loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Mapato haya TRA yawe chachu ya kulipa kodi zaidi

HIVI karibuni, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ilieleza mafanikio yaliyopatikana ndani ya mamlaka hiyo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Dk John Magufuli.

Katika mkutano na waandishi wa habari, Naibu Kamishna Mkuu wa TRA, Msafiri Mbibo, alisema TRA pamoja na mambo mengine, imefanikiwa kuongeza mapato ya serikali kwa miaka minne mfululizo.

Anasema mwaka 2015/16 mapato yalikuwa Sh trilioni 12.5, mwaka 2016/17 mapato yaliongezeka hadi kufikia Sh trilioni 14.4, mwaka 2017/18 mapato yaliongezeka pia hadi kufikia Sh trilioni 15.5 na mwaka 2018/19 makusanyo yaliongezeka zaidi kufikia Sh trilioni 15.9.

Hivyo, jumla ya mapato yote kwa miaka minne ni Sh trilioni 58.3 ikilinganishwa na Sh trilioni 34.97 zilizokusanywa kwa kipindi cha miaka minne ya mwisho kabla Rais Magufuli hajaingia madarakani. Kwa hesabu rahisi, hii inamaanisha kuwa, kuna ongezeko la Sh trilioni 23.33 katika miaka minne ya serikali ya awamu ya tano.

Kwa upande wa makusanyo ya kila mwezi, katika kipindi cha miaka hii minne, TRA imekuwa ikikusanya wastani wa Sh trilioni 1.3 ikilinganishwa na wastani wa Sh bilioni 850 kabla awamu hii ya tano.

Sambamba na ongezeko hilo, kuanzia Julai hadi Oktoba 2019/20 wastani wa makusanyo umepanda hadi kufikia Sh trilioni 1.45 kwa mwezi. Hatubezi kiasi kilichokusanywa kabla ya uongozi wa Rais Magufuli isipokuwa tunataka kuonesha jinsi wananchi walivyoelewa umuhimu wa kulipa kodi kwa maendeleo yao na nchi yetu kwa ujumla.

Naibu Kamishna Mkuu Mbibo anafafanua sababu za kuongezeka kwa mapato hayo ni msukumo wa serikali ya awamu ya tano wa kuendelea kuboresha mikakati ya kuimarisha ukusanyaji wa mapato, kuibua vyanzo vipya vya kodi pamoja na utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Tano wa TRA wa ukusanyaji kodi wenye dhamira ya kuongeza makusanyo ya kodi za ndani kwa kukuza ridhaa ya ulipaji kodi wa hiari.

“Pamoja na msukumo huo, tunapata pia ushirikiano kutoka kwa wadau wengine, ikiwemo vyombo vya ulinzi na usalama, asasi zisizokuwa za kiserikali, wizara, taasisi, wakala na idara za serikali pamoja na mawakala wa forodha,” anasema Mbibo.

Anabainisha sababu nyingine iliyochangia kuongezeka kwa mapato hayo kuwa ni kuimarika kwa matumizi ya mashine za kielektroniki za kutolea risiti (EFD) badala ya stakabadhi zinazoandikwa kwa mkono.

Ongezeko la mizigo kutoka nje ya nchi kupitia bandari zetu za Dar es Salaam na udhibiti wa makusanyo ya bidhaa zinazopaswa kulipiwa kodi na ushuru ziendazo nje ya nchi kwa mfano korosho ghafi na mazao ya ngozi na kwato ilibainishwa kuwa ni sehemu ya sababu ya kuongezeka kwa makusanyo hayo. Vilevile, wananchi wamejionea kwa macho yao wenyewe jinsi kodi wanazolipa zinavyotumika vizuri katika kutoa huduma kwa jamii, kuleta maendeleo kwa taifa na hivyo kutambua na kupenda kulipa kodi kwa hiari.

“Napenda kuchukua fursa hii kuwapongeza na kuwashukuru watanzania na walipakodi wote kwa ujumla kwa kulipa kodi zao kwa hiari na kuitikia mwito wa serikali wa kutumia mashine za EFD bila kusahau wananchi ambao wamekuwa wakidai risiti kila wanaponunua bidhaa na huduma mbalimbali,” anasema Mbibo.

Anasema mwitikio huu unaonesha kukua kwa uelewa wa wafanyabiashara na watanzania kuhusu wajibu wao wa kulipa kodi. TRA pia inawapongeza viongozi katika ngazi zote za serikali, kuanzia Rais Magufuli, Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, mawaziri, wakuu wa mikoa, wilaya na hata viongozi wengine kuanzia ngazi za kata, vitongoji, mitaa na vijiji katika kufanikisha ukusanyaji wa mapato hayo.

“Tunapenda pia kwa namna mahususi kutambua miongozo ya Wizara ya Fedha na Mipango ambayo ndio wizara mama inayoisimamia mamlaka. Tunawashukuru sana Dk Philip Mpango, Waziri wa Fedha na Mipango, Naibu Waziri Dk Ashatu Kijaji, Katibu Mkuu Ndugu Dotto James pamoja na timu nzima ya wizara,” anabainisha Mbibo.

Anaongeza: “Kwa upande wa Bunge na mihimili mingine, tumekuwa tukipata msaada mkubwa sana. Pale panapokuwa na vikwazo vya kisheria, Bunge na mahakama imekuwa ikitusaidia kuondoa vikwazo ama ugumu wa aina yoyote hususani tafsiri sahihi za sheria ili tuweze kutimiza wajibu wetu wa kukusanya mapato.” Tunapozungumzia kuongezeka kwa mapato, hatuwezi kuacha kuonesha uanzishwaji wa mifumo ambayo imerahisisha ukusanyaji wa mapato hayo.

Kati ya mifumo iliyoanzishwa na TRA ni Mfumo wa Stempu za Kodi za Kielektroniki ulioanza mwezi Juni mwaka 2018 na kuanza kutumika rasmi Januari 15 mwaka huu. Mfumo huo ni mbadala wa stempu za karatasi za kubandika ambazo zilikuwa zikitumika hapo awali.

Lengo la kuanzisha mfumo huo mpya ni pamoja na kuongeza mapato ya serikali yanayotokana na ushuru wa bidhaa, Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT), Kodi ya Mapato pamoja na kuondoa malalamiko kutoka kwa wafanyabiashara ya kutokutendewa haki ya makadirio ya kodi zinazosimamiwa na TRA. Kutokana na utekelezaji wa mfumo huo, kwenye eneo la pombe kali na mvinyo tu, TRA imekusanya ushuru wa bidhaa Sh bilioni 77.8 kwa kipindi cha mwezi Februari hadi Oktoba, 2019 ukilinganisha na kiasi cha Sh bilioni 58.2 kilichokusanywa kipindi kama hicho mwaka jana.

Kwa upande wa bidhaa za vinywaji laini, yaani soda na vinywaji vingine visivyo vya kilevi ambapo matumizi ya mfumo huo yalianza Agosti, 2019, kwa mwezi Septemba na Oktoba mwaka huu, TRA ilifanikiwa kukusanya Sh bilioni 10 ukilinganisha na Sh bilioni 9.2 zilizokusanywa kipindi kama hicho mwaka uliopita. Suala lingine ambalo ni muhimu pia katika mapato yaliyotangazwa na TRA ni msamaha maalumu wa riba na adhabu kwenye malimbikizo ya madeni ya kodi uliotolewa kwa asilimia 100 tofauti na asilimia 50 iliyokuwepo awali.

Msamaha huo maalumu ulitangazwa mnamo tarehe 11 Julai, 2018 kwa lengo la kutoa unafuu kwa walipakodi wenye malimbikizo ya madeni ya riba na adhabu kwa kuwapa fursa ya kulipa kodi ya msingi mara moja au kwa awamu ndani ya mwaka wa fedha wa 2018/19. Jumla ya walipakodi 9,406 waliomba msamaha na waliokidhi vigezo na kukubaliwa ni walipakodi 8,687.

Kwa idadi hii, jumla ya Sh bilioni 328.4 za riba na adhabu zilisamehewa wakati jumla ya Sh bilioni 458.58 zinaendelea kukusanywa kama kodi ya msingi. Mpaka sasa, Mamlaka ya Mapato Tanzania imeshakusanya Sh bilioni 120.01 kutokana na kodi ya msingi inayotakiwa kulipwa na walipakodi waliosamehewa riba na adhabu. Hata hivyo, serikali iliongeza muda wa kulipa kodi hiyo kutoka muda uliowekwa awali wa Juni 30, 2019 kuwa Desemba 31, 2019.

Hii ni habari njema kwa wale wote waliosamehewa riba na adhabu ili waweze kukamilisha kulipa kodi ya msingi kwa mujibu wa makubaliano yao na TRA wakati wanaomba msamaha huo maalumu. Shime walipakodi na Watanzania wote, mapato haya yaliyokusanywa na TRA yawe chachu ya kuendelea kulipa kodi kwa hiari na kwa wakati ili kuunga mkono dhamira ya Rais Magufuli ya kuifikisha Tanzania kwenye uchumi wa kati na wa viwanda ifikapo mwaka 2025.

Nasema iwe chachu ya kulipa kodi kwa hiari kwa sababu, kila mwananchi anaona jinsi serikali ya awamu ya tano inavyotumia kodi katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo hapa nchini. Kwa mfano, kupitia mapato hayo, serikali imeweza kutekeleza miradi mingi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa hospitali na vituo vya afya, ujenzi wa barabara za lami na za kawaida, reli, elimu bure, ununuzi wa ndege, ujenzi wa viwanja vya ndege, madaraja ya juu na chini pamoja na uanzishwaji wa miradi mikubwa ya umeme.

Ni kutokana na utekelezaji huo, TRA imejipanga kuendelea kutoa elimu ya kodi kwa wafanyabiashara na wananchi wote kwa ujumla kwa ajili ya kukuza ridhaa ya kulipa kodi kwa hiari ikiwa ni pamoja na kutoa huduma bora kwa wateja wake na hatimaye kuongeza mapato ya serikali. Kulwa Karedia ambaye ni mwandishi wa habari, alikiri wazi kuwa, TRA inafanya mapinduzi makubwa siyo tu kwenye suala la ukusanyaji mapato na utoaji elimu ya kodi bali hata katika eneo la utoaji huduma bora kwa wateja wake.

“Nakumbuka mara ya mwisho nilikwenda ku-renew leseni nilikaa wiki tatu lakini wiki iliyopita nilikwenda kama leo saa 4:00 asubuhi na kesho yake saa 5:00 asubuhi nikapata ujumbe kwenye simu yangu ya mkononi kwamba leseni yako iko tayari. Haya ni mapinduzi makubwa ambayo yanafanyika TRA, kwa kweli nawapongeza sana,” alisema Karedia.

Nahitimisha makala yangu kwa kusema kuwa, kila mwananchi aone fahari kulipa kodi ili tuweze kujitegemea. Ikumbukwe kwamba, nchi nyingi zilizoendelea na zinazoendelea duniani hivi sasa, hutegemea kodi. Tanzania ni kati ya nchi zinazoendelea hivyo tulipe kodi kwa ajili ya maendeleo ya kila Mtanzania.

HUDUMA bora za afya ya msingi zinapunguza uhitaji, gharama na ...

foto
Mwandishi: Veronica Kazimoto

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi