loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Hadhi na heshima ya walimu, wanafunzi yarejea

SEKTA ya elimu nchini ilikuwa inakabiliwa na changamoto nyingi kwa muda mrefu. Moja ya changamoto hizo ni ubovu wa miundombinu katika shule zetu.

Katika kipindi cha miaka minne tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani, jitihada za kurejesha hadhi na heshima ya sekta hiyo kwa upande wa miundombinu zimefanikiwa kwa kiwango kikubwa kama Casmir Ndambalilo wa Idara ya Habari – MAELEZO anavyoeleza katika makala haya.

Ni vigumu kuamini kwa namna ambavyo Serikali ya Awamu ya Tano imetekeleza ahadi zake kwa wananchi katika kipindi cha miaka minne tu tangu iingie madarakani. Hii inatokana na ukweli kwamba kwa miaka kadhaa hali ya uchumi wa nchini ilikuwa si ya kuridhisha, hivyo kuwa vigumu kufanikisha shughuli nyingi za maendeleo kwa wananchi ikiwemo za sekta ya elimu.

Wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu mwaka 2015, moja ya maeneo yaliyojitokeza kwa kulalamikiwa na wananchi ni sekta ya elimu. Malalamiko hayo yaligusa uhaba wa vifaa vya kujifunzia na kufundishia, michango mingi isiyo ya lazima, malalamiko ya walimu yasiyoisha, mazingira ya kusomea ikiwa ni pamoja na majengo, madawati, ukosefu wa nyumba za walimu, n.k. yalitawala katika kipindi chote cha kampeni.

Ni dhahiri kwamba, mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alikuwa na wakati mgumu kuweza kutafakari namna atakavyotekeleza ahadi zake kwa wananchi, sio tu kero zinazohusu sekta ya elimu bali pia sekta nyingine.

Wakati wa ufunguzi wa Bunge la 11 Novemba 20, 2015, Rais John Magufuli alitaja mengi ambayo yalikuwa yakilalamikiwa na wananchi mbali na sekta ya elimu ikiwa ni pamoja na kukithiri kwa rushwa, upotevu wa mapato, kukatika kwa umeme mara kwa mara, ujangili, uduni wa huduma za afya, kiwango cha chini cha upatikanaji wa maji safi na salama, migogoro ya wakulima na wafugaji, viwanja, kuhodhi maeneo bila kuyaendeleza, mipango miji, kujenga maeneo ya wazi n.k.

Katika hotuba yake hiyo bungeni, Rais Magufuli alisema: “Nataka wananchi mniamini kuwa sikutoa ahadi hii ili nipigiwe kura ya Rais, bali niliwaahidi kwa lengo la kuwatumikia na kuwafanyia kazi na hicho ndicho nitakachofanya.”

Kwa upande wa sekta ya elimu ambayo makala haya imelenga zaidi, Dk Magufuli alisema wakati wa kampeni kwamba anatambua juhudi kubwa zilizofanywa na Serikali za awamu zilizopita katika upanuzi wa elimu ya awali, msingi, sekondari na vyuo vikuu. Hivyo akasema Serikali ya Awamu ya Tano itajielekeza katika kuongeza ubora wa elimu inayotolewa ikiwa ni pamoja na kuongeza mkazo katika masomo ya sayansi.

Aidha, aliwahakikishia wananchi kwamba vifaa vya kufundishia na kujifunzia vinapatikana ikiwa ni pamoja na maabara, vitabu, madawati. Vile vile alisema kuwa serikali itahakikisha kuanzia Januari (2016) elimu kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne inatolewa bure, wanafunzi wengi zaidi wa elimu ya juu wanapata mikopo kwa wakati na kushughulikia maslahi na kero za walimu wa ngazi zote ikiwa ni pamoja na kujenga nyumba za walimu vijijini.

Katika kipindi cha miaka minne tumeshuhudia mabadiliko makubwa yakifanyika hususan ujenzi na ukarabati wa miundombinu kuanzia shule za msingi, sekondari za ufundi na za kawaida, vyuo vya ufundi na vyuo vikuu.

Mabadiliko haya yamerejesha hadhi na heshima kwa walimu na wanafunzi, jambo ambalo limeleta hamasa kubwa kwanza kwa walimu wenyewe kuongeza ari ya kufundisha, lakini pia upande wa wanafunzi kumekuwepo na ongezeko kubwa na udahili katika shule za msingi, sekondari, ufundi na vyuo vikuu. Chuo cha Ualimu Mpuguso ni miongoni mwa vyuo vya walimu vilivyonufaika na ujenzi na ukarabati wa miundombinu yake.

Vyuo vingine vilivyonufaika na mradi huo wenye thamani ya Sh 36,475,000,000 ni pamoja na Kitangali wilayani Newala, Ndala wilayani Nzega na Shinyanga Manispaa ya Shinyanga.

Akielezea kuhusu ujenzi na ukarabati huo, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa anasema mradi ulilenga kuongeza fursa kwa wanafunzi wenye sifa za kupata nafasi ya kujiunga na mafunzo ya ualimu na shule za sekondari za ufundi na za kawaida. Anasema mradi huo umesaidia, sio tu kuongeza fursa za wanafunzi kusomea ualimu lakini pia kuongeza udahili katika vyuo vya ualimu vya serikali kutoka wanachuo 20,535 mwaka 2017 hadi kufikia wanachuo 23,835 mwaka 2018, ikiwa ni ongezeko la wanachuo 3,300.

Tukijikita katika Chuo cha Ualimu Mpuguso kilichopo kijiji cha Mpuguso, umbali wa kilometa 11 kutoka Makao Makuu ya Wilaya ya Rungwe, awali kilikuwa kinatumia majengo yaliyojengwa mwaka 1926 kwa ajili ya kutoa elimu kwa watoto wa machifu. Mkuu wa chuo hicho, Doroth Mhaiki anasema serikali imetoa zaidi ya Sh bilioni tisa kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu yake ambayo mwaka 1975 serikali iligeuza rasmi kuwa chuo cha ualimu.

Anafafanua kuwa sehemu ya kwanza ya mradi huo ilihusisha ujenzi wa mabweni mawili ya ghorofa moja yenye uwezo wa kubeba wanachuo 314 kwa thamani ya Sh 2,092,854,800 na nyumba tatu za watumishi za ghorofa moja zenye uwezo wa kuishi familia nne kila moja kwa thamani ya Sh 1,611,264,900. Aidha anasema ujenzi huo umehusisha pia nyumba moja inayojitegemea yenye thamani ya shilingi 6,059,700 na ukarabati wa nyumba nne kwa gharama ya Sh 169,974,008.

Mhaiki anafafanua kuwa Sh 388,006,054 na Sh 371,168,921 zimetumika kwa kazi za nje na dharura. Mkuu huyo wa chuo ameendelea kufafanua kuwa awamu ya pili ya ujenzi na ukarabati wa chuo hicho ulihusisha ujenzi wa majengo 2 ya ghorofa moja yenye madarasa manne kila moja kwa thamani ya Sh 2,092,854,800 na ukumbi wa mihadhara wenye uwezo wa kuchukua wanachuo 294 kwa wakati mmoja kwa thamani ya Sh 1,611,264,900.

Ujenzi huo anasema ulihusisha pia maktaba yenye thamani ya Sh 307,048,000, maabara moja ya sayansi yenye vyumba viwili, kila chumba kikiwa na uwezo wa kubeba wanachuo 40 kwa thamani Sh 298,127,275, ukumbi wa mikutano wenye thamani ya Sh 232,716,667 wenye uwezo wa kubeba wanachuo 240, vyoo vya madarasa kwa thamani ya Sh 140,274,169, ukarabati wa jengo la bafu na choo cha wasichana kwa Sh 55,729,300 na kazi za nje Sh 107,860,300. Mhaiki anasema chuo hicho sasa kimepanda hadhi kwa vile awali hakukuwa na maabara, maktaba, ukumbi wa mikutano, vyo vya kutosha na miundombinu mingine.

Aidha anasema kwa upande wa makazi ya wanachuo kumewekwa na vitanda vipya, makabati na viti. Anaongeza kwamba awali chumba kimoja walikuwa wakilala wanachuo 22 lakini kwa sasa wanalala wanachuo wanne tu. “Mradi umekuwa na tija kubwa kwa wanachuo na walimu kwa kuongeza morali ya kusoma na ufundishaji,” anasisitiza mkuu huyo wa chuo.

“Kwa niaba ya uongozi wa chuo, sina budi kuipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa kutekeleza ahadi zake alizozitoa wakati wa kampeni ya kugombea urais,” anasema Doroth Mhaiki.

FIGO ambayo jukumu lake kubwa ni kuchuja damu na kutoa ...

foto
Mwandishi: Isdory Kitunda

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi