loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Kimiti na Nyerere walivyokutana kuisuka Tanganyika huru (2)

FEDHA hizo ambazo sasa ni sawa na takribani Sh milioni 50 zilikuwa ni nyingi wakati huo na zilitokana na mauzo ya rekodi zao za muziki.

“Mwalimu Nyerere alipokuja tulikusanyana wanafunzi wote tuliokuwa Uholanzi. Tulikuwa zaidi ya 70. Sisi (Kimiti na Lyimo) tukasema kwa kuwa alikuwa akizunguka kuomba msaada kwa ajili ya kusukuma maendeleo ya nchi yetu, tukasema tuna hela kidogo tukampa pauni 20,000.”

Kimiti anasema: “Mwalimu alishangaa akahoji mmepata wapi? Unajua Mwalimu alipenda kuhoji kila kitu, hapendi kupata hela ambazo hazijulikani… Tukamwambia, alipojua hilo, akafurahi sana.”

Kwa mujibu wa Kimiti, Mwalimu alipongeza hatua hiyo na kusema amefurahi kwa ubunifu wao wa kuunda bendi na pia, kufikiria nyumbani na Watanganyika wenzao badala ya kujifikiria.

“Nyerere alisema, ‘tunatuma watu ili watakapokwenda kusoma, warudi wasaidie nchi.”

Tofauti na Watanganyika wengine waliolowea ughaibuni kipindi hicho, Kimiti baada ya kuhitimu mafunzo yake alirejea nchini mwaka 1965 na kupangiwa kwenda kufundisha Chuo cha Kilimo cha Ukiriguru.

Akiwa chuoni hapo mkoani Mwanza, Kimiti anasema aliendelea na asili yake ya kupenda muziki kwa kuanzisha bendi aliyoiita ‘Crooning Stars’ na baadaye aliibadili na kuiita ‘Luna Fiesta’. Baada ya mwaka mmoja alikwenda Marekani kusoma na aliporudi aliendelea kufundisha Ukiriguru.

Baadaye alihamishiwa Makao Makuu ya Tanu kama Katibu Msaidizi baada ya Mwalimu Nyerere kugundua talanta yake kwenye tasnia ya utangazaji. Moja ya majukumu yake makubwa ilikuwa ni kuandaa programu za mafunzo ya siasa kwa wana-Tanu. Kimiti akawa anafundisha makuruta kambi za JKT, wanafunzi shuleni na vyuo mbalimbali ikiwemo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Aidha, alikuwa DJ na mtangazaji aliyeandaa na kutangaza vipindi vya siasa kama vile ‘The Rise of TANU’, ‘TANU katika Historia’ na kupiga nyimbo za kizalendo za kulaani mabeberu huku akipigia debe Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea. Kati ya mwaka 1969 na 1970 alikwenda Ujerumani kwenye kozi na kutunukiwa cheti cha masuala ya kazi (Labour Movement).

Mwaka 1973 alikwenda tena Marekani kuchukua Shahada ya Uzamili ya Sayansi ya Kilimo kwa miaka minne katika chuo cha Calpoly, California. Aliporejea nchini kutoka Marekani, alipangwa kuwa Mkuu wa Chuo cha Kilimo cha Uyole cha mkoani Mbeya tangu mwaka 1975 hadi 1979 kabla ya kuhamishwa na kuwa Mkuu wa Chuo cha Kilimo Nyegezi hadi mwaka 1982.

“Nilikuwa nasoma tu. Nilisoma kwenye nchi nyingi sana… Italia, Ujerumani, Romania, Bulgaria … mpaka wakaanza kuniita unprofessional figure kwa sababu kila mwaka wananipeleka kusoma. Walikuwa wananipeleka wenyewe (serikali). Ilikuwa bahati yangu tu.”

Bahati hiyo anaihusisha na alivyokuwa baba yake mzazi (Petro) ambaye kutokana na uadilifu, uaminifu wakati wa serikali ya kikoloni, mwaka 1954 alitunukiwa cheti cha utumishi bora uliotukuka kutoka kwa Malkia Elizabeth wa Pili. Alikabidhiwa cheti hicho na Gavana wa Kiingereza nchini Tanganyika, Edward Twining. Kimiti anasema: “Baada ya kupata hiyo tuzo, baba alituita watoto wake akatuambia kwamba cheti hicho ni matokeo ya kufanya kazi kwa uaminifu.

Akatuomba katika kazi zetu tusimuangushe. Hata baada ya uhuru, baba aliendelea na udereva na aliondoka kwa heshima zote akasema endeleeni wanangu.” Kisimati cha Kimiti kiliendelea kwa kuteuliwa katika nyadhifa mbalimbali katika Serikali ya Awamu ya Kwanza chini ya Mwalimu Nyerere.

Miongoni mwa nyadhifa ni pamoja na ubunge wa taifa ambao jina lake lilikuwa moja ya majina matatu yaliyofikishwa kwenye vikao vikuu vya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kupigiwa kura hatimaye kuibuka mshindi. Sambamba na ubunge wa taifa, mwaka 1982 Mwalimu Nyerere alimteua kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu mwaka 1982.

Alianza kufanya kazi chini ya Waziri Mkuu, Cleopa Msuya na baadaye chini ya Edward Sokoine (marehemu). Kimiti anamkumbuka Sokoine kwa uchapakazi na namna alivyothamini kila mtu. Miongoni mwa mambo anayokumbuka ni pamoja na alipowataka yeye (Kimiti) na mawaziri wenzake, Anna Makinda na Getrude Mongella kwenda Kanisa la Mtakatifu Joseph, jijini Dar es Salaam kusoma masomo kanisani.

“Alifanya hivyo kuonesha kwamba mawaziri nao wanapaswa kuwa watu wa kawaida, washiriki kikamilifu mambo ya kiimani,” anasema Kimiti na kusimulia kwamba walifanya hivyo na kuvuta hisia za waumini wa Kanisa hilo la Katoliki kwani walizoeleka kuonekana kwenye masuala ya siasa pekee.

Kisimati cha Kimiti kiliendelea pia kwenye awamu nyingine za serikali mpaka Awamu ya Tano (sasa) chini ya Rais John Magufuli kama atakavyosimulia kwenye makala ijayo, akiainisha juhudi za Mwalimu Nyerere kuikwamua nchi kiuchumi na kijamii.

BODI ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), ...

foto
Mwandishi: Stella Nyemenohi

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi