loader
Picha

PPRA yanusa ufisadi wa mabilioni

MAMLAKA ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) imesema tathmini ya rushwa iliyoifanya kwa mikataba 39 ya manunuzi ya umma katika taasisi 39 za ununuzi (PEs) imeonesha kuwa na viashiria vya juu vya rushwa.

Mikataba 12 yenye thamani ya Sh bilioni 25.8 kutoka taasisi tisa za ununuzi ilikuwa na alama za juu za viashiria vya rushwa katika tathmini ya jumla.

Kwa mujibu wa Ripoti ya Mwaka ya PPRA kuhusu Tathmini ya Utendaji katika Ununuzi wa Umma kwa Mwaka wa Fedha 2018/19, mikataba hiyo ilikuwa ikitekelezwa na Wizara ya Maji, Shirika la Reli Tanzania (TRC) na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA).

Taasisi zingine zilizokuwa zikitekeleza mikataba hiyo ni Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Mamlaka za Maji Safi na Maji Taka Singida na Wang’ing’ombe (UWASA), manispaa za Kigamboni na Ubungo na Halmashauri ya Mji Kahama (Kahama TC).

Katika hatua nyingine, PPRA pia ilifanya uchunguzi kwa taasisi tano za ununuzi zinazohusika na zabuni au mikataba. Taasisi hizo ni Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi, Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Wakala wa Nishati Vijijini (REA) pamoja na TBS.

Thamani ya zabuni au mikataba iliyochunguzwa kwa mujibu wa ripoti hiyo ni Sh bilioni 375.05 na chunguzi hizo ziliweza kuokoa Sh bilioni 3.39 ambazo zingetumiwa vibaya na wazabuni au maofisa wa serikali.

“Uchunguzi zaidi ulibaini kuwa serikali ilipata hasara ya Sh bilioni 4.36 kutokana na ada ambayo ingelipwa serikalini pamoja na kubadilishwa michoro ya miradi hali iliyosababisha kutelekezwa kwa baadhi ya kazi zilizokuwa zikitekelezwa na bidhaa zilizokwishanunuliwa,” ilieleza taarifa hiyo ambayo iliwasilishwa bungeni hivi karibuni.

Mbali na tathmini na chunguzi hizo, kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu na thamani ya fedha, mamlaka hiyo pia ilikagua jumla ya mikataba ya ununuzi 7,738 yenye thamani ya Sh trilioni 9.122.

Ukaguzi huo ulizihusu taasisi za ununuzi 104 zikiwemo Wizara, Idara na Wakala 43, Mamlaka ya Serikali za Mitaa 28 na Mamlaka za Umma 33 pamoja na matawi matano ya taasisi za ununuzi yaliyokasimiwa mamlaka ya ununuzi.

Katika hilo, taarifa hiyo ilieleza kuwa taasisi za ununuzi 43 zilifanyiwa tu ukaguzi ili kubaini kama zilizingatia sheria, kanuni na taratibu, taasisi moja ilikaguliwa kuona kama thamani ya fedha ilizingatiwa na taasisi 60 za ununuzi pamoja na matawi matano ya taasisi za ununuzi zilikaguliwa kwa kuzingatia vigezo vyote viwili ikiwemo sheria, kanuni na taratibu pamoja na thamani ya fedha.

Ripoti hiyo imeelezwa kuwa kati ya taasisi zilizokaguliwa, taasisi 18 za ununuzi ambazo ukubwa wa manunuzi yake ulikuwa Sh bilioni 20 au zaidi yalikuwa asilimia 96.3 ya mikataba yote iliyokaguliwa, huku kiwango cha wastani wa jumla katika kuzingatia sheria, kanuni na taratibu kilikuwa asilimia 76 kati ya asilimia 80 zilizokusudiwa ikilinganishwa na asilimia 74 katika mwaka wa fedha uliopita wa 2017/18.

Kuhusu thamani ya fedha, PPRA pia ilikagua mikataba ya ununuzi 290 yenye thamani ya Sh bilioni 8,478.33. Mikataba iliyokaguliwa inajumuisha ya majengo, barabara, madaraja na kazi za kiraia yenye thamani ya Sh bilioni 996.82.

Mikataba mingine ni ile ya kazi za umeme zenye thamani ya Sh bilioni 25.85; kazi za ujenzi wa reli zenye thamani ya Sh bilioni 7,222.43; miradi ya usambazaji maji na umwagiliaji yenye thamani ya Sh bilioni 60.11; bidhaa zenye thamani ya Sh bilioni 124.84 na huduma za ushauri zenye thamani ya Sh bilioni 48.24.

Kwa mujibu wa PPRA, kati ya mikataba 290 iliyokaguliwa kwa kuangaliwa thamani ya fedha, mikataba 239 yenye thamani ya Sh bilioni 8,407.68 ilitathiminiwa na kupata utendaji unaoridhisha; mikataba 49 yenye thamani ya Sh bilioni 70.56 ilitathminiwa na kupata utendaji mzuri na mikataba miwili yenye thamani ya Sh milioni 95.32 ilitathminiwa na kupata utendaji mbaya.

Taarifa hiyo ya PPRA ni ya 13 kutolewa na tangu Mamlaka hiyo ianze kazi mwaka 2005.

WAKURUGENZI wawili wa Kampuni ya Tanzanite One Mining Ltd ya ...

foto
Mwandishi: Matern Kayera

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi