loader
Picha

Maporomoko Kenya na sababu zake

HIVI karibuni, Kenya imetikiswa na majanga ya maporomoko ya udongo baada ya mvua kubwa iliyonyesha na kuathiri kwa kiasi kikubwa maeneo ya Kusini ya nchi hiyo. Watu takribani 29 hadi makala haya yanaandikwa walikuwa wameripotiwa kupoteza maisha.

Maporomoko hayo yalianzia katika jimbo la Pokot mpakani mwa Kenya na Uganda na kushika kasi nyakati za usiku na kusababisha mafuriko, matope sambamba na kuharibika kwa miundombinu ya madaraja na hivyo kukata mawasiliano kwa baadhi ya vijiji.

Wataalamu na watafiti wanasema maporomoko hayo ni matokeo ya mabadiliko ya tabianchi. Wanafafanua kwamba kuongezeka kwa joto baharini kumesababisha mabadiliko ya hali ya hewa yasiyotarajiwa ikiwemo mvua kubwa katika eneo la Afrika Mashariki na hivyo watu wanapaswa kuchukua hatua za tahadhari.

Mamlaka ya hali ya hewa nchini Kenya imetoa taarifa ya tahadhari inayoeleza kuwa Kenya itaendelea kupokea kiasi kikubwa cha mvua katika kipindi cha wiki tatu zijazo inayoweza kusababisha mafuriko katika maeneo mbalimbali. Maporomoko ni nini? Maporomoko ya ardhi au udongo hutokea pale ardhi inapodhoofika na kutikisika kiasi cha kuporomoka, kwa sababu mbalimbali ikiwemo mvua kubwa.

Maporomoko ya ardhi yanaweza kuwa ya mawe, vifusi vya udongo au kuporomoka kwa udongo katika maeneo ya mteremko. Maporomoko haya yanaweza kutokea katika hali ya taratibu na kuleta madhara ya polepole au kwa kasi kubwa na kusababisha uharibifu mkubwa wa mali na hata vifo. Tafiti zinaonesha kuwa mahali ambapo maporomoko yanatokea yalishawahi kutokea awali hivyo ni tukio kujirudia.

Sababu za maporomoko Sababu ya kwanza kubwa ya maporomoko ya ardhi ni nguvu ya uvutano inayotokea na kusababisha mtikisiko katika uso wa ardhi na kuleta maporomoko. Sababu za asili ni pamoja na mabadiliko ya muda mrefu ya hali ya hewa ambayo yanaweza kusababisha kutikisika na kudhoofika kwa udongo na baadaye kuporomoka. Hali ya usimbisishaji nayo inaweza kuwa sababu kubwa ya maporomoko ya ardhi.

Usimbisishaji ni hali ya kuongezeka kwa kiasi cha joto ardhini kinachozalisha hewa yenye joto kali na mvuke kuelekea juu na inapofika juu huanza kupoa na kutengeneza matone madogo madogo ambayo huunganika na kuwa makubwa ambayo baadaye huanguka kama mvua, theluji au mvua ya mawe. Mvua inaposhuka na kukutana na ardhi iliyotikishwa na kukosa nguvu katika maeneo ya miteremko ndipo maporomoko ya ardhi au udogo hutokea.

Tetemeko la ardhi pia linaweza kuwa sababu ya maporomoko ya ardhi. Wakati wowote tetemeko linapotokea hutikisa uso wa ardhi na kiasi kikubwa cha udongo unahama na kama hali hiyo ikitokea katika maeneo yenye mteremko huweza kusababisha kuporomoka kwa udongo na mawe.

Sababu nyingine za asili za maporomoko ya udongo ni pamoja na mmomonyoko wa udongo na kulipuka kwa volkano. Endapo mlipuko wa volkano unatokea wakati ardhi ikiwa na unyevu au ikiwa imelowa inaweza kuleta maporomoko ya ardhi kutokana na kushindwa kushikilia miamba na vitu vingine vilivyomo.

Sababu za kibinadamu Pamoja na kuwa tunasema maporomoko ya ardhi ni majanga ya asili bado zipo sababu zinazoletwa na binadamu katika shughuli mbalimbali wanazofanya. Shughuli za uchimbaji wa madini migodini kwa kutumia baruti zinaweza kusababisha maporomoko ya ardhi kutokana na mtikisiko unaotokea ardhini wakati wa kulipua baruti unaosababisha kudhoofika kwa udongo.

Uvunaji wa misitu bila kupanda miti mingine na kuacha eneo husika likiwa wazi unaweza kudhoofisha udongo na kusababisha maporomoko ya ardhi. Mizizi ya mimea huiongezea ardhi nguvu hivyo wakati miti inapokatwa inafaa kupandwa mingine ili ardhi iendelee kuwa na nguvu kwa faida ya vizazi endelevu. Mabadiliko ya tabianchi pia kwa sehemu kubwa yanasababishwa na shughuli za binadamu zinazoharibu mazingira.

Makala haya yameandaliwa na Anna Mwikola kwa msaada wa vyanzo mbalimbali vya habari.

AWAMU ya Kwanza ya Serikali ya Tanzania iliyoongozwa na Mwalimu ...

foto
Mwandishi: Anna Mwikola

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi