loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Tanzania ya uchumi wa kati ifikapo 2025 inawezekana

Tanzania kuelekea nchi ya uchumi wa kati ifi kapo mwaka 2025 ni suala ambalo mgombea urais kupitia CCM katika uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 2015, Dk John Magufuli alikuwa akilihubiri kila alipokuwa akisimama katika mikutano ya hadhara.

Alieleza kwamba serikali atakayoiunda akipewa ridhaa hiyo amekusudia iwe ambayo itabadili maisha ya Watanzania, hususani wale wenye kipato cha chini. Ili kufanikisha lengo hilo, Dk Magufuli aliwaahidi watanzania kuwa ataunda serikali ndogo ya wachapakazi ambao watawatumikia watu na hasa wananchi wa kawaida.

Aidha, aliahidi kuwa viongozi atakaowateua watakuwa wanawahudumia wananchi kwa haraka na sio kuwasumbua sumbua na kuwazungusha. Alitoa rai kwa watumishi wa serikali, hasa wale wazembe na wavivu, kujiandaa akifafanua kwamba, kwa muda mrefu watendaji serikalini wamekuwa hawawajibiki ipasavyo na sasa umefika mwisho wake kwani watumishi wa aina hiyo hawatavumiliwa katika serikali atakayoiongoza.

VIPAUMBELE

Ili kuifanya Tanzania kuwa nchi ya kipato cha kati, Dk Magufuli alielezea vipaumbele vitakavyozingatiwa katika serikali yake vikiwemo kupunguza urasimu ili kuongeza kasi ya utekelezaji wa maamuzi na miradi ya serikali; kubana matumizi kwa kupunguza yale ambayo kutokana na hali ya nchi kiuchumi kwa sasa yanaweza kuepukika; kuongeza mapato ya serikali na kurejesha nidhamu ya serikali na utumishi wa umma kwa kuongeza uwazi na uwajibikaji.

Ni dhahiri kwamba katika kipindi cha miaka minne tangu serikali ya awamu ya tano iingie madarakani chini ya Rais Magufuli kumekuwepo na mafanikio makubwa katika kutekeleza ahadi zake, ikiwemo ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya kipato cha kati ifikapo mwaka 2025. Jambo kubwa na la msingi ambalo Rais Magufuli amelifanya ni kuhakikisha kwamba sekta zote ambazo ni chachu ya maendeleo ya kiuchumi zinasimamiwa ipasavyo. Ili kuhakikisha kuwa viongozi waliopewa dhamana ya kusimamia sekta hizo wanatekeleza wajibu wao, amekuwa akifuatilia kwa karibu zaidi utendaji wao pamoja na mafanikio yanayopatikana.

WATU, ARDHI, SIASA SAFI NA UONGOZI BORA

Aidha, Rais Magufuli katika miaka hii minne hakuangalia sura ya mtu kwa maana kwamba hakusita kutengua nafasi za kiongozi yeyote aliyemteua pale inapodhihirika ameshindwa kufanya kwenda kasi yake katika kutekeleza majukumu yake. Kama ambavyo Baba wa Taifa Mwalimu Julius K. Nyerere amewahi kusema katika mikutano yake na wananchi kwamba ili nchi iweze kuendelea inahitaji mambo makubwa manne; watu, ardhi, siasa safi na uongozi bora ukitafakari uhalisia wa kauli hiyo, katika kipindi cha miaka minne cha serikali ya awamu ya tano, Rais Magufuli ameifanyia kazi kwa vitendo. Ukiacha suala la kuwatumia watu ipasavyo huku akisisitiza Watanzania kuendelea kuzaliana bila kuogopa kwa sababu watu ni mtaji, kwa upande wa ardhi, amehakikisha rasilimali zilizopo katika ardhi yetu zinatumika kama chachu ya kukua kwa uchumi wa nchi.

Sekta za kilimo, nishati, madini, utatii, uvuvi na miundombinu zinasimamiwa ipasavyo ili kuongeza pato la taifa. Amehakikisha migogoro yote inayozihusu sekta hizo inapatiwa ufumbuzi na kuanzisha mifumo mipya ya ukusanyaji wa kodi ili kudhibiti mianya ya rushwa na ukwepaji wa kodi. Ujenzi wa bwawa la kufua umeme utokanao na nguvu ya maji katika mto Rufiji wenye uwezo wa kuzalisha megawati 2,115 ameusimamia kidete pamoja na changamoto mbalimbali zilizojitokeza kutoka ndani na nje ya nchi. Amefanya hivyo akiamini kwamba, mapinduzi ya viwanda hayawezi kufanikiwa bila kuwa na chanzo cha uhakika cha nishati hiyo.

Kukamilika kwa ujenzi huo wenye thamani ya shilingi trilioni 6.5 kutakuwa chachu ya shughuli zote za uzalishaji viwandani. Aidha, kwa upande wa siasa safi na uongozi bora, Rais Magufuli baada ya shughuli za uchaguzi kumalizika, alipiga marufuku mikutano ya kisiasa kwani wakati wake ulikwishapita na sasa kilichobaki ni wananchi kufanya kazi.

Aliamini kwamba, mikutano ya kisiasa itawapotezea wananchi muda wa kuchapa kazi za uzalishaji mali na huduma nyingine muhimu za kijamii na nchi kujikuta kama ambayo iko ndani ya uchaguzi wakati wote. Katika mikutano aliyoifanya kwa wananchi kwa lengo la kuwashukuru kumchagua, Magufuli aliendelea kuwahimiza kufanya kazi badala ya kukaa vijiweni kuzungumzia masuala ya uchaguzi. Aliwakumbusha kuwa wakati utafika wa kufanya mikutano ya kisiasa pale uchaguzi mwingine utakapokaribia. Katika kuonesha umuhimu wa utawala bora, Rais Magufuli aliwatahadharisha viongozi aliowateua kuwatumikia wananchi kwa kuzingatia misingi ya utawala bora. Yeye mwenyewe ameonesha kwa vitendo jinsi ambavyo kiongozi anavyopaswa kuwanyenyekea wananchi na kusikiliza kero zao. Amekuwa akifanya hivyo kwenye mikutano ya hadhara alipokuwa ziarani sehemu mbalimbali nchini.

KUKUTANA NA WAFANYABIASHARA

Katika kutekeleza azma ya kuifanya Tanzania kuwa nchi yenye kipato cha kati, Rais Magufuli amekuwa akikutana na wafanyabiashara katika ngazi mbalimbali ili kusikiliza kero zao katika kuendesha shughuli za biashara nchini na masuala ya uwekezaji katika viwanda. Amekuwa akichukua nafasi hiyo kuelezea fursa zilizopo na jinsi serikali ilivyojipanga kuhakikisha kuwa wafanyabiashara na wawekezaji nchini wanashirikiana kwa karibu na serikali ili shughuli zao zisikwame. UTOROSHAJI MADINI Tukio kubwa la kihistoria ambalo Rais Magufuli amelifanya ni kudhibiti utoroshaji na uuzaji wa madini nje ya nchi ili kuwezesha Taifa kunufaika na rasilimali zake ikiwa ni pamoja na kufanya marekebisho ya Sheria ya Madini ya Mwaka 2010, kutunga Sheria ya Mamlaka ya Nchi Kuhusiana na Umiliki wa Maliasili ya Mwaka 2017, na ujenzi wa uzio kuzunguka eneo la migodi ya tanzanite Mirerani sambamba na kuanzisha masoko ya madini.

VIGEZO KUELEKEA UCHUMI WA KATI

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiunga mkono juhudi za Rais Magufuli amesema ili Tanzania ifikie lengo la kuwa nchi ya kipato cha kati inayoongozwa na uchumi wa viwanda, haina budi kuhakikisha kuwa inatimiza vigezo kadhaa, kikiwamo cha ukuaji wa uchumi kwa kiwango cha asilimia 12 kwa mwaka. Majaliwa anasema vigezo vingine ni mchango wa viwanda katika pato la Taifa usiopungua asilimia 15; kuongezeka kwa utoaji ajira rasmi na za moja kwa moja na kufikia asilimia asilimia 40 ya ajira zote; na sekta ya viwanda iweze kuiingizia nchi mapato ya fedha za kigeni zaidi ya asilimia 25.

Amefafanua kuwa ili kufikia vigezo hivyo na kuongeza kasi ya ukuaji wa sekta ya viwanda, serikali imejizatiti kwa kuimarisha ushirikiano wa karibu baina ya sekta ya umma na sekta binafsi, huku akizishawishi sekta binafsi kutumia fursa walizopata ili kutafakari mbinu mpya za kufikia vigezo hivyo muhimu vya kuijenga Tanzania mpya ya viwanda.

“Kila mmoja wetu anatambua umuhimu wa sekta ya viwanda katika kukuza uchumi wa nchi yoyote duniani. Viwanda ndivyo vimekuwa chimbuko la maendeleo ya haraka ya nchi mbalimbali na mhimili mkuu wa kutegemewa katika kuondoa umasikini kwa kutoa ajira nyingi na za uhakika kwa wananchi,” anasisitiza Majaliwa. Ameeleza kuwa maendeleo ya sayasi na teknolojia yanategemea sana sekta ya viwanda.

“Takwimu pia, zinaonesha kwamba katika mwaka 2018, sekta ya viwanda imetoa ajira rasmi 306,180 ikilinganishwa na ajira 280,899 za mwaka 2017; sawa na ongezeko la asilimia tisa. “Tutaendelea kuchukua hatua zinazostahiki ili kuwezesha sekta hii ikue kwa haraka na kutoa mchango mkubwa zaidi katika pato la Taifa na hivyo kuchangia katika kukuza uchumi na kuondoa umaskini wa wananchi wetu,” anasema Waziri Mkuu.

Anasema kutokana na jitihada kubwa zinazoendelea kufanywa na serikali za kujenga uchumi wa viwanda, jumla ya viwanda vipya zaidi ya 4,000 vimejengwa katika mikoa mbalimbali.

“Viwanda vilivyojengwa vinazalisha bidhaa za ujenzi (saruji, nondo, vigae, mabomba, marumaru); pamoja na viwanda vya kusindika mazao ya kilimo ikiwemo nafaka, matunda, mafuta ya kula na bidhaa za ngozi,” anasema.

Anasema viwanda vingi vimeanzishwa nchini na kwamba hiyo ni faraja kuona wawekezaji wa ndani nao wanaendelea kufungua viwanda vipya pamoja kuongeza uwekezaji wao. Moja ya viwanda vinavyohamasishwa ni vile vinavyochochea uzalishaji wa ajira kwa wingi. Ujenzi wa viwanda vipya nchini, katika kipindi cha serikali ya awamu ya tano, umechangia kupatikana kwa ajira mpya 482,601 nchi nzima,” anasema.

Waziri Mkuu anasema katika dhamira ya kufikia uchumi wa kati ifikapo 2025 unaotegemea viwanda, jumla ya ekari 127,859 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa viwanda vipya. Anafafanua kwamba serikali kwa kushirikiana na Halmashauri za Kibaha na Kilosa, imetenga hekta 2,710 za ardhi kwa ajili ya uwekezaji wa viwanda vikubwa na vidogo. Anafafanua kuwa serikali imeziagiza mamlaka hizo za upangaji zizingatie utengaji wa asilimia 10 ya kila eneo la Mpango Kabambe wa Mji kwa ajili ya uwekezaji wa biashara na viwanda.

Anasema katika mwaka 2018/2019, Serikali imeandaa Mwongozo wa Tathmini ya Mazingira Kimkakati ambao utawezesha mpango wa uchumi na viwanda kufanyiwa tathmini ya mazingira kimkakati.

“Katika maboresho ya kanuni yaliyofanyika, yanampa Waziri mwenye dhamana ya mazingira mamlaka ya kutoa vibali vya muda kwa ajili ya miradi ya uwekezaji kwenye sekta ya viwanda na hivyo kuboresha taratibu za uwekezaji wa viwanda nchini,” anasema.

Waziri Mkuu ameendelea kufafanua kuwa katika mwaka wa fedha 2019/2020, Serikali itaendelea kuhuisha, kuboresha na kutekeleza sera, sheria, taratibu na mikakati ya maendeleo ya viwanda, biashara na masoko. Anasema maboresho hayo yatahusu uongezaji wa thamani ya mazao ya kilimo, mifugo, uvuvi, misitu na madini; kuimarisha na kusimamia mfumo wa biashara ya ndani na kutumia kikamilifu fursa za masoko.

Waziri Mkuu anaongeza kuwa serikali itaendelea kujenga uwezo wa taasisi za utafiti zinazohusika na maendeleo ya viwanda na kuhamasisha uanzishaji na maendeleo ya viwanda vidogo sana, vidogo na vya kati. Kwa mujibu wa Waziri Mkuu, sekta ya madini ina mchango mkubwa katika kukuza uchumi, hivyo Serikali itaendelea kutoa kipaumbele katika kulinda rasilimali hizo kwa: ustawi, maendeleo na manufaa ya Watanzania.

“Katika hilo tuna kila sababu ya kumpongeza Rais John Magufuli, kwa kuelekeza mamlaka za Serikali kutunga Sheria ya Mamlaka ya Nchi Kuhusu Umiliki wa Maliasili Na.5 ya mwaka 2017. Sheria ya mapitio na majadiliano kuhusu masharti hasi katika mikataba ya maliasili za nchi namba 6 ya mwaka 2017 pamoja na kufanya marekebisho ya sheria ya madini sura 123.”

KUONDOA KERO ZA UWEKEZAJI

Waziri wa Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa, anasema wizara yake kwa kushirikiana na sekta binafsi itaendelea kuondoa kero zinazokwamisha ufanisi na ukuaji wa sekta ya viwanda zikiwemo kero kubwa zinazolalamikiwa na sekta hiyo. Anazitaja baadhi ya kero hizo kuwa ni ucheleweshaji wa malipo ya madai ya kodi za ongezeko la thamani (VAT) na asilimia 15 ya ziada inayolipwa na waagizaji wa sukari ya viwandani.

Kero nyingine anasema ni ushindani usio na uwiano na bidhaa za bei nafuu kutoka nje ya nchi kama vile nondo, mabomba ya plastiki, nguo na mavazi, bidhaa za ngozi na marumaru.

“Pia tutaangalia upya uwepo wa utitiri wa tozo na ada za juu zinazotozwa na taasisi mbalimbali za serikali, ongezeko la kodi ya kuagiza malighafi kutoka njeya nchini na kucheleweshwa upatikanaji wa vibali vya kufanya kazi kwa wataalamu wa kigeni wasiopatikana hapa nchini,” anasema.

Kuhusu usajili wa makampuni, Waziri Bashungwa anasema wizara hiyo kupitia Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) imekamilisha kuweka mifumo ya kusajili majina ya biashara kwa njia ya mtandao.

“Mifumo hiyo inawawezesha wafanyabiashara kusajili jina la biashara, uandikishwaji wa makampuni, usajili wa alama za biashara na usajili wa viwanda mahali popote walipo kupitia tovuti ya wakala (www.brela.go.tz).”

Hapana shaka juhudi hizo zote zilizofanyika katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Magufuli inawezeka kabisa kuifanya Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025. Dhamira aliyonayo Rais na jitihada za serikali kwa ujumla katika ujenzi wa uchumi wa kipato cha kati ni kuona sura na maisha ya Watanzania walio wengi yanafanana na nchi ya kipato cha kati.

IJUMAA iliyopita, tulianza kuangalia manufaa ambayo nchi inaweza kuyapata kupitia ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi