loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Simujanja zilivyorahisisha na kuboresha maisha

UKIFUMBA macho ukafi kiri kidogo, unaona itakuwaje kuendesha maisha ya sasa bila simujanja?

Mwandishi mmoja wa habari wa gazeti hili alipoulizwa umuhimu wa simujanja kwake alijibu, ni sawa na kompyuta mpakato kwake na sehemu muhimu ya maisha yake.

Anasema inamwezesha kupata taarifa kedekede mitandaoni na kusoma barua pepe kiganjani, kupiga picha zenye ubora wakati wowote, kuunganishwa na familia, marafiki na wafanyakazi wenzake kupitia mitandao ya kijamii.

“Siku hizi sihitaji kuwa na diski ya flashi (flash disc) wala modem. Nikiwa na shida ya kuchukua kitu kwenye kompyuta yangu ya ofisini ili nikikafanyie kwenye kompyuta ya nyumbani natumia simu yangu kama flash disk au ninaweza kujitumia kwenye barua pepe, kisha nikifika nyumbani natumia simu yangu kama modem kisha nafungua intaneti na kukihamishia kwenye kompyuta yangu ya nyumbani,” anasema mwandishi bila kutaka jina lake liandikwe gazetini.

Anasema mkewe ambaye ni mfanyabiashara, simujanja pia inamsaidia kumuunganisha na wateja wake.

“Vile vile inamwezesha mtu kununua bidhaa mtandaoni kupitia programu mbalimbali (apps) kama Zoom, Amazon na eBay na nyingine za aina hiyo na kupata taarifa za hali ya hewa kiganjani mwake,” anasema.

Simujanja pia inaweza kukusaidia kuangalia uelekeo wa mahali, kufika eneo husika na viashiria vya matatizo ya msongamano barabarani na pia inakuonesha barabara mbadala kwa kutumia programu ya Google Maps.

Halikadhalika kupatia simujanja yako mtu unaweza kupata burudani kama muziki, filamu, michezo, vitabu, majarida na nyinginezo.

Kwa kifupi, simujanja zimebadilisha kwa kasi kubwa maisha ya watu wengi na kurahisisha kama siyo kuboresha maisha kama anavyosema mwandishi huyo wa habari.

Kabla ya ujio wa simujanja, watu walitumia simu za kawaida kwa ajili ya kupiga simu na kutumiana ujumbe wa maandishi pekee lakini kwa sasa, kupitia simujanja kutokana na mapinduzi ya kiteknolojia yanayokua kwa kasi unaweza kufanya yote yaliyotajwa hapo juu.

Kwa mujibu wa takwimu ya tovuti ya www.statista.com/statistics/ 330695, takribani nusu ya watu wote duniani wanamiliki na kutumia simujanja.

Utafiti mmoja unaoweza kuuona katika https://saucelabs. com/blog/how-smartphones-andmobile- internet-have-changed-ourlives, uliofanywa na Benki Kuu ya Marekani mwaka 2016 unaonesha asilimia 96 ya vijana wenye umri kati ya miaka 18 hadi 24 walieleza kuwa kwao simujanja ni muhimu sana kuliko marashi na miswaki.

Pia utafiti huo ulionesha kwamba mtumiaji wa simujanja huangalia simu yake kila baada ya dakika sita na nusu.

Safari ya simujanja ilivyoanza

Simujanja ya kwanza ilikuwa iPhone iliyozinduliwa mwaka 2007. Simu hiyo inaendeshwa na mfumo wa simu ujulikanao kama mfumo wa uendeshaji simu wa Apple, (Apple’s iOS), ambao ulianzishwa na Steve Jobs na timu yake ya Macworld.

iPhone ilikuwa simu ya kwanza ambayo mtumiaji aliandika kwa kugusa kioo (touch screen) na kutoa huduma bora ya intaneti na pia kuwapa watumiaji uwezo wa kuvinjari kwenye wavuti (browse) kama ambavyo wangeweza kufanya kwenye kompyuta.

Simu ya kwanza yenye kutumia mfumo wa uendeshaji wa Android ilikuwa HTC Dream (kwa jina jingine T-Mobile G1) mwaka 2008. Simu janja ya Android ni simu ambayo hutumia mfumo wa uendeshaji wa Google uitwao Android OS.

Android ilitengenezwa kwa mara ya kwanza mwaka 2003 na Andy Rubin, mwasisi mwenza wa kampuni ya Android, aliyeanza kwa kutengeneza mfumo huo kwa ajili ya kamera za kidijiti na baadaye kubadilisha mwelekeo kwenye matumizi ya simujanja.

Mwaka 2005, kampuni ya Google iliinunua kampuni ya Android, wakati ule mfumo wa Android haukufahamika sana, watu wengi walidhani kwamba Google ingetumia mfumo huo kama nyenzo ya kuingia kwenye biashara ya simu.

Matokeo yake, Google iliingia kwenye biashara ya simu, lakini siyo kama mtengenezaji wa simu, bali kuweka mfumo wa Android sokoni kwa watengenezaji wa simu, wa kwanza ikiwa ni kampuni ya simu ya HTC, ambayo iliutumia mfumo huo wa Android kwa mara ya kwanza kwenye simu iitwayo HTC Dream, mwaka 2008.

Mfumo huu wa uendeshaji wa Android uliotumika kwenye simu za HTC Dream iliyotajwa ndiyo kitovu cha toleo la kwanza la Android (Android 1.0) mwaka 2008.

Matoleo yaliyofuata ni Android 1.5 Cupcake (2009), Android 1.6 Donut (2009), Android 2.0 Eclair (2009), Android 2.2 Froyo (2010), Android 2.3 Gingerbread (2010), Android 3.0 Honeycomb (2011), Android 4.0 Ice Cream Sandwich (2011), Android 4.1 Jelly Bean (2012), Android 4.4 KitKat (2013), Android 5.0 Lollipop (2014), Android 6.0 Marshmallow (2015), Android 7.0 Nougat (2016), Android 8.0 Oreo (2017), Android 9.0 Pie (2018) na ya sasa ni Android 10.0 (2019). Matoleo haya yataelezewa kwa kina kwenye makala yatakayofuata.

Ukuaji endelevu wa Android

Sasa yapata miaka 11 tangu mfumo wa uendeshaji wa Android uanze kutumika mwaka 2008. Ukuaji endelevu na wa kasi unaopatikana kwenye simujanja za Android za sasa ni matokeo ya matoleo mbalimbali ya mapinduzi ya kiteknolojia katika simu kupitia uboreshaji na uongezaji wa viambatanisho (features) mbalimbali ili kuzalisha na kutosheleza mahitaji ya watumiaji yasiyo na kikomo katika ulimwengu huu wenye mwendokasi wa kiteknolojia.

Je, ni viambatanisho vingapi unavyoona kwenye simujanja ya toleo la sasa la Android? Bila shaka ni lukuki!

Toleo la sasa la Android, Android 10 (2019), ni la 16 tangu ilipoanza kutumika mwaka 2008. Kila toleo linaambatana na viambatanisho vya kipekee, ambapo toleo hili jipya limejumuisha viambatanisho vya matoleo yote.

Wahenga walisema, hakuna masika yasiyo na mbu. Hivyo basi pamoja na simujanja kuwa na faida nyingi, vile vile zinaleta hasara kwa watumiaji. Hebu kwanza tuangalie faida.

Mawasiliano ya papo kwa papo

Simujanja zimeleta mawasiliano ya kisasa kwa watumiaji. Zimerahisisha mawasiliano ya moja kwa moja sehemu yoyote duniani kwa njia mbalimbali kwa kutumia programu za simu za kimawasiliano kwa njia tofauti tofauti zikiwemo ujumbe mfupi wa maandishi (SMS), kutuma matini, kupiga simu, kuwasiliana kwa njia ya video.

Itaendelea wiki ijayo

Kifo cha Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamini Mkapa ...

foto
Mwandishi: Isdory Kitunda

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi