loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Kaseja atemwa Kilimanjaro Stars

KIPA mkongwe nchini Juma Kaseja ametemwa kwenye kikosi cha timu ya soka ya Tanzania Bara ‘Kilimanjaro Stars’ kilichosafi ri kuelekea Uganda kwa ajili ya michuano ya Chalenji kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati.

Michuano hiyo inayoandaliwa na Baraza la Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) inatarajiwa kutimua vumbi kuanzia kesho katika jiji la Kampala, Uganda. Kaseja alikuwa kipa chaguo la kwanza la kocha Etienne Ndayiragije kwenye kikosi cha Taifa Stars kwenye mchezo wa mchujo kuingia hatua ya makundi ya kufuzu fainali za kombe la Dunia.

Lakini pia alitumika kwenye michezo ya kufuzu kwa Fainali za Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN) na pia kwenye michezo ya kufuzu kwa Fainali za Mataifa ya Afrika (CAN).

Hata hivyo, Kocha wa Stars, Juma Mgunda hakumjumuisha mlinda mlango huyo mkongwe kwenye orodha yake ya mwisho ya timu itakayoshiriki mashindano ya Kombe la Chalenji yatakayofanyika Uganda huku makipa Aisha Manula, Metacha Mnata wa Yanga na David Kisu wa Gor Mahia ya Kenya wakiitwa badala yake.

Orodha ya kikosi cha wachezaji 22 kama kilivyotangazwa na kocha Juma Mgunda kinajumuisha makipa Aisha Manula (Simba) Metacha Mnata (Yanga) na David Kisu (Gor Mahia) Wengine ni Juma Abdul, Nikson Kibabage, Gadiel Michael, Mwaita Gereza, Mohamed Hussein, Bakari Mwamnyeto, Kelvin Yondani na Bakari Majogoro.

Wengine ni Jonas Mkude, Zawadi Mauya, Mzamiru Yassin, Hassan Dilunga, Ditram Nchimbi, Mkandala Cleofas, Paul Nonga, Miraji Athumani, Eliuter Mpepo, Kikoti Lucas na Rashid Chambo.

Mbali na Kaseja, wengine waliotemwa ni Salum Kimenya, Abdulmajid Mangalo, Fred Tangalu, Idd Selemani (majeruhi), Jafar Kibaya, Salum Abubakari, Eliud Ambokile (hakuja), Yusuf Mhilu na Shaban Chilunda (majeruhi).

Kilimanjaro Stars kinatarajiwa kucheza mchezo wake wa kwanza dhidi ya Kenya kesho kutwa. Kocha Mgunda alisema wamejiandaa kushindana ili kupata matokeo mazuri. “Tumejiandaa kushindana Chalenji na lengo letu ni kuhakikisha tunapata matokeo mazuri kwa kila mchezo ulioko mbele yetu,”alisema.

KLABU ya Yanga imetangaza kumsajili winga wa kimataifa wa Tanzania ...

foto
Mwandishi: Grace Mkojera

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi