loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Watoto wachache chanzo saratani ya matiti

WAKATI imebainika kuwa saratani ya mlango wa kizazi, ndio inayoongoza kwa kuwa na wagonjwa wengi nchini, Jiji la Dar es Salaam limebainika kuongoza kwa saratani ya matiti, inayochangiwa na wanawake kuzaa watoto wachache chini ya wanne.

Hayo yamebainishwa jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI), Dk Julius Mwaiselage wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya taasisi hiyo ndani ya miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Tano.

Dk Mwaiselage amesema nchini Tanzania kwa sasa aina 10 za saratani, ndizo zinazoongoza ambazo ya kwanza ni saratani ya mlango wa kizazi, matiti, ya njia ya chakula kooni, ya ngozi aina ya Kaposi Sarcoma, saratani mchanganyiko, ya matezi, ya damu, tezi dume, kibofu cha mkojo na ya ngozi kwa albino.

Akizungumzia ongezeko la wagonjwa wa saratani nchini na aina zake, Dk Mwaiselage alifafanua kuwa ziko aina zaidi ya 200 za saratani duniani, lakini nchini Tanzania aina 10 ndizo zinazoongoza, kwa kuwa na wagonjwa na kwamba kila kanda nchini, ina aina ya saratani inayoongoza.

“Mfano, kwa Jiji la Dar es Salaam, saratani ya matiti ndiyo inaongoza kwa kuwa na wagonjwa wengi, hii inachangiwa na wanawake wengi kutozaa watoto wa kutosha, wengi wao wamezaa watoto mmoja au wawili, sasa hao ni wachache ila mama akizaa watoto kuanzia wanne, anapunguza vichocheo vya kupata saratani ya matiti,” ameshauri Dk Mwaiselage.

Alifafanua kuwa mama anapozaa watoto wa kutosha kuanzia wanne na kunyonyesha kwa muda unaokubalika wa miaka miwili huwa anapunguza vichocheo vya saratani ya matiti. Lakini, tatizo lililopo ni wanawake wengi jijini humo, kuzaa watoto wachache mmoja au wawili.

Mbali na kuzaa watoto wachache, Dk Mwaiselage alibainisha chanzo au kisababishi kingine cha saratani zote ni ulaji mbaya wa vyakula, usiozingatia lishe na ulaji wa mboga za majani na matunda.

Akitoa takwimu alisema kwa mwaka ORCI inaona wagonjwa wapya 7,600 na kati ya hao asilimia 14 ni wa saratani ya matiti.

Alishauri wananchi kufuata kanuni bora za lishe na kuzaa watoto wa kutosha na kuwanyonyesha kwa muda unaoshauriwa kitaalamu.

Akizungumzia saratani ya mlango wa kizazi, Dk Mwaiselage alisema Mkoa wa Mbeya ndiyo unaongoza, kwa kuwa na wagonjwa wengi wa saratani hiyo na inachangiwa na mtindo wa maisha wa eneo husika.

Hata hivyo, saratani ya mlango wa kizazi hutokana na maambukizi ya virusi vya ‘Human Papillomavirus’ au HPV vilivyoko katika jamii ya papilloma.

Baadhi ya virusi hivyo huambukizwa kwa njia ya kujamiana au ngono zembe. Kadhalika, alisema katika Kanda ya Ziwa, saratani ya kibofu cha mkojo ndiyo inawatesa zaidi kutokana na eneo hilo wakazi wake wengi kupatwa na maradhi ya kichocho.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma za Kinga ya Saratani katika ORCI, Dk Crispian Kahesa alisema wagonjwa wa saratani ya matiti wameongezeka.

Alisema sasa hata wanawake wenye umri kuanzia miaka 30, nao wanaweza kuwa na saratani hiyo wakati awali umri ulikuwa ni kuanzia miaka 55, lakini ikashuka hadi miaka 50.

Kwa upande wa wanaume, Dk Kahesa alisema saratani hiyo huathiri asilimia moja kwa wanaume. Hata hivyo, kwa upande huo ni hatari zaidi na isipogundulika haraka, huweza kuathiri mapafu kwa haraka. Wakati ORCI wakisema hayo, Shirika la Afya Duniani (WHO) linasema saratani ndio chanzo cha kifo cha mtu mmoja kati ya watu sita duniani.

Hata hivyo, asilimia 50 ya aina zote za saratani zinaweza kuzuilika, iwapo mgonjwa atawahi kupata tiba mapema wakati ugonjwa ukiwa hatua za awali.

Pamoja na kuzungumzia ongezeko la maradhi hayo, Dk Mwaiselage alisema ndani ya miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Tano, serikali imefanya mageuzi kwenye taasisi hiyo, kwa kuongeza fedha za ununuzi wa dawa na vifaa tiba, ambapo sasa upatikanaji wa dawa za saratani ni asilimia 95.

“Ugonjwa wa saratani ni miongoni mwa maradhi ambayo serikali inayagharamia bure, na dawa zake ni za ghali na kiwango cha fedha kwa ajili ya ununuzi wa dawa kimeongezeka kutoka shilingi milioni 790 mwaka 2015/16 hadi kufikia shilingi bilioni 10 kwa sasa,” alisema

BODI ya Michezo ya Kubahatisha nchini kwa kushirikiana na Mamlaka ...

foto
Mwandishi: Ikunda Erick

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi