loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Milioni 574/-kumaliza tatizo la maji Chamwino

SHILINGI milioni 574 ambazo zitatumika katika kujenga matangi na kusambaza maji zinalenga kumaliza tatizo la maji katika wilaya ya Chamwino pamoja na Ikulu, mkoani Dodoma.

Akizungumza mara baada ya kufanya ziara na kukagua mradi wa maji katika wilaya hiyo unaotekelezwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira (Duwasa), Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa alisema tayari serikali imeshatoa Sh milioni 290 kwa ajili ya kuanza utekelezaji huo.

Hadi Januari mwakani Duwasa itakuwa tayari imeshaanza kujenga tangi la lita milioni 2.2 kwa lengo la kusambaza maji katika maeneo mbalimbali, ikiwemo Ikulu pamoja na Hospitali ya Uhuru inayojengwa wilayani humo.

Pia mkakati huo wa kusambaza maji utahusisha ujenzi wa tangi lingine kubwa katika kijiji cha Msangi la mita za ujazo 400,000 ili kusambaza maji Msangi na kijiji kingine jirani. Profesa Mbarawa alisema kuanzia wiki ijayo, serikali itapeleka Sh milioni 200 kwa ajili ya kuanza kazi ya kujenga tangi kubwa la ujazo wa lita milioni 2.2 katika eneo Buigiri ili kuanza mchakato wa kusambaza maji katika maeneo hayo.

Alisema mradi huo pia utahisisha uchimbaji visima unaofanywa na Wakala wa Uchimbaji Visima na Ujenzi wa mabwawa sita (DDCA) ili kuongeza idadi ya visima vitatu vilivyopo na kukusanya maji hayo hadi kwenye tangi hilo kubwa.

Alisema kazi hizo za uchimbaji visima na usambazaji maji zinaweza kufanywa na wenyewe badala ya kutegemea makandarasi ambao wamekuwa wakitaka fedha nyingi na kuchelewesha kukamilisha miradi hiyo.

Alisema katika mradi huo ambao unatekelezwa kwa Sh milioni 574 katika muda mfupi, ungechukuliwa na wakandarasi ungeweza kutumia miezi sita na kwa gharama kubwa ya Sh bilioni 1.5.

Akizungumza Meneja Ufundi wa Duwasa, Kashilimu Mayunga alisema wao wamejipanga kuhakikisha Chamwino ambayo Ikulu ipo ndani inapata maji kwa kushirikiana na DDCA kwa ajili ya kuchimba visima sita vingine.

Kuhusu kukosa maji kwa miaka 10 sababu ya kukosa umeme, Mwenyekiti wa Kijiji cha Isanga, Kata ya Isanga, Khatibu Ramadhani alimshukuru Waziri Mbarawa kwa kufika kukagua tangi lililodumu miaka 10 bila kutumika katika kijiji hicho kwa kukosa umeme akadai wanaamini safari hii watapata maji kama Tanesco watafikisha umeme.

Profesa Mbarawa alimwagiza Mkuu wa Wilaya ya Chamwino, Vumilia Nyamoga na Watalamu wa Duwasa kufuatilia Tanesco kwanini wahafikishi umeme katika mitambo yenye pampu ya kusukuma maji kwa ajili ya wananchi wa kijiji hicho.

foto
Mwandishi: Magnus Mahenge, Chamwino

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi