loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Wasindikaji alizeti waomba tozo zipunguzwe

WASINDIKAJI wa viwanda vya kuzalisha mafuta ya alizeti wameomba serikali kuzifanyia marekebisho tozo za Ongezeko la Thamani (VAT) kwenye eneo hilo ili kuongeza tija.

Wametoa ombi hilo kutokana na tozo hiyo kuonekana kikwazo cha ustawi wa viwanda na kutoa fursa viwanda vya nje kuchukua nafasi.

Wakizungumza mbele ya Naibu Waziri wa Kilimo, Omary Mgumba kwenye ziara ya kikazi kukagua miradi ya kilimo mkoani Singida, wadau hao wameiomba serikali kuondoa tozo kwenye mnyororo mzima wa uzalishaji wa mafuta hayo.

Wametaka itoe ruzuku ya ununuzi wa mbegu bora za alizeti na viuatilifu kwa wakulima kuongeza tija na bidhaa kukidhi mahitaji.

Meneja Utumishi na Uhusiano wa Kiwanda cha Mount Meru, Nelson Mwakabuta alisema,

“alizeti ni chache, wakati wa mavuno tunajikuta hatupo peke yetu, tuna ushindani kupata hiyo alizeti, sisi mashine zetu tumeziminya mpaka kwa siku tukiwa na alizeti nyingi tunaweza kuzalisha tani 300 wakati uwezo wa mashine zetu ni kuzalisha mpaka tani 750 kwa siku”.

Mwakabuta aliiomba serikali kuwapa wakulima ruzuku ya mbegu na kuongeza wazalishaji wa mbegu ya alizeti ili kuwezesha ipatikane kwa wingi na kwa kuzingatia ubora stahiki kulingana na matakwa ya soko la ndani na nje.

Alisema mbegu za kienyeji hutoa uzito mkubwa lakini mafuta ni kidogo ukilinganisha na zile za kisasa.

Alisema anaomba serikali ilegeze masharti ya kuingiza mbegu za kigeni nchini ikiwezekana zije kwa wingi, tofauti na mchakato wa sasa ambao hadi kukamilisha taratibu za uingizaji na kuingia sokoni huchukua miaka mitanohadi sita.

Mkurugenzi wa Kiwanda cha Mafuta ya Alizeti cha Singida Fresh Oil Mill, Khalid Ally Omary aliiomba serikali kuondoa tozo mnyororo wa uzalishaji wa mafuta hayo kwa wasindikaji wa ndani kuleta ushindani wa kibiashara kwa waingizaji wa nje na kukidhi hitaji la soko.

Alisema wana kiwanda cha kati kinachozalisha tani 720 kwa mwezi na kutoa ajira 167 lakini wana tozo kubwa ya VAT kwenye uzalishaji wa bidhaa hiyo na kufanya bei ya mafuta kupanda na kushindwa kuhimili ushindani wa mafuta yanaoingizwa kutoka nje yanayouzwa nafuu.

Tatizo lingine la sekta hiyo ni msururu wa kodi eneo la vipimo na uhakiki wa bidhaa ambayo hutozwa hadi Sh 100,000 eneo moja. Mathalani, Kodi ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi inatozwa na taasisi mbili, Osha na Manispaa.

Akijibu, Naibu Waziri Mgumba amesema kero nyingi zilizowasilishwa ni mtambuka ambazo zinagusa zaidi ya wizara moja, hivyo atakaa na viongozi wenzake kuangalia namna nzuri ya kurekebisha ili kuongeza tija kwenye sekta hiyo.

Akizungumzia uhaba wa mbegu, amesema serikali imewawezesha ASA kuzalisha mbegu kukidhi mahitaji, zenye ubora kulingana na mahitaji.

Aliwashauri wasindikaji kukopesha wakulima mbegu na kisha kulipana baada ya mavuno.

Mgumba alisema mwarobaini kukabiliana na ushindani wa mafuta yanayoingizwa nchini ni wasindikaji kuzalisha kwa wingi bidhaa hiyo.

KATIKA miezi sita ya mwanzo ya mwaka huu Kituo cha ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu, Singida

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi