loader
Picha

Kivumbi Yanga, Alliance leo

TIMU ya soka ya Yanga leo itakuwa ugenini jijini Mwanza kuikabili Alliance katika mchezo wa Ligi Kuu soka Tanzania Bara utakaochezwa kwenye Uwanja wa CCM, Kirumba.

Ni mchezo mgumu kwa pande zote mbili zikihitaji matokeo mazuri ili kupanda nafasi za juu. Yanga imeshacheza michezo sita ikiwa ndio timu pekee yenye viporo vingi, kati ya hivyo walishinda minne, kupata sare moja na kupoteza mchezo mmoja wakiwa wanashika nafasi ya 15 kwa pointi 13. Alliance imecheza michezo 12, imeshinda minne, sare tano, imepoteza mitatu wakishika nafasi ya 11 kwa pointi 17.

Timu hizo zilipokutana mara ya mwisho kwenye uwanja huo msimu uliopita, Yanga ilipata ushindi wa tabu wa bao 1-0. Zilipokutana msimu uliopita timu zote mbili zilikuwa na vikosi vingine na benchi la ufundi tofauti, na sasa kuna mabadiliko kwa kila kikosi lakini huenda wamesomana na kila mmoja kujua udhaifu wa mwenzake.

Tangu Yanga imechukuliwa na Kocha Charles Mkwasa aliyerithi mikoba ya Mwinyi Zahera, imeshashinda michezo miwili iliyopita. Mmoja wa nyumbani na mwingine wa ugenini. Mchezo wao uliopita walishinda kwenye uwanja wao wa nyumbani wa Uhuru kwa mabao 3-2 dhidi ya JKT Tanzania. Kwa upande wa Alliance imetoka kupoteza mchezo uliopita dhidi ya Azam FC baada ya kufungwa mabao 5-0.

Yanga bado safu yake ya ushambuliaji na ulinzi sio bora kwani wamefunga jumla ya mabao tisa na kufungwa sita na hata kwa Alliance bado hawako vizuri pia katika umaliziaji wakionekana kucheza kwa kujihami zaidi huku safu yao ya ulinzi ikiruhusu kufungwa mabao 13 na kushinda 10. Timu zote zina nafasi ya kupata matokeo kutegemea na walivyojiandaa kimbinu.

Wachezaji hatari wa Yanga ni Patrick Sibomana, Juma Balinya na David Molinga lakini kazi ipo kwani Alliance ina kikosi cha vijana wenye kasi na wanaweza kufanya lolote dhidi ya wakongwe hao.

foto
Mwandishi: Grace Mkojera

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi