loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Utalii wa picha unavyoneemesha mchoraji

“UTALII wa picha hautoshi katika hifadhi za taifa… Utalii ni pamoja na kuuza picha zako za kuvutia ambazo utazichora, hivyo tutoke nyumbani na tuendelee kuonesha kwamba tunaweza sana na tunaweza kukuza utalii kupitia sanaa zetu.”

Anasema Mkuu wa Mkoa wa Geita, Robert Gabriel alipotembelea wasanii mbalimbali na kufanya nao mazungumzo katika maonesho ya Tamasha la Urithi Wetu yaliyofanyika mkoani Geita alipowasisitiza wanasanaa kujua kuwa, muda wao ni sasa hivyo wasichezee fursa iliyopo mezani. Geita ni miongoni mwa mikoa 12 iliyofanya Tamasha la Urithi Wetu mwaka huu. Mwaka jana tamasha hilo lilihusisha mikoa 16 tu.

Mwaka huu Tamasha la Urithi Wetu mkoani Geita liliandaliwa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita, Wizara ya Maliasili na Utalii na kufadhiliwa na Shirika la Hifadhi la Taifa (Tanapa) likiwa na kaulimbiu: “URITHI WETU FAHARI YETU.”

Anasema ofisi yake itaendelea kushiriki na kuandaa eneo la pamoja litakalowakutanisha wanasanaa wote wanaochora, wanafinyanga na kuchonga ili kuwaunganisha na kuondoa changamoto za kukosa sehemu za kuonesha kazi zao kama wasanii.

Anatoa mwito kwa wadau na wawekezaji nchini kuwekeza katika sekta ya utalii, kwani serikali imekazana kufungua vivutio vya utalii hivyo ni wakati wa wananchi kunufaika kwa kujenga hoteli za kitalii, kuwekeza katika utamaduni, sanaa na kujenga vituo watakavyofikia watali.

Katika maonesho hayo, Mkuu wa Mkoa na washiriki wengine wanakutana na Jerison Lyamba (42), mkazi wa Katoro mkoani hapo ambaye ni msanii wa uchongaji, ufinyanzi wa vitu mbalimbali na uchoraji. Uchunguzi unabaini kuwa, mchoraji huyo hutumia sekunde chache kumtazama mtu na kuchora picha yake bila kurudia kumtazama hali iliyowashangaza wengi katika maonesho hayo.

Hali hiyo ya uharaka na uwezo wa kukariri sura anapotaka kuchora picha, kufinyanga ama kuchonga kitu anachokitaka, imekuwa ikiwashangaza watu wengi akiwamo Mkuu wa Mkoa, Gabriel hasa inapobainika kuwa, Jerison (Jerry) anaweza kutumia sekunde takriban 10 hivi, kujenga picha zaidi ya 50 na pia kutumia dakika 20 kuzichora au kuzifinyanga au kuchonga bila kukosea.

Katika makazi yake, utakutana na mapambo ya kuvutia, picha za wanyama na watu mbalimbali wakiwamo viongozi mashuhuri wa hapa nchini, na vitu vilivyochongwa au kufinyangwa kama vile vyungu na kadhalika. Katika mazungumzo na gazeti hili, Jerry anasema ingawa kipaji chake tangu akiwa na umri wa miaka sita kilikuwa uchoraji, uchongaji na ufinyanzi, alisomea fani ya ualimu.

Hata hivyo anasema kikwazo katika kipaji chake cha sanaa kilikuwa kwa wazazi wake ambao hawakuona kipaji hicho cha sanaa kama kitu kitakachomsaidia maishani kwake, hivyo ‘wakamlazimisha’ kusomea ualimu baada ya kuhitimu elimu ya kidato cha nne. Jerry anasema aliwahi kuajiriwa katika shule moja ya msingi hapa nchini na alikuwa akifundisha masomo ya Hisabati, Sanaa, Kiswahili na Maarifa ya Jamii.

Anasema hata hivyo, muda mwingi alikuwa anawaza namna ya kutimiza ndoto yake ya kuwa mchoraji na mchongaji bora.

“Katika moyo wangu nilijisemea na kuamini kuwa, si kazi nzuri ya kuajiriwa inayoweza kukupa furaha, bali kutumia kipaji chako kupata kipato ndiyo kazi inayokufanya upate furaha,” anasema Jerry na kuongeza: “Nilifundisha, nililipwa lakini bado furaha yangu ilikuwa haijatimia, bali nilitimiza furaha za watu wengine, hivyo niliendelea kutafuta njia.” Kwa mujibu wa mwanasanaa huyo, ajira yake ya ualimu ilidumu miaka 6 kwani aliomba ufadhili wa masomo nje ya nchi.

Mwaka 1983 alipata bahati ya kwenda Marekani na kuanza kuonesha kipaji chake cha kuchora, kufinyanga na kuchonga jambo lililomfanya asitishe ndoto za wazazi wake za kuwa mwalimu.

Anasema baada ya kuishi Marekani, alizidi kuimarika na baadaye mwaka 1998 aliajiriwa nchini Rwanda kama mwalimu wa kufundisha fani ya kuchora, kufinyanga, kuchonga na kubuni picha mbalimbali.

“Niliweza kufundisha kuchora niliona mwanga mzuri wa kuhakikisha vijana wengi wanatimiza ndoto yao ya kuwa wachoraji wazuri, taratibu wazazi walianza kunielewa kwani waliona fani hii inaniingizia fedha na kazi hii inanifanya mwenye furaha muda wote,” anasema.

Kwa mujibu wa msanii huyo mchoraji, mchongaji na mfinyanzi, mwaka 2006 alirejea nchini na kuajiriwa katika Shirika la Viwanda Vidogovidogo (SIDO) makao makuu Dar es Salaam na kufundisha vijana wengi ambao walikuwa na ndoto za kutaka kujiajiri kupitia sanaa ya uchoraji. Anasema mwaka 2007 aliamua kurejea nyumbani Geita na kuanza kutangaza fani yake katika jamii yake na kubadilisha mawazo ya wengi hasa wanaokatisha ndoto za watoto wao kwa kudhani sanaa za uchoraji ‘hazilipi’.

Jerry anasema awali jamii ilimshangaa, lakini baadaye ikaanza kumwelewa na kuhakikisha watoto, vijana na watu wazima wenye mawazo ya kuchora na kufinyanga, wanaendelea kupata elimu katika makazi yake. Anasema licha ya sanaa hiyo kupendwa na wengi, pia inazo changamoto kadhaa ikiwamo kubadili mitazamo ya baadhi ya watu wanaodhani kujishughulisha na uchoraji ni kupoteza muda.

Hata hivyo anasema, matumaini ya kurejea nyumbani yamefufuka na kuibua matumaini mapya baada ya ufunguzi wa Hifadhi ya Taifa ya Burigi-Chato anayosema ni fursa kwa wanasanaa waliopoteza matumaini kwani watapata soko la picha wanazochora kwa kuziuza kwa watu mbalimbali wakiwamo watalii.

Anasema mpaka sasa anamiliki darasa na yuko mbioni kufungua nyumba ya maonesho itakayotumika kuhifadhi picha zilizochorwa, zilizofinyangwa na kuchongwa na kila aina nyingine za picha. Anatoa mwito kwa watanzania kutumia Fursa iliyopo ya hifadhi za Rubondo, Burigi-Chato, Ibanda na Rumanyika kutangaza kazi zao na kuiona kazi yao kama ndizo kazi ya kuwaingizia kipato.

Mke wa Jerry aitwaye Magdalena Josephat anasema kwa sasa wamezaa watoto 6 na kazi hiyo ndiyo imewapa mafanikio makubwa na kukuza vipaji vya wananchi na wakazi wa eneo hilo wanaopenda kujifunza sanaa kupitia familia hiyo. Anasema aliolewa na mwanamume huyo akiwa hajui chochote, lakini baadaye alianza kuvutiwa na kazi ya kufinyanga.

Kwa sasa naye anajua kufinyanga, kuchora na kupaka picha huku watoto wao pia wakijua kuchora na kusaidia kazi mbalimbali za uchoraji. “Toka nimeolewa na huyo mwanaume nimenufaika na mengi kwanza kupata kujiajiri kwani nimefundishwa kuchora na kufinyanga, hivyo na mimi najiingizia kipato; kingine ni kutembea nchi mbalimbali kwa ajili ya kufanya maonesho na mume wangu kwani haya yote sikuyatarajia; nimejifunza kukabiliana na changamoto pamoja na kutafuta masoko kwa hilo najivunia sana,” anasema Magdalena.

Wasanii hao na mwingine Abednego Mboneko, mkazi wa Geita aliyeungana nao kupitia sanaa za uchoraji, uchongaji na ufinyanzi kuonesha kazi zake katika tamasha hilo, wanaahidi kutumia hifadhi za taifa zilizotangazwa hivi karibuni kama fursa.

Mboneko ambaye amepata elimu yake katika chuo cha sanaa cha Bagamoyo, anasema amekuwa mstari wa mbele kuchora picha nyingi katika shule ya msingi anayoifundisha mkoani Geita na shule jirani hivyo kuwafanya wanafunzi wengi kupata mwanga wa kujua vitu vingi kupitia picha.

Anasema amekuwa kielelezo kizuri cha kuibua vipaji vya watoto wanaopenda kuchora kutoka shule za msingi na kushauriana na wazazi wao kuhusu kuwapa uhuru watoto wao kuhusu wanachopenda kufanya katika maisha yao.

Wasanii hao wanasema upatikanaji wa vifaa vya kuchorea, kituo cha pamoja cha kutangaza kazi zao, ushirikishwaji juu ya taasisi mbalimbali zinazoandaaa maonesho nje ya Mkoa wa Geita ni changamoto kubwa wanayopambana nayo kwa njia mbalimbali.

Wanaiomba serikali na wadau wa utalii wakiwamo wawekezaji kuweka mazingira ya pamoja kutambua kazi za wasanii wanaochora na kuchonga kama kazi za wasanii wengine zinazoweza kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo nchini.

foto
Mwandishi: Diana Deus

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi