loader
Picha

Viongozi wa upinzani nchini ‘kitanzini’

TAASISI inayojishughulisha na utoaji wa elimu kwa wanawake, vijana kuhusu masuala ya demokrasia na utawala bora (TAFEYOCO), imesema imebaini mambo mengi kuhusu Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, uliofanyika Novemba 24, mwaka huu.

Imesema imegundua hakuna uratibu kati ya viongozi wengi wa vyama vya upinzani na wanachama wao Pia, imesema walioshinda katika uchaguzi huo, wamepokea matokeo vizuri na walioshindwa wameyakubali. Kwamba kwa sasa hali ni shwari na wananchi wanaendelea na majukumu yao kama kawaida.

Kwamba hakuna matukio ya uvunjifu wa amani yaliyojitokeza, ikiwemo kuandamana, kufanya vurugu au kupinga matokeo kwa namna yoyote. Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi hiyo, Ernest John alisema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akizungumzia uangalizi walioufanya wakati wa Uchaguzi huo wa Serikali za Mitaa wa Novemba 24.

John alisema walifanya uangalizi huo baada ya kupewa kibali kutoka Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi). Kwamba walifanya uangalizi huo mikoa ya Dar es Salaam na Pwani kwa baadhi ya maeneo.

Akifafanua kuhusu uangalizi huo, alisema katika kipindi cha uchaguzi, vyama vya siasa vilipewa Mwongozo wa Uchaguzi ili wagombea wao wajaze kulingana na matakwa ya sheria, jambo ambalo lilikuwa kinyume kwa baadhi ya vyama.

“Viongozi hawakukaa na wagombea wao ili kuwaeleza kile walichotakiwa, waliona kama ni kawaida kwa wagombea kujaza wenyewe, jambo lililosababisha wagombea wengi kufanya makosa madogomadogo katika fomu zao,” alisema John.

Alitoa mfano kwa fomu za wagombea, kuwa eneo la kujaza chama wanachotoka, walishindwa kuandika kwa kirefu, badala yake wakajaza kama wanavyotamka. Kwa kuwa sheria ilikuwa ni lazima itekelezwe, ndio maana ilionekana hawana sifa.

Kuhusu kukosekana kwa uratibu, alisema walichogundua ni kwamba hakuna uhusiano mzuri kati ya viongozi wa juu na wanachama. Kwamba hata pale chama kilipoamua kujitoa kutoshiriki uchaguzi, baadhi ya wanachama na wagombea hawakupenda suala hilo. “Unakuta mgombea alishatengeneza utaratibu wake wa kushiriki akiwa tayari na timu yake ya ushindi.

Kujiondoa kushiriki kwenye uchaguzi kumewasumbua wengine,” alisema John. Aliongeza kuwa hata baada ya vyama kujitoa, bado serikali ilitakiwa kufanya jambo. Aidha, alisema wapo wagombea ambao walishinda rufaa. Lakini, baada ya uamuzi wa rufaa zao kutolewa, vyama vyao vilikuwa vimejitoa kushiriki katika uchaguzi huo, hivyo walibaki wakilalamika.

Alisema katika siku ya uchaguzi, baadhi ya maeneo wagombea walipita bila kupingwa. Pia siku hiyo wananchi wengi walishiriki kupiga kura, na hakuna sehemu yoyote paliporipotiwa uvunjifu wa amani.

“Muda mwingine wanasiasa ndio wanaowavuruga wananchi, kuna picha nyingine hutengenezwa na wanasiasa ili kuleta taharuki kwa wananchi. Hakuna aliyelalamika. Watu walipiga kura na kuondoka kwa amani,” alisema.

Mkurugenzi wa Programu wa taasisi hiyo, Emanuel Manumba alipongeza wote walioratibu uchaguzi na kutangaza matokeo, ambayo alisema yalikuwa ya haki na sawa. Katika Uchaguzi huo vyama vilivyosusia uchaguzi ni Chama cha Wananchi (CUF), Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ACT Wazalendo, Chaumma, NLD, UPDP, CCK na NCCR Mageuzi. Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilishinda uchaguzi huo kwa asilimia 99.9.

WAKURUGENZI wawili wa Kampuni ya Tanzanite One Mining Ltd ya ...

foto
Mwandishi: Lucy Lyatuu

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi