loader
Picha

Tanzania, Burundi, DRC kujenga SGR

SERIKALI za Tanzania, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), zimekubaliana kwa kauli moja kutekelezwa kwa mradi wa ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) kutoka Dar es Salaam kupitia Burundi hadi Mashariki mwa DRC.

Kauli hiyo ilitolewa juzi na mawaziri wa uchukuzi na mawasiliano wa nchi hizo tatu mjini Kigoma.

Ilitolewa wakati wa hafla ya kusaini mkataba wa awali wa makubaliano kati ya Serikali ya Tanzania na Burundi ya awamu ya kwanza ya ujenzi wa reli hiyo, kutoka Uvinza mkoani Kigoma hadi Gitega kupitia Msongati nchini Burundi.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano wa Tanzania, Isack Kamwelwe akizungumza baada ya kutiwa saini kwa makubaliano hayo, alisema wamefanyia marekebisho makubaliano hayo ya ujenzi wa reli hiyo, yaliyofanyika mwaka 2015 kutokana na mabadiliko mengi na makubwa ya ujenzi wa reli hiyo.

Kamwelwe alisema awamu ya kwanza ya ujenzi wa reli hiyo, itaanzia wilayani Uvinza mkoani Kigoma kwenda Msongati nchini Burundi na baadaye kupelekwa hadi mkoani Gitega, Burundi.

Baada ya kukamilika kwa kipande hicho, reli hiyo pia itaelekea mikoa ya Mashariki mwa DRC.

“Upembuzi wa kina na usanifu umeshafanywa na Mhandisi Mshauri kutoka Kampuni ya Gulf Engineering kutoka Uvinza mkoani Kigoma hadi Msongati na Gitega nchini Burundi ambao unatarajia kukamilika mwezi Januari mwakani, lakini nchi zote mbili (DRC na Burundi) zimeonesha nia ya dhati kuunga mkono ujenzi wa reli hiyo na kwa sasa kinachotafutwa ni pesa kwa ajili ya kuanza upembuzi na usanifu kuelekea DRC,” alisema Kamwelwe.

Kwa upande wake, Waziri wa Uchukuzi, Mitambo na Upangaji wa Ardhi wa Burundi, Jean Bosco Ntunzwenimana alisema wamevutiwa na kazi anayoifanya Rais John Magufuli katika ujenzi wa reli ya kisasa iendayo kasi (SGR), hivyo serikali ya Burundi imeona ifanye haraka ili reli hiyo ifike nchini mwao.

Ntunzwenimana alisema reli hiyo, ina maana kubwa kwao Burundi katika kuinua na kuimarisha shughuli za kiuchumi hasa usafirishaji wa shehena, kwani itapunguza gharama za usafirishaji wa shehena kutoka bandari ya Dar es Salaam na kupunguza muda wa usafirishaji wa shehena hiyo.

Mratibu wa Ukanda wa Kati wa Serikali ya DRC, Roger TE Biasu aliyemwakilisha Waziri wa Uchukuzi na Miundombinu wa nchi hiyo, alisema kwao DRC reli hiyo ni muhimu katika usafirishaji wa shehena na bidhaa za wafanyabiashara.

Alisema wana shida kubwa ya gharama kubwa ya usafirishaji shehena kwenda nchini mwao, hasa wale wa majimbo ya Congo ya Mashariki yanayopakana na Tanzania.

Alisema reli ya kisasa ya mwendo kasi, itakuwa mkombozi mkubwa wa uchumi wa wananchi wa Congo ya Mashariki, ambako hali ya miundombinu yake siyo mizuri na itakuwa chachu ya kuboresha hali ya maisha ya wananchi wa eneo hilo.

WAKURUGENZI wawili wa Kampuni ya Tanzanite One Mining Ltd ya ...

foto
Mwandishi: Fadhili Abdallah, Kigoma

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi