loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Uongozi adilifu na ujenzi wa taasisi yenye maadili

Wiki iliyopita, tuliangalia namna kiwango cha juu cha elimu, kinavyoweza kusaidia katika kuhakikisha mtumishi wa umma anakuwa na uwezo mkubwa wa kujifunza mambo muhimu, kuhusu maadili ya utumishi wa umma na maadili ya kitaaluma, ili aweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi mkubwa.

Leo tunaangalia uongozi adilifu, kama mojawapo ya mambo yanayoweza kusaidia sana katika ujenzi wa taasisi zenye maadili ndani ya utumishi wa umma na hivyo kuhakikisha kuwa wananchi ambao kimsingi ndiyo wateja wa utumishi wa umma, wanafaidika na utumishi huo.

Uongozi adilifu unaweza kutafsiriwa kama uongozi unaozingatia maadili ya utumishi wa umma na maadili ya kitaaluma, katika utekelezaji wa majukumu mbalimbali ya taasisi, ili kufikia malengo ya taasisi husika.

Wanazuoni Jose na Thibodeaux katika makala yao ya mwaka 1999, walibainisha waziwazi kuwa kuna mambo mbalimbali yanayoweza kusaidia katika ujenzi wa taasisi zenye maadili na kwamba moja ya mambo hayo ni uongozi adilifu, kwa maana ya uongozi unaozingatia maadili katika kutekeleza majukumu mbalimbali ya taasisi.

Kwa kiasi kikubwa, uongozi adilifu ni muhimu katika kujenga taasisi inayotekeleza majukumu yake kwa kuzingatia maadili, kwa vile viongozi wanafanya shughuli zao kwa kuzingatia maadili ya utumishi wa umma na maadili ya kitaaluma na kwa kufanya hivyo, wanakuwa mfano bora wa kuigwa na watumishi wengine walioko chini ya viongozi hao.

Hii ndiyo maana wakati wa kuapa, watu mbalimbali walioteuliwa kushika nafasi mbalimbali za uongozi katika utumishi wa umma, wanalazimika kutoa ahadi ya uadilifu, ambapo pamoja na mambo mengine, wanatamka bayana kwamba katika kipindi chao cha uongozi na hata baada ya kipindi hicho, watakuwa waadilifu na mfano kwa watumishi wa umma na watu wengine katika kukuza na kusimamia maadili.

Ahadi hii ya uadilifu, inayowataka viongozi katika utumishi wa umma kuwa mfano kwa watumishi wa chini yao na wananchi wengine kwa ujumla, inatokana na misingi mbalimbali ya maadili kama ilivyoainishwa na Ibara ya 132 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na masharti yaliyomo katika sheria namba 13 ya maadili ya viongozi wa umma ya mwaka 1995.

Haja ya viongozi katika utumishi wa umma kuwa mfano katika maadili ya utumishi wa umma na maadili ya kitaaluma, inatokana na ukweli kwamba ni rahaisi kwa watumishi wa umma kujifunza kwa kupitia matendo mazuri ya wale walioko juu yao, kuliko wanavyoweza kujifunza kwa kusikiliza maneno mazuri na yasiyotekelezwa na viongozi walioko juu yao.

Hii maana yake ni kwamba, iwapo viongozi katika utumishi wa umma watatekeleza majukumu yao kulingana na viapo vyao, ni wazi kuwa watumishi walioko chini yao watakuwa na nafasi kubwa ya kujifunza na kuishi kulingana na matakwa ya kanuni za maadili ya utumishi wa umma na maadili ya kitaaluma.

Vile vile, uongozi adilifu katika utumishi wa umma unatoa nafasi kubwa kwa watumishi wa chini kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia maadili ya utumishi wa umma na maadili ya kitaaluma, kwavile katika mazingira kama hayo, uongozi unakuwa na uwezo mkubwa wa kusimamia maadili, ikiwa ni pamoja na kuchukua hatua dhidi ya watumishi wanaokiuka maadili.

Pamoja na umuhimu wake katika kujenga taasisi inayozingatia maadili katika utumishi wa umma, kazi ya kuanzisha uongozi adilifu siyo kazi rahisi kwa vile watumishi ambao wamekuwa wakinufaika na ukiukwaji wa maadili, hawawezi kukubali kushindwa kirahisi na kwa maana hiyo, kuna uwezekano wa watumishi hao kufanya kila linalowezekana ili kukwamisha juhudi hizo.

Hata hivyo, viongozi wakiwa imara na kushirikisha watumishi wengi iwezekanavyo katika kujenga uongozi adilifu, mazingira mazuri yatakayoanza kujitokeza, yanaweza kuwavutia watumishi wengi na hivyo watumishi hao wanakuwa na nafasi kubwa, ya kuunga mkono juhudi za uongozi katika kujenga uongozi adilifu.

Kwa mfano, kwa kuwa mambo mengi yatakuwa yakifanywa kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu mbalimbali, kuna uwezekano mkubwa wa kuondokana na aina zote za upendeleo na unyanyasaji katika taasisi na hivyo kuwafanya watumishi kufurahia uongozi adilifu.

Vilevile, watumishi wanaweza kufurahia uongozi adilifu kwa kuwa chini ya uongozi wa namna hiyo, kuna uwezekano wa maamuzi mbalimbali kufanyika kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu mbalimbali kwa lengo la kuhakikisha kuwa taasisi inafikia malengo yake na watumishi wanapta stahiki zao mbalimbali kama inavyotakiwa.

Mwisho ni vizuri ikakumbukwa kuwa uongozi adilifu hauwezi kufanikiwa katika kujenga taasisi inayozingatia maadili, bila uwezo wa mambo mengine muhimu yanatakiwa kuwepo kwa minajili ya kujenga taasisi za namna hiyo, ikiwa ni pamoja na ukuzaji wa tamaduni zinazozingatia maadili na ufuatiliaji wa wateule mbalimbali kwenye nafasi za uongozi, ili kuhakikisha kuwa wale wenye historia ya kukiuka maadili hawapati nafasi hizo za uongozi.

FIKIRIA tunda linaloweza kutumiwa kukuza uchumi, kutumiwa kama dawa, kiungo, ...

foto
Mwandishi: Dk Alfred Nchimbi

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi