loader
Picha

Wanafunzi vyuo vikuu kuishi nyumba za NHC, NSSF

WAZIRI Mkuu, Kasssim Majaliwa ameagiza nyumba 1,500 zilizopo katika miradi ya Shirika la Taifa la Hifadhi ya Taifa (NSSF), Shirika la Nyumba (NHC) pamoja na Watumishi Housing zilizopo Toangoma na Mtoni Kijichi zitolewe kwa vyuo vya elimu ya juu vilivyopo Dar es Salaam ili kuwawezesha wanafunzi kupata makazi ya gharama nafuu.

Aidha, amewataka wakuu wa vyuo hivyo na wakurugenzi wa mashirika hayo kukutana pamoja ili kuona namna ya utekelezaji wa suala hilo linalolenga kuyafanya majengo hayo kutumika.

Waziri Mkuu ameyasema hayo jijini Dar es Salaam wakati wa Mahafali ya 45 ya Chuo Cha Usimamizi wa Fedha (IFM) ambako pamoja na mambo mengine, amesema ofisi yake itatoa majengo yaliyokuwa yakitumiwa na wizara mbali mbali kwa vyuo hivyo ili kutatua uhaba wa majengo unaovikabili.

“Nimeshatoa maelekezo kwa wakuu wa mashirika hayo kuona namna bora ya matumizi ya majengo hayo ambayo mengi yamekamilika lakini hayatumiki, hatua hii naomba utekelezaji wake ufanyike haraka ili kuwapa fursa hiyo wanafunzi,” alisema Majaliwa na kuibua shangwe kutoka kwa wanafunzi.

Pia alisema ili kuhakikisha wanafunzi watakaoishi katika nyumba hizo wanaondokana na adha ya usafiri, ameagiza wa wakuu wa wilaya zote za Dar es Salaam, kukutana na Mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu (LATRA) ili kupanga vizuri njia za usafiri kutoka Kigamboni, Tuangoma, Mtoni Kijichi hadi Feri ili kurahisisha usafiri kwa wanafunzi hao.

Aidha, aliwataka wahitimu kwenda kuwa mfano bora katika jamii na kufanya kazi kwa bidii pindi watakapopata ajira, huku akitoa wito kwa vyuo kuhakikisha vinawafundisha wanafunzi mbinu bora za kujiajiri badala ya kutegemea kuajiriwa.

Alisema Tanzania kama zilivyo nchi nyingine duniani inakabiliwa na changamoto ya ajira ambayo katika kukabiliana na hali hiyo, serikali katika kipindi cha miaka minne imeongeza wigo wa utoaji ajira kutoka milioni 20 mwaka 2014 hadi milioni 22 mwaka jana.

Kwa upande wake, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango amesema uwepo wa IFM umekuwa msaada mkubwa kwa serikali kutokana na kuzalisha wataalamu mbali mbali wanaofanya kazi katika usimamizi wa kodi, bima na uhifadhi wa jamii na kuiomba serikali kuendelea kukisaidia chuo hicho ili kizidi kutimiza malengo yake.

Aidha, alisema katika kuhakikisha chuo hicho kinatimiza malengo yake, serikali imekuwa ikikiachia fedha zote chuo hicho zinazotokana na ada ili kukiwezesha kijiendeshe katika maendeleo na kwamba ili kuonesha kuwa kina uwezo huo, hivi karibuni kilitoa gawio serikalini kiasi cha Sh bilioni mbili.

Awali Mkuu wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha, Profesa Thadeo Satta alisema tangu kuanzishwa kwake mwaka 1972 kikiwa na wanafunzi 72, kimeendelea kupitia hatua mbali mbali za kimaendeleo ikiwemo kuongeza udahili wa wanafunzi uliokiwezesha kufikisha wanafunzi 10,820 katika mwaka wa masomo 2019/2020.

Alisema juhudi mbalimbali kutoka kwa wahadhiri wa chuo hicho umekuwa ukitoa matunda mazuri kwa wahitimu chuoni hapo huku akimueleza Waziri Mkuu mipango ya upanuzi wa chuo hicho katika Jiji la Dodoma na Simiyu.

Jumla ya wahitimu 2,275 wametunukiwa tuzo zao katika kozi mbalimbali zikiwamo za usimamizi wa kodi, bima na majanga, benki na fedha, teknolojia na habari na zinginezo

WAKURUGENZI wawili wa Kampuni ya Tanzanite One Mining Ltd ya ...

foto
Mwandishi: Oscar Job

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi