loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Bunge, Udom na PhD ya JPM

NI miaka minne ya kazi kubwa. Ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) 2015-2020 ambao kwa hakika umekuwa wa kupigiwa mfano.

Hakuna ubishi kwamba ndani ya miaka minne ya muhula wa kwanza wa Serikali ya Awamu ya Tano ya Rais John Magufuli, makubwa yamefanyika katika kila sekta inayogusa maisha ya mwanadamu.

Chini ya falsafa yake ya “Hapa Kazi Tu” iliyomuingiza Ikulu ya Magogoni, Novemba 5, 2015, Rais Magufuli ametenda yale aliyoyaahidi katika hotuba yake wakati wa ufunguzi wa Bunge la 11, Novemba 20, 2015 mkoani Dodoma ambayo mengi pia yamo katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2015-2020.

Kwa kifupi, katika hotuba hiyo, Rais Magufuli alisema: “Mheshimiwa Spika, sikusudii kurejea mambo yote niliyoyaahidi katika hotuba yangu hii ya leo lakini nataka niwatoe wasiwasi kabisa wananchi wote kwamba tuliyoyaahidi tumeyaahidi na ahadi ni deni.”

Aliongeza, “Nataka wananchi mniamini kuwa sikutoa ahadi hii ili nipigiwe kura ya Rais, bali niliwaahidi kwa lengo la kuwatumikia na kuwafanyia kazi na hicho ndicho nitakachofanya.”

Akaenda mbali zaidi na kueleza maeneo ambayo yalilalamikiwa sana na wananchi wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa 2015.

“Eneo kubwa sana ni rushwa. Suala la rushwa limelalamikiwa sana takriban katika maeneo yote yanayowagusa wananchi.”

Akataja maeneo mengine zaidi kama Tamisemi, ardhi, bandari, maji, TRA, Tanesco, maliasili na utalii, huduma za afya, uhamiaji na ajira, elimu, polisi, mizani, madini, kilimo na mifugo, uvuvi, reli, ATC na makundi maalumu. Pia wafanyakazi, wasanii na wanamichezo, mzigo wa kodi kwa wafanyakazi, haki, maslahi yao na kadhalika.

“Kero hizi ni lazima tuzishughulikie kwa nguvu zetu zote,” aliahidi Rais Magufuli mbele ya Bunge.

Katika hotuba hiyo ambayo ilizaa msamiati wa kutumbua majipu, Rais Magufuli alifafanua kwa kina kila eneo na jinsi serikali yake itakavyojipanga kulitatua na kulipatia ufumbuzi ili kuwapa maisha mazuri Watanzania. Miaka minne baada ya hotuba hiyo, Rais Magufuli ametembea katika maneno yake. Bunge ambalo Novemba 20, 2015 lilimsikiliza kwa makini na kumshangilia kila alipoeleza mwelekeo wa serikali yake, Novemba 13, 2019 limekubaliana na maneno yake, limempongeza kwa kazi kubwa aliyoifanya.

Bunge limetaja mambo takriban 16 ambayo Rais Magufuli na serikali yake, ndani ya miaka minne, imeyatekeleza na mengi kati ya hayo, yamo katika yale aliyoyaahidi kwa Watanzania kupitia hotuba yake hiyo kwa Bunge. Kupitia kwa Katibu wa Wabunge wa CCM na Mbunge wa Bukoba Vijijini, Jason Rweikiza, Bunge linataja makubwa ya Rais Magufuli na serikali yake wakianzia na kusimamia kwa ukamilifu taratibu za makusanyo ya mapato ya serikali ambayo yamewezesha kuongezeka kwa makusanyo ya mwezi kutoka wastani wa Sh bilioni 850 hadi Sh trilioni 1.3.

Mengine ni kupunguza matumizi ya serikali yasiyo ya lazima; mathalani, safari za nje zisizo na faida wala tija kwa Taifa ambapo zilikuwa zikiligharimu Taifa mabilioni ya fedha na vilevile kuondoa watumishi hewa ambao ilibainika kuwa zaidi ya watumishi hewa 10,000 waliokuwa wakilipwa mishahara bure.

Kutoa elimu bila malipo kuanzia Elimu ya Awali hadi Kidato cha Nne katika Mpango wa Elimumsingi, kuongeza mikopo ya elimu ya juu kutoka Sh bilioni 341 (2014/2015) kwa mwaka hadi Sh biilioni 450 zilizotengwa mwaka 2019/2020, kuimarisha miundombinu katika nyanja zote, ikiwemo ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kote nchini, madaraja na barabara za juu, ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR), kufufua njia ya reli kutoka Tanga hadi Moshi.

Pia kuimarisha Bandari za Dar es Salaam, Tanga na Mtwara, miundombinu ya maji, ujenzi wa mabweni ya wanafunzi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, viwanja vya ndege na uimarishaji wa ATCL, kupambana na rushwa kwa kuimarisha Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na kuanzisha Mahakama ya Mafisadi. Mengine ni kujali wanyonge, kuinua sekta ya kilimo ikiwamo kusimamia bei yenye maslahi kwa wakulima wa korosho, pamba, kahawa na ufuta.

Pia Rais Magufuli ameweza kuimarisha sekta ya madini kwa kuongeza mapato na kutunga sheria zinazosimamia rasilimali na maliasili za nchi kwa manufaa ya Taifa, kuanzisha masoko ya madini na ujenzi wa Ukuta wa Mirerani, kuimarisha upatikanaji wa huduma mbalimbali za kijamii maeneo ya vijijini ikiwa ni pamoja na kuanzisha Wakala wa Barabara za Miji na Vijijini (TARURA) na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA); Pia kuimarisha sekta ya afya kwa kuongeza bajeti ya afya, kuimarisha Hospitali za Rufaa kama vile Muhimbili, MOI, Mloganzila na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, kujenga hospitali za wilaya takribani 69 kote nchini na vituo vya kutolea huduma ya afya 352, kupeleka umeme hasa maeneo ya vijijini.

Sambamba na hayo, Serikali ya Awamu ya Tano imeanza ujenzi wa Bwawa la Nyerere katika Mto Rufiji kuzalisha umeme wa megawati zaidi ya 2,115, ambao ukikamilika utaimarisha upatikanaji mkubwa wa umeme na hivyo kwenda sambamba na azma ya Tanzania ya Viwanda; uamuzi wa kuhamishia serikali Makao Makuu Dodoma.

Haya na mengineyo, Bunge limeyapigia saluti kwa Serikali ya Rais Magufuli ndani ya miaka minne ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM, saluti ambazo siku chache baadaye Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) ilizikubali pia.

Chuo hicho nacho kilipiga saluti kwa Rais Magufuli kutokana na mambo yake makubwa kwa nchi na Novemba 21, mwaka huu kilimtunuku Shahada ya Heshima ya Udaktari wa Falsafa katika Sayansi ya Chuo Kikuu cha Dodoma. Profesa Davis Mwamfupe anataja sababu za kumtunuku Rais Magufuli shahada hiyo. Anasema Baraza la Chuo Kikuu cha Udom lililokutana kwenye kikao chake maalumu cha 64 liliamua kumtunukia Rais shahada hiyo baada ya kuchambua ukuaji wa sekta mbalimbali na kubainisha azma yake ya kusimamia Dira ya Maendeleo ya viwanda kuelekea uchumi wa kati ifikapo 2025.

“Tulijiuliza, je, Rais John Magufuli anawezaje kulifikisha taifa hapa ikiwa ni mwaka mmoja kabla ya kipindi chake cha uongozi wa awamu ya kwanza hakijaisha. Tulibaini msingi wa mafanikio yake yapo katika aina ya uongozi wake,” alisema Profesa Mwamfupe na kuongeza kuwa walibaini Rais Magufuli ni kiongozi wa aina yake ambaye Tanzania imewahi kumpata na kuwa ni kiongozi anayejali matokeo lakini bila kuathiri ubora wa matokeo hayo.

“Rais amefanikiwa kuendeleza sekta zote za kimkakati kwa lengo la kuifikisha Tanzania kwenye uchumi wa kati ifikapo 2025 kupitia mapinduzi ya viwanda,” alisema na kuongeza kuwa shahada hiyo imetolewa pia kutokana na kutoa mchango uliotukuka katika sekta zote zinazochagiza maendeleo ya viwanda nchini ikiwa ni pamoja na elimu, nishati, miundombinu na uchukuzi, maji, mawasiliano, maliasili na utalii, afya, madini na kilimo.

Haya ndiyo ambayo Rais Magufuli ameyafanya ndani ya miaka minne ya uongozi wake ambayo siyo Bunge na Udom pekee ambao wameyaona. Watanzania wanaopenda maendeleo wameyaona, nchi nyingine za Afrika na dunia kwa ujumla wanamjua Rais Magufuli na yale aliyoyafanya ndani ya miaka yake minne.

Hakika ametembea katika maneno yaliyomo katika hotuba yake kwa Bunge la 11. Anastahili zaidi ya Shahada ya Heshima ya Udaktari wa Falsafa (PhD). Viva Rais Magufuli. Hapa Kazi Tu.

FIKIRIA tunda linaloweza kutumiwa kukuza uchumi, kutumiwa kama dawa, kiungo, ...

foto
Mwandishi: Mgaya Kingoba

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi