loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Papaa Msofe kortini kwa kutakatisha milioni 900/-

MFANYABIASHARA maarufu Marijan Msofe maarufu ‘Papaa Msofe’ na wenzake wanne wamefi kishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam wakikabiliwa na mashitaka matano ikiwamo utakatishaji wa fedha wa zaidi ya Sh milioni 900.

Papaa Msofe ambaye aliwahi kufikishwa mahakamani hapo 2012 akikabiliwa na mashitaka ya mauaji na mwaka 2015 kesi ya kughushi, alifikishwa mahakamani hapo jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba.

Mbali na Msofe, washitakiwa wengine ni Wakili wa Kujitegemea, Mwesigwa Muhingo, Fadhil Mganga, Wencelaus Mtui na Joseph Haule. Wakili Mwandamizi wa Serikali, Ladslaus Komanya alidai kuwa washitakiwa wametenda makosa yao kwa nyakati tofauti tofauti.

Katika kosa la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu inadaiwa walilitenda kati ya Desemba 2018 na Septemba 2019 katika Jiji la Dar es Salaam ambako wakiwa na nia hiyo walijipatia Dola za Marekani 300,000 (sawa na Sh milioni 660) kutoka kwa Pascal Camille wakidai ni fedha za kuumuzia madini ya dhahabu kilogramu 200 ambayo wangemsafirishia kwenda Ureno wakati wakijua si kweli.

Pia inadaiwa walitenda kosa hilo kati ya tarehe hizo hizo ambapo walimlaghai Johnson Mason kwamba watamuuzia kilo 20 za madini ya dhahabu yenye thamani ya Sh milioni 253 kwenda Ureno wakati wakijua si kweli.

Katika kosa la utakatishaji fedha inadaiwa walilitenda kati ya Desemba 2018 na Septemba 2019 katika maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam ambako walijipatia Dola za Marekani 300,000 (Sh milioni 660) na Dola 110,000 (sawa na Sh milioni 253) ambazo ni zaidi ya Sh milioni 900 huku wakijua fedha hizo ni zao la udanganyifu.

Washitakiwa hao hawakutakiwa kujibu chochote kwa sababu kesi hiyo ni ya Uhujumu Uchumi, hivyo haina dhamana ambako shauri hilo limeahirishwa hadi Desemba 16, mwaka huu.

foto
Mwandishi: Francisca Emmanuel

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi