loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

TARI ilivyojipanga kuona uagizaji mafuta ya kula nje unakoma

TAKWIMU zilizopo zinaonesha kwamba Tanzania hutumia tani 570 za mafuta ya kula kwa mwaka lakini kiasi kinachozalishwa ni tani 205,000 tu, hivyo kuwa na upungufu wa tani 365,000 za mafuta.

Kiasi hicho kinapoagizwa nje huigharimu nchi dola za Marekani 193,712,000 (takribani Sh bilioni 443) kwa mwaka na hii maana yake ni kwamba, mbali ya fedha hizo za kigeni kufanya mambo mengine hutumika kuajiri watu wa nje badala ya Watanzania! Ni katika muktadha huo, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, aliiagiza Taasisi ya Utafiti wa Kilimo nchini (TARI) kuhakikisha kunakuwa na ongezeko la uzalishaji wa mazao ya mafuta ya kula, hususani mchikichi.

Chikichi ambayo ni miongoni mwa mazao ya kimkakati limechaguliwa kutokana na ukweli kwamba ni zao linaloongoza kwa kutoa kiwango kikubwa cha mafuta ya kula ikilinganishwa na mengine kama vile alizeti, karanga, pamba, nazi, ufuta na kadhalika. Na ikumbukwe kwamba hata asilimia kubwa ya mafuta yanayoagizwa kutoka nje yanatokana na chikichi.

Mkurugenzi Mkuu wa TARI, Dk Geoffrey Mkamilo, anasema taasisi hiyo inatekeleza agizo la Waziri Mkuu kwa kuanza kuzalisha miche mipya na ya kisasa na inayotoa mazao mengi zaidi hasa kwa kuzingatia kwamba iliyopo mingi imezeeka, ikiwa na miaka zaidi ya 50. Dk Mkamilo anayasema hayo wakati wa ziara yake aliyoifanya mkoani Kigoma kufuatilia uzalishaji wa zao hilo katika maeneo mbalimbali kuangalia umefikia hatua gani.

Anasema baada ya agizo la Waziri Mkuu, TARI ilianzisha kituo cha Kihinga ambacho kinajishughulisha na uchunguzi pamoja na uzalishaji wa mbegu za chikichi na kuzisambaza kwa taasisi za umma na binafsi. Anasema TARI inazalisha mbegu hizo za kisasa kwa wingi ikishirikiana na baadhi ya kampuni binafsi ili kuondoa changamoto hiyo kwa taifa.

Kwa mujibu wa Dk Mkamilo, mkoa wa Kigoma kwa sasa una eneo la hekta 21,000 kwa ajili ya kulima zao hilo, lakini kutokana na tija ndogo ya uzalishaji wa chikichi iliyokuwa inapatikana wengi walikuwa wameanza kukitega mgongo kilimo hicho. Inaelezwa kwamba kwa kutegemea michikichi ya kizamani iliyozeeka, miti 125 inaweza kutoa tani 1.6 za mafuta wakati katika nchi ya Malaysia wanaofanya kilimo cha kisasa kama kinachosimamiwa na TARI sasa, idadi hiyo ya miti hutoa tani nane hadi tisa.

Dk Mkamilo anasema Taasisi ya TARI Kihinga imeshazalisha mbegu ambazo imezigawa katika halmashauri sita za mkoa wa Kigoma za Uvinza, Buligwe, Kasulu Mji, Wilaya ya Kasulu, Manispaa ya Kigoma Ujiji na Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma. Lakini pia TARI ina mpango wa kuliendeleza zao hilo katika mikoa mingine nchini ambako imeonekana chikichi inastawi vyema kama vile Wilaya za Kyela (Mbeya), Mkuranga na Bagamoyo (Pwani), Tanga pamoja na Zanzibar.

“Ipo mikoa ambayo ina fursa ya kulima zao la chikichi mbali na Kigoma. Sasa tumepanga kuongeza nguvu katika kuhamasisha wakulima katika mikoa hiyo kulima chikichi na kuwapelekea mbegu za kisasa na zenye tija,” anasema.

Dk Mkamilo anaamini kwamba Tanzania ina uwezo wa kuongeza uzalishaji wa mafuta na ziada na hivyo kuuza katika nchi jirani ikiwemo Kenya ambayo inaagiza takribani asilimia 80 ya mafuta yake ya kula kutoka nje. Nchi nyingine zinazoagiza kwa wingi mafuta ya kula nje ni Rwanda, Congo na Sudan.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa TARI kituo cha Kihinga kilichopo Kigoma, Dk Filson Kagimbo, anasema mkakati wao ndani ya miaka mitatu ni kusambaza miche milioni 15 sawa na wastani wa miche milioni tano kwa kila mwaka. Anasema moja ya kazi inayofanywa na kituo cha TARI Kihinga ni utafiti wa zao hilo kwa kuwa kilimo hicho nchini kina changamoto mbalimbali ikiwemo upungufu wa mbegu za kisasa aina ya Tenera. “Wakulima zaidi ya asilimia 90 wanalima mbegu ya kienyeji inayoitwa dura ambayo inatoa mafuta kidogo kulinganisha na tenera.

“Mbegu za tenera upatikanaji wake ni kama asilimia 10 na za kienyeji ni asilimia 90 hivyo kituo kimeweka kipaumbele cha kuzalisha mbegu nyingi za kisasa ili zisambazwe kwa wakulima waachane na mbegu zisizo na tija,” anasema.

Anasema kimsingi, mchikichi unapaswa kukaa takribani miaka 30 tu lakini iliyopo ina miaka 50 hadi 100 na hivyo kuwa na changamoto ya uzalishaji duni sana. Mshauri wa Kilimo, Sekretarieti ya Mkoa wa Kigoma, Joseph Lubuye anasema halmashauri zote zinazostawi michikichi katika mkoa huo, zimeitika mwito huo wa Waziri Mkuu wa kuzalisha na kutumia mbegu za kisasa.

Ni kwa mantiki hiyo, TARI Kihinga imewaongezea nguvu kwa kuwapa mbegu za kisasa inazozalisha, hali iliyowafanya waokoe fedha ambazo wangenunulia miche hiyo kutoka nje ya nchi na hivyo fedha hizo zinatumika kutunzia vitalu vya miche wanazopewa. Wawekezaji mbalimbali wa viwanda vya kuzalisha mawese wamejitokeza kwa kuandika barua ya kuanza kununua malighafi ya zao hilo, akiwemo mwekezaji kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Uvinza, Kachengwa Masumbuko anayabainisha hayo katika ziara hiyo ya Dk Mkamilo mkoani humo ambayo mwandishi wa makala haya alikuwepo pia. Masumbuko anasema kupatikana kwa mwekezaji huyo kutaongeza tija kwa wakulima wa zao hilo kwa kuwa watakuwa na sehemu ya kupeleka mazao yao baada ya kuvuna.

Sambamba na hilo, Mkurugenzi huyo anasema halmashauri yake imezitaka shule za msingi na sekondari kuanza kuwafundisha wanafunzi jinsi ya kupanda zao la michikichi ili kuwajengea uwezo, kulipenda na kulithamini zao hilo. Anasema halmashauri pia inaandaa sheria ndogo ambazo zitawabana na kuwahimiza wakulima kuweka msisitizo katika kilimo cha kisasa cha zao hilo.

Naye Kaimu Mkuu wa Kikosi cha 821, JKT Bulombora, Kapteni Benitho Lubida, anasema kwa kushirikiana na TARI wameandaa miche aina ya Tenera 100,000 itakayopandwa kwenye shamba la ekari 2000. Tayari miche 19,600 imeshapandwa wakati wakiendelea na maandalizi ya miche mingine iliyobaki, lakini pia anasema wameshatayarisha shamba lenye ukubwa wa ekari 916 tayari kwa kupanda michikichi.

“Sisi kama JKT tumepewa jukumu na Waziri Mkuu na tayari tumeanza utekelezaji wake kwa kasi sana na tumeshatayarisha shamba letu na kuandaa miche na kazi bado inaendelea,” anasema.

Anasema kwa kushirikiana na TARI wanaandaa miche aina ya tenera 500,000 kwa ajili ya kuhudumia halmashauri sita pamoja na vijiji mbalimbali vinavyozunguka eneo la jeshi hilo. Mkuu wa Gereza la Kwitanga, Dominic Kazimile, anasema lengo la Serikali ni kuhakikisha gereza hilo linakuwa ni kituo kwa ajili ya kuzalisha mbegu bora za chikichi aina ya tenera. Anasema gereza hilo limepanga kupanda mbegu mpya za chikichi katika eneo la ekari 6,000 na tayari limeshaanda ekari 400 katika mpango wake wa awamu ya kwanza.

Anasema kwa sasa shamba linaotesha mbegu bora 10,795 pamoja na kuondoa michikichi ya zamani iliyopandwa tangu mwaka 1968. Naye Mkuu wa Gereza la Ilagala lililopo wilayani Uvinza, Mangole Mbaruk, anasema wamepokea mbegu 10,000 kutoka TARI na wameandaa ekari 200 kwa ajili ya kuzipanda. Kwa upande wake, Mkulima Safina Fredrick, Mkazi wa Mwamila wilayani Uvinza, anasema mbegu mpya za michikichi ni nzuri kwa kuwa zinakua kwa muda mfupi tofauti na zile za zamani.

Anaamini kwamba ndani ya miaka mitatu ya ulimaji wa mbegu hizo mpya mkulima ataanza kuona matokeo chanya. Katibu Tawala wa mkoa wa Kigoma, Rashid Mchatta ametaka kupatiwa taarifa za zao hilo kila mwezi kutoka kwa wasaidizi wake ili kama kuna changamoto yoyote zieleweke na kupatiwa ufumbuzi. Mchatta anakiri kuwa kuna wilaya zimefanya vizuri katika kuitikia agizo hilo la Waziri Mkuu na nyingine hazijafanya vizuri ila atazifuatilia.

“Tutawafuatilia wakurugenzi kwenye bajeti ili watenge bajeti ya michikichi na kutuletea taarifa,” anasisitiza.

Mwakilishi wa baadhi ya wafanyakazi wanaoandaa mafuta hayo ya mawese, Ally Athuman anasema shughuli hiyo ya uandaaji wa mafuta inawapatia fedha kidogo tofauti na kazi kubwa wanayoifanya.

Malalamiko makubwa yapo kwenye madumu wanayoyatumia ambayo yana lita 30, yakiwa na mafuta huuzwa kati ya Sh 22,000 hadi 28,000 kiasi ambacho anasema ni kidogo. “Hii inatuumiza sana wakati kazi ni ngumu kwani tunakata mikungu hiyo, tunasomba pamoja na kuisaga ili mafuta yapatikane,” anasema.

HUDUMA bora za afya ya msingi zinapunguza uhitaji, gharama na ...

foto
Mwandishi: Lucy Ngowi

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi