loader
Picha

Waziri: Tushikamane kupambana na VVU

SERIKALI imeyataka madhehebu ya dini, taasisi za kiserikali na mashirika yasiyo ya kiserikali nchini, kushikamana pamoja katika mapambano dhidi ya vita ya Ukimwi ili kuhakikisha maambukizi mapya ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) nchini hayaongezeki.

Rai hiyo imetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu), Jenista Mhagama aliyemwakilisha Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kwenye maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani ambayo kitaifa yamefanyika jijini Mwanza, ambayo kaulimbiu ya maadhimisho hayo ni “Jamii ni chachu ya mabadiliko, tuungane kuzuia maambukizi mapya ya VVU.”

Jenista alisema juhudi hizo za pamoja, zitaiwezesha nchi na serikali kuwa na mikakati ya kupambana na maambukizi mapya ya VVU, ambayo kwa mujibu wa takwimu za kitaifa jumla ya watu milioni 1.6 kwa sasa wanaishi na VVU. Alifafanua kuwa kiwango cha maambukizi, kimeendelea kuongezeka kutoka asilimia 4.7 mwaka 2000 hadi asilimia 7 mwaka 2016.

Amesema juhudi ambazo zimekuwa zikifanywa na serikali dhidi ya mapambano ya VVU, zimesaidia kiwango cha maambukizi hayo kupungua kutoka maambukizi 120,000 mwaka 2000 hadi maambukizi 72,000 mwaka 2017.

“Kufuatia hatua hiyo, Waziri Mkuu anaiagiza Tume ya Kudhibiti Ukimwi nchini kuratibu afua zote za Ukimwi ili ziweze kuwafikia watanzania wote bila ya kubaguliwa ili waweze kupatiwa huduma stahiki,” amesema Jenista.

Alizitaka pia Kamati za Kudhibiti Ukimwi zilizo kwenye halmashauri nchini, kuhakikisha zinazingatia mahitaji ya jamii kwenye mapambano dhidi ya Ukimwi na kamwe zisishughulike wala kuzingatia mambo yake ya binafsi ya tume.

Kuhusu udhibiti wa maambukizi ya VVU kwenye vyuo vikuu, alisema serikali kwa kushirikiana na Wizara ya Afya na wadau wengine, itahakikisha inaanzisha kampeni maalumu ya kudhibiti VVU vyuoni kuanzia Februari mwakani.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alimpongeza Waziri Mkuu, Majaliwa kwa kukubali kuwa Balozi wa Kupambana na Ukimwi nchini.

Ummy alisema wizara yake imeendelea kupambana na maambukizi mapya ya VVU kwa wanaume, ambapo katika kipindi cha miaka 10 iliyopita (2009-2019) zaidi ya wanaume milioni 4 walifanyiwa tohara kama sehemu ya kudhibiti maambukizi mapya ya Virusi Vya Ukimwi.

“Hadi kufikia mwezi Septemba mwaka huu jumla ya wanaume 634,000 wamefanyiwa tohara,” alisema.

Aidha, katika kudhibiti UKIMWI kwa vijana, alisema serikali imeruhusu kisheria vijana wenye umri wa kuanzia miaka 15 hadi 18, kwenda kupima virusi vya Ukimwi bila kusubiri ridhaa ya wazazi au walezi wao na pia kuruhusu upimaji binafsi wa virusi vya Ukimwi kwa wananchi.

Alisema jumla ya watu 17,000 walijitokeza kupima VVU kwa njia binafsi na kuwasilisha majibu yao kwenye vituo vya kutolea huduma kwa mikoa 13 nchini iliyokuwa imefanyiwa majaribio.

“Katika kuendelea na mapambano ya UKIMWI, tumeongeza vituo vya kutolea huduma kutoka vituo 3,450 mwaka 2015 hadi vituo 6,529 kwa mwaka huu,” alisema.

WAKURUGENZI wawili wa Kampuni ya Tanzanite One Mining Ltd ya ...

foto
Mwandishi: Nashon Kennedy, Mwanza

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi