loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Ndalichako ahimiza wazazi kuruhusu matumizi ya teknolojia kwa watoto

WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako amewataka wazazi wasiwabane watoto katika ulimwengu wa teknolojia wakati wa makuzi yao.

Alisema hayo akizungumza wakati wa Kongamano la Saba la Watafiti wa Afya na Wadau wa Elimu lenye kaulimbiu ‘Elimu ya awali ya makuzi kwa maendeleo ya mtoto,’ lililofanyika Chuo Kikuu cha Aga Khan (AKU) jijini Dar es Salaam juzi.

Profesa Ndalichako alisema maisha mtoto anayopitia kipindi cha miaka mitano ya mwanzo yanachangia uwezo wake kiakili, kimtazamo, kuhusu elimu na maisha yake ya baadaye na kuwataka wazazi kwenda na kasi ya teknolojia itakayomwezesha mtoto kuchangamsha akili.

Profesa Ndalichako alisema uwezo wa mtoto unachangiwa na mambo mengi kama vile lishe, mazingira salama, afya na hali ya kuchangamshwa kiakili, na kusema kutokana na hilo elimu ya awali ni ufunguo wa muhimu katika maisha ya baadaye ya mtoto.

“Teknolojia ni sehemu ya maisha yetu, karibu nyanja zote za maisha zimenufaika kwa namna moja au nyingine na teknolojia, kwa mfano, ukigusa sekta ya mawasiliano utaona wazi mchango wa teknolojia, hivyo hivyo, katika usafiri, afya, elimu, kilimo, ufugaji na ujenzi. Kwa jumla, teknolojia imerahisisha maisha yetu,” alisema.

Alisema fursa kubwa inayoletwa na teknolojia ni neema kwa watoto kama itaweza kutumika vyema hasa katika sekta ya elimu na malezi.

“Usimnyime mtoto simu, lakini inabidi udhibiti mifumo mibaya na jitahidi kumuwekea mifumo mizuri ya kumjenga, sasa hivi kuna programu nyingi za watato kulingana na umri wao,” alisema Waziri wa Elimu.

Akitolea mfano baadhi ya kazi maarufu za watoto zilizopo katika mfumo wa kidijiti ni vibonzo jongevu (katuni-hai). Hizi ni filamu fupifupi zenye maudhui mbalimbali yenye malengo ya kufundisha na kutoa burudani kwa watoto.

Huko nyuma, filamu hizi zilionekana kama burudani tu, lakini siku hizi, vibonzo jongevu vinatumika sana katika lugha ya taaluma. Alisema kupitia filamu hizo, watoto wanapata maarifa muhimu kama vile Hisabati, Sayansi, Lugha hasa za kigeni kama Kiarabu, Kiingereza, Kichina na Kifaransa na pia zinawajengea uwezo wa kuhoji na kudadisi.

Akizungumzia elimu ya awali, alisema kuna vyuo 15,000 vya ualimu wa awali, na kwa mwaka huu walimu wa awali waliohitimu ni 3,167 huku serikali ikitumia Sh bilioni 985 kwa elimu bure, na kutoa mwongozo katika shule zote za msingi pia kuwe na shule ya awali.

Awali akizungumza katika kongamano hilo, Mkuu wa Chuo cha Aga Khan, Joel Lugalla alisema kongamano hilo limeshirikisha watafiti mbali mbali ndani na nje ya nchi na alisema lengo la kongamano hilo ni kupeana mbinu mbali mbali za kuboresha elimu kuanzia shule za awali, msingi na sekondari.

BODI ya Michezo ya Kubahatisha nchini kwa kushirikiana na Mamlaka ...

foto
Mwandishi: Vicky Kimaro

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi