loader
Picha

‘Tutafanya kosa tukitega mgongo utamaduni wetu’

UTAMADUNI ni jinsi binadamu anavyokabili maisha katika mazingira yake, hivyo mara nyingi utamaduni wa mtu unajumuisha ujuzi, imani, sanaa, lugha, maadili, sheria, mila, desturi na vitu vingi anavyojipatia mwanajamii kulingana na mazingira anayoishi.

Utamaduni ni suala la msingi katika jamii ambapo kila mwanajamii kulingana na mazingira yake anapaswa kulinda na kuheshimu utamaduni wake ili hata akienda sehemu yeyote atambulishwe na utamaduni huo ambao ameuishi. Licha ya kwamba wapo ambao wameendelea kuheshimu na kutunza tamaduni zao za tangu na tangu, mabadiliko ya teknolojia, utandawazi na mahitaji ya uchumi ni kati ya mambo ambayo yanasababisha kwa kiasi fulani utamaduni wa watu kubadilika.

Kupitia hifadhi za taifa zinazoendelea kufunguliwa na serikali ya awamu ya tano ikiwemo ya Burigi-Chato na ya Nyerere zimetoa pia fursa wakazi wanaoishi jirani na hifadhi hizo. Kwamba watalii wa ndani na wa nje wanapozitembelea waue ndege kwa jiwe moja kwa maana ya kuona pia tamaduni za Watanzania kupitia vyakula vyao, zana za asili, ngoma za asili, mavazi, mapishi, lugha na utunzaji wa vifaa mbalimbali vinavyoelezea matumizi ya vizazi vilivyopita.

Ni katika muktadha huo, sasa wakazi wa mkoa wa Geita wanasema hawawezi kupitwa na fursa ya hifadhi ya Taifa ya Burigi-Chato pamoja na ile ya Rubondo juu ya kutangaza utamaduni wao ili kuvutia watalii wa ndani na nje ya nchi kufanya pia utalii wa kiutamaduni. Athuman Maligo (87), mkazi wa Nyantorotoro, Geita anasema kwa miaka mingi amekuwa akielimisha jamii yake juu ya kulinda utamaduni ingawa hakujua kama itakuja kutokea kuwa muhimu kwa ajili ya suala zima la utalii wa utamaduni.

Ni kwa mantiki hiyo, Maligo anaungana na wakazi wenzake wa Geita kupongeza hatua ya serikali ya kufungua hifadhi Burigi- Chato karibu na hifadhi ya Rubondo, hatua inayochochea pia wananchi kukuza utalii wa utamaduni katika eneo hilo. Licha ya kwamba anazeeka, Maligo ansema amekuwa akiendelea kutunza vifaa vya kale vilivyotumiwa na mababu zake huku pia akitoa elimu juu ya matumizi ya vifaa hivyo, masimulizi juu ya kutunza utamuduni na jinsi ya kuwa na familia bora zinaheshimu asili zao.

Anasema ingawa vitu alivyotunza ni vichache lakini amekuwa akipokea watu mbalimbali wanaokuja kumtembelea, kujifunza na kupata ushauri na kati ya hao hakuna anayekuja mikono mitupu. Anakiri kuwa teknolojia ya sasa imebadili mambo mengi kiasi cha vijana wa sasa kuanza kusahau utamaduni wao lakini anasema kuna mambo yalifanywa na mababu na hadi sasa yana maana kubwa na jamii haipaswi kuyatega mgongo.

“Nimeishi na kuona mengi na sasa nina wajukuu na vitukuu, lakini nataka niseme kwamba kuacha utamaduni nyuma ni chanzo cha kizazi kuanza kubadilika na maadili kuporomoka. Mambo yamerahisishwa hakuna anayeweza kupinga lakini hatuwezi kusahau kabisa mambo mazuri katika tamaduni zetu. Ambaye ataacha utamaduni wake ni mtumwa na hawezi kubaki salama,” anasema Maligo.

Anajivunua kuwekeza katika vikundi mbalimbali ambavyo vinaendelea kutangaza utamaduni wa mtanzania na hivyo anataka serikali wakati ikihubiri umuhimu wa kutumia teknolojia ya kisasa isiache nyuma utamaduni. Sulugwai Motonkali Mtobela ni kikundi kinachoongozwa na Maligo ambacho sasa kimeanza kujizolea umaarufu katika mkoa Geita na nje ya mkoa huo kutokana na kutunza vitu vya asili na tamaduni za makabila mbalimbali yanayopatikana ndani ya mkoa wa Geita.

Vifaa mbalimbali kama ngoma, zana mbalimbali zilizotumika zamani kwa shughuli mbalimbali, mavazi na mitishamba ndicho kitambulisho cha kwanza unapoamua kuingia rasmi katika makazi ya kikundi hiki. Kikundi hiki kinalenga kuhifadhi utamaduni uliosahaulika, kueneza habari njema za umuhimu wa kutunza utamaduni, kuihamasisha jamii kutosahau tamaduni zao pamoja na kuhakikisha watalii watakaotembelea mbuga za taifa wanapata elimu ya utamaduni wa eneo hilo.

“Mimi ndiye niliyeunda kikundi hiki na huu ulikuwa msisitizo wa familia yangu hasa babu yangu ambaye alikuwa na desturi ya kutunza vitu vya kale na jinsi vilivyokuwa vinafanya kazi na jinsi jamii ilivyozingatia maadili,” anasema Malingo.

Kundi Montonkali lilipata ursa ya kushiriki maonesho ya Tamasha la Urithi lililofanyika mkoani Geita kwa kufadhiliwa na ofisi ya mkuu wa mkoa huo na Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Sirika la Hifadhi ya Taifa (Tanapa). Katika tamasha hilo, kundi hilo lilitia fora ikiwa ni pamoja na kuwasha moto kupitia vijiti badala ya kiberiti kama walivyofanya mababu zetu.

Kikundi hicho pia kilionesha zana na njia za asili za kuwinda bila kufanya uwindaji haramu na mambo lukuki yaliyohusu utamaduni. Baadhi ya washiriki wa tamasha hilo alikuwepo pia Edina Charles (32) mkazi wa Katoro, Geita, ambaye amekuwa akitengeneza zana mbalimbali za asili tangu akiwa na umri wa miaka tisa, wakati huo akiwa darasa la tatu.

Anasema akiwa na umri wa miaka 12 tayari aliweza kufanya kila kitu alichomfundisha bibi yake kama kufinyanga vyungu, kutengeneza vikapu, ungo, kamba bila kusaidiwa na mtu yeyote na kupitia kazi hiyo yeye na bibi yake walipata pesa za kuendesha maisha yao.

Anasema hakubahatika kuendelea na masomo ya sekondari baada ya kuhitimu elimu ya msingi lakini aliendelea na kazi hiyo na hata bibi yake alipofariki dunia mwaka 2005 alimwacha akiwa na ujuzi kamili anaouendeleza. Edina mweye familia ya watoto wanne anasema anakabiliana na maisha kutokana na kuendelea kutengeneza vitu vya asili na kuviuza katika maeneo mbalimbali. Anasema anaamini ongezeko la watalii katika mkoa wa Geita kutokana na kuanzishwa kwa hifadhi ya Burigi-Chato kutaongeza pia soko la bidhaa zake za asili.

Mkuu wa mkoa wa Geita, Robert Gabriel anasema mkoa wake umebarikiwa kuwa na vikundi vingi vya utamaduni na vinavyotunza zana za asili. Anasema anaamimi kufunguliwa kwa hifadhi ya Burigi-Chato watalii wa ndani na nje, watapata pia fursa ya kujionea utamaduni wa makabila ya Geita na kujipatia zana za asili kwa ajili ya mapambo au matumizi kama anazotengeneza Edna.

Kadhalika amewahimiza wananchi na wasanii kukaa mkao wa kuchangamkia firsa ya kutangaza tamaduni walizo nazo kwa watalii wa ndani na nje. Mkuu wa mkoa anasema tamasha la aina hiyo litakuwa linaandaliwa kila mwaka kwa kushirikiana na hifadhi za taifa ili kutoa mwanya kwa watu kuonesha sanaa zao na kuwaweka pamoja wasanii mbalimbali.

Anasema ni tamasha pia litakalosaidia kutangaza kazi za sanaa na utamaduni wa mwananchi wa Geita na kutoa fursa kwa wananchi kutembelea vivutio vya utalii wa kiutamaduni kwa gharama ndogo. Kupitia tamasha hilo lililokuwa na kaulimbiu ya “Urithi Wetu ni Fahari Yetu,” vikundi mbalimbali vilihimiza Watanzania kutodharau au kuacha nyuma utamaduni wao.

MAKUBALIANO ya mkataba kati ya Serikali ya Tanzania na Kampuni ...

foto
Mwandishi: Diana Deus

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi