakulima wadogo, yamekifanya kilimo kuzidi kuvutia huduma za kibenki na kuongeza ajira. Sekta ya kilimo ni muhimu sana nchini Tanzania, na kuiendeleza sekta hii ni kipaumbele kwani zaidi ya asilimia 75 ya wananchi wanategemea kilimo kama ajira zao na njia kuu ya kuwaingizia kipato.

Halikadhalika, asilimia 27 ya pato la taifa linatoka katika sekta hii. Benki za biashara na taasisi nyingine za fedha zinahimizwa kushiriki katika kuinua uchumi wa nchi kwa kushirikiana na TADB, na pia tunawahamasisha wakulima wadogo kutumia fursa za mfumo huu katika kupata manufaa katika shughuli za kilimo. Kilimo ni sekta ambayo inahitaji ubunifu wa miradi iletayo maendeleo. Utafiti pia unatakiwa kufanyika katika kutengeneza mipango ya uwekezaji katika kilimo yenye tija moja kwa moja kwa wakulima.

Mafanikio ya kilimo yatafikia pale ambapo tunaunganisha uzalishaji na uwekezaji wa viwanda, katika mnyororo wote wa thamani. Lengo la TADB ni kuendelea kuchachusha uwekezaji katika kilimo kwa kushirikiana na wadau mbalimbali. Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) ambayo ni washirika muhimu katika maendeleo na mapinduzi ya sekta ya kilimo, ilianza shughuli zake 2016.

Hadi sasa ina ofisi za tano za kanda; Dar es Salaam, Dodoma, Mwanza, Mbeya na Kigoma. TADB kama chombo cha sera kwa serikali, ina jukumu la kufungua fursa za kilimo: Jumla ya minyororo ya thamani 22 imewezeshwa kwa kupitia mikopo iliyotolewa kwa miradi 153 hadi sasa ambapo wakulima zaidi ya 1.7 kutoka mikoa 24 nchini wamenufaika, kati ya hao asilimia 33 ni wanawake. Kwa maelezo zaidi wasiliana nasi kupitia communication@ tadb.co.tz au piga simu bure 0800 110 120

IJUMAA iliyopita, tulianza kuangalia manufaa ambayo nchi inaweza kuyapata kupitia ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

3 Comments

 • avatar
  Thomas Nchama
  22/06/2020

  Mda wa kurejesha ukoje na riba ikoje?? Pia vigezo ili kupata mkopo ni vipi

 • avatar
  Thomas Nchama
  22/06/2020

  Mda wa kurejesha ukoje na riba ikoje?? Pia vigezo ili kupata mkopo ni vipi

 • avatar
  allanlwiza
  22/06/2020

  Tatapataje sisi huku mikopo ya kuanzisha ufugaji ,kahama

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi