loader
Picha

Hospitali zaagizwa zipime wajawazito na wenza wao

SERIKALI imeziagiza hospitali, vituo vya afya na zahanati zote nchini zikiwamo zinazomilikiwa na watu binafsi na taasisi za dini kufuata mwongozo wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kuhakikisha kila mjamzito anapimwa Virusi Vya Ukimwi akiwa na mwenza wake.

Pamoja na hayo, imesisitiza kuwa imejiwekea malengo kwamba ifikapo mwaka 2030, Tanzania lazima iwe imetokomeza kabisa ugonjwa huo.

Aidha, serikali imebainisha kuwa pamoja na kwamba takwimu zinaonesha kuwa wasichana ndio waathirika wa Ukimwi zaidi kuliko wavulana, lakini wameambukizwa ugonjwa huo na watu wazima.

Hayo yameelezwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu wakati akizungumza kuhusu maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani iliyoadhimishwa jana duniani kote, kwenye kipindi cha Tuongee Asubuhi kinachorushwa na televisheni ya Star TV akiwa jijini Mwanza.

Ummy amesema tayari hospitali, vituo na zahanati za serikali zinatekeleza mwongozo huo wa kumtaka kila mjamzito kupima VVU akiwa na mwenza wake, lakini kuna baadhi ya hospitali na vituo binafsi havifuati mwongozo huo.

“Ni lazima tuwe na dhamira ya kweli kutokomeza ugonjwa huu na moja ya mkakati ni kuhakikisha watu wengi zaidi wanapima Ukimwi wakiwemo mama mjamzito na mwenza wake,” amesisitiza Ummy.

Alisema agizo hilo pia ataliandika kwa maandishi na kulisambaza nchi nzima ili kuhakikisha idadi kubwa ya wanaume nao wanapima tofauti na sasa ambapo wengi wanawaachia zaidi wake zao.

Alisema tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani hali ya maambukizi ya Ukimwi kati ya mama mjamzito kwenda kwa mtoto ilikuwa ni asilimia 12 kati ya akinamama 100 lakini kwa sasa maambukizi hayo yamepungua na kufikia asilimia 4.8 kati ya akinamama 100.

Alieleza kuwa hali hiyo imetokana na ukweli kuwa kwa sasa mwitikio wa wajawazito kupima Ukimwi ni mkubwa kwa zaidi ya asilimia 90 tofauti na mwanzo.

Hata hivyo, alifafanua kuwa ili kufikia azma ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kutokomeza ugonjwa huo ifikapo mwaka 2030, ni lazima kufikia asilimia 90 ya watanzania waliopima na kujitambua hali zao.

Alisema hadi sasa jumla ya Watanzania milioni 1.6 wanaishi na Virusi Vya Ukimwi nchini ambapo tangu kampeni ya kupima kwa hiari ianzishwe asilimia 78 ya Watanzania sasa wanatambua hali zao kutoka asilimia 52 ya awali.

Alisema katika maambukizi hayo mapya 72,000 asilimia 40 ni vijana wanaoanzia miaka 15 hadi 24 ambao kati yao asilimia 80 ni wasichana na asilimia 20 ni wavulana.

“Sababu hasa ni kwamba wasichana wengi wanaanza kujihusisha kwenye mapenzi wakiwa na umri mdogo kuliko wanaume,” alisisitiza Ummy.

WAKURUGENZI wawili wa Kampuni ya Tanzanite One Mining Ltd ya ...

foto
Mwandishi: Halima Mlacha

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi