loader
Picha

Kwa njia hizi Kiswahili kitapiga hatua

AWALI ya yote tupate usuli kidogo kuhusu hali ya lugha ya Kiswahili kwa sasa. Matumizi ya lugha ya Kiswahili yanazidi kuongezeka kila siku kutokana na ongezeko la watumiaji wake kutoka katika nchi mbalimbali barani Afrika na duniani kwa ujumla.

Miongoni mwa nchi hizo ni Tanzania, Kenya, Uganda, Congo, Rwanda, Burundi na Msumbiji. Nchi hizi ndizo zinazojulikana zaidi kwa matumizi ya lugha ya Kiswahili duniani, licha ya hivyo lugha ya Kiswahili inafundishwa katika vyuo mbalimbali duniani kama vya Namibia, Ujerumani, Uingereza, China, Uholanzi, Korea, Misri na Marekani.

Hizi ni baadhi tu ya nchi ambazo zinafundisha lugha ya Kiswahili katika baadhi ya vyuo vyao. Afrika Kusini imeazimia ifikapo mwaka 2020 wataanza kufundisha lugha ya Kiswahili katika mfumo wao wa elimu ya shule za msingi. Huu ni mwanzo mzuri katika kuikuza lugha ya Kiswahili duniani. Nchi zilizopendekezwa katika usaidizi wa kutoa walimu ni nchi za ukanda wa Afrika Mashariki.

Nchi ya Kenya imekuwa maarufu sana katika kujitangaza na kuandika vitabu vingi vya Kiswahili, hatua inayowafanya Wakenya waonekane zaidi ya Tanzania na nchi nyingine za Afrika ya Mashariki katika kukiendeleza Kiswahili. Yafuatayo ni mapendekezo kuhusu mambo ya kufanya ili kukikuza Kiswahili. Mambo haya yanahusisha sekta mbalimbali zinazopaswa kutimiza majukumu yao ili kukifanya Kiswahili kionekane na watu wazidi kukipenda na kutamani kujifunza na kukitumia.

Mapendekezo haya yanawahusu wanajamii wenyewe, viongozi wa nchi, wataalamu wa lugha ya Kiswahili, walimu wa Kiswahili na waandishi wa vitabu. Wanajamii wanapaswa kujivunia katika kutumia lugha ya Kiswahili na kuachana na kasumba ya kuziona lugha za kigeni kuwa ni bora kuliko lugha ya Kiswahili kwani hakuna lugha iliyo bora kuliko lugha nyingine kwa kuwa lengo kuu la lugha ni kukidhi haja ya mawasiliano baina ya wazungumzaji.

Hivyo, wanajamii wa lugha ya Kiswahili wanapaswa kuwa wazalendo wa lugha yao, kwanza katika kupata maarifa lakini pili kujifunza lugha nyingine katika kuongezea maarifa yao. Viongozi wa nchi nao wanapaswa kujikita zaidi katika matumizi ya lugha ya Kiswahili kwani wakifanya hivyo wanawahamasisha hata wananchi wao katika matumizi ya lugha ya Kiswahili na kujivunia lugha yao.

Kutokana na mamlaka waliyonayo viongozi, mathalani, rais, mawaziri, wabunge, wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya na madiwani hawana budi kujivunia lugha ya Kiswahili na hata kuitumia katika shughuli zao za kila siku. Wakifanya hivyo, wananchi wanaowasikiliza watavutiwa na matumizi sahihi ya lugha ya Kiswahili kutoka kwa viongozi wao. Wataalamu wa lugha ya Kiswahili na walimu wa Kiswahili hawana budi kuandika na kuchapisha vitabu vingi iwezekanavyo na kusisitiza matumizi sahihi ya lugha ya Kiswahili bila ya kukiharibu.

Maarifa mengi hupatikana katika vitabu, hivyo, hatuna budi kuandika vitabu vingi vya lugha ya Kiswahili na hata kuandaa makongamano kuhusu lugha ya hii. Aidha tunapaswa kuunda vikundi mbalimbali vya lugha ya Kiswahili na hata kuandaa matangazo bora katika redio na runinga ya kuelezea mada mbalimbali zinazohusu lugha ya Kiswahili. Aidha, kuna matumizi ya mitandao ya kijamii ambapo kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia, tunaweza tukatumia mitandao ya kijamii katika kujitangaza na kukitangaza Kiswahili ulimwenguni mathalani katika vikundi sogozi.

Kufanya hivyo kutaifanya Tanzania kujulikana kama nchi yenye kukipenda, kukijua na kukithamini Kiswahili ulimwenguni kote. Hii itasaidia hata katika fursa za Kiswahili zinazotangazwa kwa Tanzania kupewa kipaumbele kwenda kufundisha, mathalani Afrika Kusini na nchi nyingine duniani kutokana na kuwa na wataalamu wanaokidhi mahitaji hayo.

Vilevile, watungaji wa Sera ya Elimu nchini Tanzania wanapaswa kukipa kipaumbele Kiswahili kuwa lugha ya kufundishia kuanzia shule za msingi hadi vyuo vikuu kwani wakifanya hivi maarifa yatapatikana kwa urahisi zaidi kwa vile wanafunzi watakuwa wanatumia lugha waliyoizoea na katika mazingira yao. Hatua hii itakuza uelewa wa kiwango cha juu zaidi.

Pia, nchi itapata wataalamu wengi zaidi na vilevile inabidi kusisitiza au kufanya ni lazima kwa kila mwanafunzi katika kujifunza kwake ni lazima ajifunze na lugha nyingine ili kujiongezea maarifa kama wafanyavyo mataifa mengine mathalani Ujerumani, China, Japani, Marekani pamoja na India. Tukiiga mfano huu tutaitambulisha lugha yetu na pia tutakuza uchumi wa nchi yetu.

Zaidi ya hayo, vyombo vya katika jamii maana hutoa taarifa mbalimbali kwa wanajamii. Hivyo, vyombo hivi vishirikiane na wataalamu wa lugha ya Kiswahili na taasisi zinazoshughulikia Kiswahili kama vile Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA), Baraza la Kiswahili la Zanzibar (BAKIZA), Taasisi ya Taaluma za Kiswahili ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (TATAKI) na vyama vya wahadhiri na wanafunzi wanaosoma Kiswahili. Ushirikiano huu unaweza kuwa katika maandalizi ya vipindi na matangazo.

Jambo hili ni muhimu katika kuikuza lugha ya Kiswahili maana taarifa wanazotoa zitawafikia wanajamii kwa wakati, nao wataona umuhimu wa kujivunia na kutumia lugha ya Kiswahili kwa usanifu na ufasaha. Nihitimishe kwa kutoa rai kwamba jukumu la kukiendeleza Kiswahili ni la kila mmoja wetu mahali popote alipo.

Makundi yaliyotajwa katika makala haya ni mifano tu. Tunaamini kuwa yako makundi mengine mengi ambayo yakiwajibika Kiswahili chetu kitapiga hatua kubwa. Hivyo, tuanze kwa pamoja na kwa kila mtu mahali alipo kujitahidi kuhakikisha kwamba Kiswahili chetu kinapiga hatua kutoka hapa kilipo na kwenda mbele zaidi. Tujivunie Kiswahili. Mwandishi wa makala haya ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam aliyekuwa Bakita kwa mafunzo ya vitendo.

MSIMU wa Ligi Kuu Tanzania Bara 2019/2020 utarejea tena Juni ...

foto
Mwandishi: Denis Genes

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi