loader
Picha

Kocha Taifa Stars ‘amlinda’ Samatta

KOCHA wa timu ya Soka ya Tanzania, Taifa Stars, Etienne Ndayiragije amesema watu wamekuwa na matokeo mfukoni na ndio maana wamekuwa wakimtupia lawama nahodha wa timu hiyo, Mbwana Samatta.

Wadau mbalimbali wa soka walimtupia lawama Samatta wakidai kuwa nahodha huyo wa timu ya taifa hakujituma wakati wa mchezo dhidi ya Libya uliofanyika nchini Tunisia wa kufuzu kwa Michuano ya Mataifa ya Afrika, Afcon 2021 Cameroon.

Taifa Stars licha ya kuwa mbele kwa bao 1-0 lakini ilijikuta ikifungwa mabao 2-1 na Libya na kuzua mjadala mrefu kuhusu kiwango cha mchezaji huyo, ambaye kwa sasa anang’ara na klabu yake ya Genk ya Ubelgiji.

Alisema mchango anaoutoa kwa timu ya taifa ni mkubwa, lakini watu wanashindwa kuelewa, kwani wengi huwa na matokeo yao mfukoni na ndio maana wamekuwa wakitupa lawama kwa mchezaji huyo.

Alisema Watanzania wanapaswa kujua wachezaji anaocheza nao Genk ni tofauti kabisa na anaokutana nao kwenye timu ya taifa, hivyo yeye ni binadamu anakuja katika timu hivyo wanahitaji kushirikiana kutafuta matokeo.

Ndayiragije ambaye ni raia wa Burundi aliongeza kwamba timu za Afrika ni tofauti na Ulaya, kwani timu za Afrika zinapocheza dhidi ya Tanzania zimekuwa zikimkamia sana mchezaji huyo, tofauti na zile za Ulaya.

Ndayiragije alisisitiza kusema kuwa kamwe haitatokea Samatta kucheza kwa ubora kama anavyocheza Ulaya kwani mazingira ya timu ni tofauti na hata wachezaji anaocheza nao ni tofauti kabisa.

foto
Mwandishi: Tuzo Mapunda

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi