loader
Picha

TRC yajaribu treni Dar -Moshi

USAFIRI wa treni kutokea Dar es Salaam kwenda Moshi mkoani Kilimanjaro utafanyika wakati wa usiku, huku treni hiyo ikianza majaribio ya siku mbili ya kuangalia ufanisi wa treni hiyo jana.

Akizungumzia safari ya treni hiyo itakayoanza Desemba 6, mwaka huu, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa alifafanua kuwa treni hiyo itakuwa ikifanya safari zake usiku kwa kuondoka Dar es Salaam kwenda Moshi na kurejea Dar es Salaam kuanzia jioni na kushika safarini usiku kucha kabla ya kufika kituo husika asubuhi.

Kadogosa amesema jana watendaji wa TRC wakishirikiana na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (LATRA), walisafiri kutokea Dar es Salaam kwenda Moshi ikiwa ni matakwa ya kisheria yanayoitaka TRC kufanya majaribio ya safari zake kwanza kabla ya kuanza kwa safari rasmi.

Alisema leo usiku treni hiyo itaondoka Moshi kurejea Dar es Salaam ikiwa ni jaribio la kuangalia uwezo wake wa kusafiri usiku.

“Hapa ninaongea na wewe tumefikia Korogwe na tunaendelea na majaribio ya usafiri huu, ni safari ya treni nzima kwa maana ya mabehewa yote yapo kwenye majaribio,” alisema Kadogosa jana saa alasiri.

Aliongeza: “Tupo na wadau wote wa usafiri wa ardhini ambao kila mmoja atatoa tathimini yake kuhusiana na usafiri huu kwa namna walivyouona na TRC itatoa tathmini kamili kabla ya kuanza kwa usafiri huu.”

Usafiri huo wa treni kwenda mikoa hiyo ya Kanda ya Kaskazini ulisitishwa miaka mingi iliyopita na ulipaswa kuanza Septemba 5, mwaka huu lakini ukasogezwa mbele hadi hiyo Desemba 6, kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo ya kutokamilika kwa miundombinu yake kutokana na mvua.

Kuanza kwa usafiri huo itakuwa ni neema kwa wasafiri wanaokwenda mikoa inayopita treni hiyo hasa wanaoenda mkoani Kilimanjaro ikizingatiwa kuwa inaanza wakati wa kipindi cha mwisho wa mwaka ambacho kunakuwa na abiria wengie wanaokwenda mkoani Kilimanjaro kwa mapumziko ya Sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya.

Usafiri wa treni ni nafuu kwao kutokana kiwango kidogo cha nauli kitakachokuwa kikitozwa ikilinganishwa na kiwango cha nauli ya mabasi ya kawaida ambayo huanzia Sh 20,000 huku bado kukiwa na uhuni wa kuongeza bei iya nauli bila utaratibu maalumu.

Bei za usafiri wa treni kutokea Dar es Salaam hadi Korogwe daraja la tatu itakuwa Sh 10,700, daraja la pili kukaa itakuwa Sh 15,300 na daraja la pili kulala Sh 25,400.

Usafiri wa Dar es Salaam kwenda Moshi daraja la tatu itakuwa Sh 16,500, daraja la pili itakuwa Sh 23,500 na daraja la pili kulala Sh 39,100.

Tangu kuingia madarakani miaka minne iliyopita, Rais John Magufuli amekuwa akisisitiza nia ya serikali yake ya kuimarisha miundombinu ya usafiri, ambao tayari amerejesha usafiri wa treni ya mizigo ya Tanga – Moshi na sasa usafiri huo wa abiria wa Dar es Salaam – Tanga – Moshi ambao ulikuwa maarufu miaka ya nyuma.

Licha ya kuhakikisha usafiri huo wa treni ya kaskazini unarejea, ameanza mchakato wa treni ya umeme kutokea Dar es Salaam hadi Makao Makuu ya Nchi Dodoma, huku katika sekta ya anga akiwa amenunua ndege nane na akiendelea na ujenzi wa barabara na madaraja sehemu mbalimbali za nchi.

WAKURUGENZI wawili wa Kampuni ya Tanzanite One Mining Ltd ya ...

foto
Mwandishi: Evance Ng’ingo

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi