loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Asante Rais Magufuli, samahani Watanzania

ILIKUWA furaha kwa wafungwa 5,533, walioachiwa na Rais John Magufuli kwenye maadhimisho ya miaka 58 ya Uhuru wa Tanzania Bara, huku vifi jo na machozi ya furaha yakiwabubujika raia hao, walioanza kuachia jana, kutoka magereza mbalimbali nchini.

Mithili ya bibi harusi anayeingia ukumbini, ndivyo ilivyokuwa kwa wafungwa wa kike, waliaachiwa kwenye magereza mbalimbali, ambao walibubujikwa machozi ya furaha wakati waaachiwa na kuungana na familia zao.

Wakizungumza katika Gereza la Butimba mkoani Mwanza, baadhi ya wafungwa walioachiwa huru, walisema wanashukuru kuachiwa kwao na sasa wamebadilika kitabia kutokana na mafunzo mbalimbali, waliyopata wakiwa gerezani na wako tayari kuishi katika jamii.

“Namshukuru Rais Magufuli kwa msamaha huu, nakiri kwamba gerezani kumetufundisha mengi, naahidi kuwa mama bora, nimejutia makosa yangu”, ni kauli ya Rachel Josia, mkazi wa Kibara Bunda mkoani Mara, aliyekuwa akibubujikwa machozi.

Mama huyo alifungwa miaka mitano kwa kosa la kupigana na kumtorosha mtoto. Vailet Rashidi ambaye ni mkazi wa jijini Mwanza, alihukumiwa kifungo cha miaka mitano kwa kesi ya mauaji, alisema hana zawadi ya kumpa Rais Magufuli, bali anamshukuru kwa kutoa msamaha na kuahidi kufanya kazi kwa bidii ili kumuunga mkono.

Mbali ya kumshukuru Rais Magufuli, pia wamewaomba radhi watanzania kwa vitendo viovu, walivyofanya na kwamba sasa wamejirekebisha. Walisema gerezani kulikuwa shule ya ufundi, ambayo imewapa mafunzo mengi yakiwemo ya ufundi. Waliahidi kuendeleza vipaji vyao uraiani.

Akizungumza kwa furaha baada ya kuachiwa huru nje ya gereza hilo, Timothy Silas mkazi wa Kaliua mkoani Tabora, ambaye alifungwa miaka 30 kwa kesi ya unyang’anyi, alisema anamshukuru Rais Magufuli kwa kuwasamehe bila ya kujali makosa waliyofanya.

“Tunamshukuru sana Rais wetu Magufuli, tunaomba msamaha kwa viongozi wetu wote wa serikali, vyama vya siasa, viongozi wa dini na wananchi, tumejutia makosa yetu,” alisema Silas. Silas alisema binafsi alijutia kosa lake, lakini alipoingia gerezani hajajuta kukaa humo kwa miaka 20, kwa sababu akiwa humo alipata mafunzo ya ufundi uashi na anajivunia elimu hiyo.

“Kosa najutia, ila nashukuru gerezani palibadilika na kuwa shule kwangu, nimejifunza ufundi uashi, najivunia kujenga majengo ya nyumba mbalimbali za watumishi katika jeshi la magereza mkoa wa Mwanza, jengo la Kituo cha Polisi cha Nyamhongoro wilayani Nyamagana, baadhi ya vyoo katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando, sijatoka bure,”alisema Silas.

Aliwapongeza viongozi wa dini, waliokuwa wakihubiri katika gereza hilo kuwa wamewajenga kiroho na kimaadili, akiwemo yeye mwenyewe ambaye kwa sasa ni Mchungaji wa Kanisa la Wasabato (SDA). Alisema yeye alikuwa akitoa huduma za kiroho ndani ya gereza.

“Nafurahi na namshukuru sana Rais John Magufuli na sasa naenda nyumbani kuungana na familia yangu, Mwenyezi Mungu amlinde na ampe maisha marefu,” alisema.

William Ngosa ambaye ni mkazi wa jijini Mwanza, aliyehukumiwa kifungo cha miaka 30 kwa kosa la kuvunja na kuiba mwaka 2,000, alisema awali alifungwa miaka 15 jela, lakini baada ya kukata rufani, rufani yake haikuzaa matunda na ndipo alipohukumiwa miaka 30 kwa kosa hilo na amekaa gerezani kwa miaka 19.

“Natoa shukurani zangu za dhati kwa Rais Magufuli, tuliposikia ametangaza msamaha kwetu wafungwa wote tulifurahi, nashukuru pia uongozi wa Magereza kwa kututunza na kutulea kimaadili,” alisema Ngosa na kuomba jamii iwapokee, kwani sasa ni raia wema.

Mkoani Ruvuma, jumla ya wafungwa 181 waliachiwa kutoka magereza sita ya mkoa huo, huku baadhi yao wakisema wanajutia makosa yao na kuahidi sasa kuwa mfano mzuri kwenye jamii.

Akizungumza kwa niaba ya wenzake, mmoja wa wafungwa hao, Gallus Ndunguru alimshukuru Rais Magufuli kwa uamuzi wa kuwasamehe na kumuomba kuwaangalia wenzao waliobaki, kwani wapo wanaotumikia vifungo bila hatia.

Ndunguru aliahidi kuwa mfano mzuri kwa jamii inayowazunguka na kwamba ataenda kushiriki kazi za kujitolea na kujiletea maendeleo, kwani muda waliokaa gerezani umewafundisha mambo mengi mazuri na kuwapa mafunzo ya ufundi.

Mkoani Tabora, jumla ya wafungwa 207 wameachiwa huru huku baadhi ya waliosamehewa, wakikiri kufungwa kutokana na vitendo viovu walivyofanya. Walisema sasa wanajutia, kwa kushawishika kuingia kwenye makundi ya ulevi wa kupindukia.

Baadhi ya wafungwa hao walioachiwa kwa msamaha huo na kujutia makosa yao ni Sonda Mayumbi, aliyetumikia kifungo cha miaka 19 jela kutokana na kosa la kumpa mimba mwanafunzi.

“Najutia kosa langu kwa sababu limenigharimu maisha yangu ya ujana, nilifungwa kutokana na makundi na ulevi wa kupindukia uliosababisha kutumikia kifungo cha muda mrefu gerezani,”alisema Mayumbi.

Alisema alishawishika kufuata makundi ya ulevi uliopitiliza, ambao ulimshawishi kufanya jambo lolote baya bila woga.

Aliwaasa vijana nchini, kutumia muda wao vizuri na kuepuka makundi, kama alivyofanya yeye na kupoteza ujana wake gerezani na sasa ametoka nguvu zikiwa zimepungua, na sio kijana tena.

Agoma kuachiwa huru Wakati wenzao wakifurahia kutoka magerezani, hali ilikuwa tofauti katika gereza la Ruanda mkoani Mbeya, ambako mfungwa Merad Abraham aliyeachiwa kwenye msamaha huo, amegoma kutoka kwa madai hana mahali pa kuishi.

Badala yake, mtu huyo ameomba ahamishiwe Gereza la Ukonga, jijini Dar es Salaam.

Merad alikuwa akitumikia kifungo cha miaka 30 gerezani, kwa kosa la kubaka na adhabu yake ilikuwa inaisha Juni 20 mwakani na alifungwa Juni 20 mwaka 2000.

Kwa sasa mfungwa huyo amepelekwa kwenye zahanati ya gereza hilo kwa ajili ya matibabu, baada ya kugoma kuondoka, kwani amejijeruhi kwa jiwe usoni, kama msisitizo wa kukataa kuachiwa huru.

Mkoani Dodoma msamaha wa Rais Magufuli umewapa kicheko wafungwa 385 ambao wameachiwa huru na kuungana na familia zao uraiani, wakiwemo 114 wa Gereza la Isanga.

Akizungumza mara baada ya kuachiwa huru, Abdallah Ramadhan (55) Mkazi wa Singida aliyefungwa kwa kosa la kubaka mwaka 2000, alisema alibambikiwa kesi ya kubaka akiwa na miaka 35.

Ramadhan ambaye alikuwa anatumikia kifungo cha miaka 30 jela kwa kosa la ubakaji huku akiwa ametumikia miaka 19, amemuomba Rais John Magufuli kuwakumbuka na kuwapa msamaha wafungwa wengine, kwa sababu hali ndani ya gereza sio nzuri.

“Namshukuru Rais pamoja na wenzangu kwa kuweza kutupa msamaha, tumefarijika lakini kule bado kuna wazee na mahabusu wanateseka, kwa kifupi maisha ya kule sio mazuri hili liangaliwe,” alisema

Alisema wakati anatumikia kifungo chake, amejifunza mambo mengi, huku akionesha kusikitishwa na kifo cha mke wake. “Nimeambiwa mke wangu alifariki, nimeumia sana, nilimuacha akiwa na watoto wangu wawili wadogo leo ni miaka 19, nina hamu ya kwenda kuungana na watoto wangu japo mama yao katangulia mbele za haki,”alisema Ramadhan.

Aliongeza: “ Nimuombe sana Rais, hili la watu kubambikiziwa kesi aliangalie, mimi niliingiza mifugo shambani nikabambikiziwa kesi ya kubaka nikafungwa miaka 30 nimekuwa kwenye maumivu makali mno,”alisema Ramadhan.

Ramadhan alisema atakuwa balozi mzuri wa kufanya kazi kwa bidii kutokana na mafunzo, ambayo ameyapata wakati akiwa gerezani.

“Msamaha tuliopewa na Rais iwe chachu kwao ya kwenda kuwa walimu wa nidhamu katika mitaa wanayoenda kuishi” alisema.

Jijini Dar es Salaam, jumla ya wafungwa 293 wamepata msamaha huo wa Rais Magufuli, ambapo Mkuu wa Magereza jijini humo, Julius Ntambala alibainisha kuwa wafungwa hao walianza kuachiwa huru jana na kulakiwa na ndugu zao.

Alisema kuwa leo wataachiwa wengine na kuwa watakuwa wakiachiwa taratibu na hadi kufikia kesho kutwa, wote watakuwa wameachiwa kutoka magereza ya Keko, Segerea na Ukonga.

Alisema, kuna taratibu za kawaida za kiutendaji, zinazofanywa na uongozi wa gereza katika kuwaachia wafungwa hao, huku akibainisha kuwa wote watatolewa kama ilivyoagizwa.

Alisema,”Kesho (leo) tunaendelea kuwaachia wafungwa wengine hadi idadi kamili ya kuwaachia wafungwa wote 293 wa Mkoa huu wa Dar es Salaam na wote wataachiwa ili wakaungane na familia za wapendwa wao”.

Akitoa taarifa, Mkuu wa Magereza wa Mkoa wa Dodoma, Keneth Mwambije alisema wafungwa 385 walioachiwa kwa msamaha wa Rais, walikuwa miongoni mwa wafungwa waliopata mafunzo mbalimbali ya ujenzi, kilimo na kazi za mkono, kama ufumaji wa vitambaa na vikapu.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongela aliongozana na Kamati ya Ulinzi na Usalama kwenda Gereza la Butimba ambako alisema amehakikishiwa wafungwa wote waliosamehewa wataachiwa huru.

Aliwashukuru wafungwa walioachiwa huru gerezani hapo, kwa kuonesha utulivu na kwamba hatua yao ya kupatiwa msamaha na Rais Magufuli, inatokana na upendo wake kwa Watanzania hasa wanyonge.

Kamishina Mkuu wa Jeshi la Magereza nchini, Phaustine Kasike alimshukuru Rais John Magufuli kwa msamaha huo mkubwa na wa kihistoria aliuotoa kwa mara ya kwanza hapa nchini.

Alisema msamaha huo una utofauti na misamaha ya nyuma, ambayo iliwahi kutolewa kwa wafungwa nchini, ambayo ilijikita katika kuangalia aina ya makosa na kesi kama vile za unyang’anyi, wizi wa kutumia silaha, ulawiti na uhujumu uchumi, lakini msamaha wa mwaka huu uliotolewa umejikita katika kuangalia muda wa kifungo.

Aliwataka wafungwa waliopata mafunzo wakiwa magerezani, waende wakatumie ujuzi walioupata kwenye makazi yao katika kufanya kazi kwa bidii, kwa kuzingatia kanuni na sheria za nchi pasipo tena kujihusisha kwenye vitendo vya uhalifu.

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Christina Mndeme aliyeshuhudia kuachiwa kwa wafungwa kutoka magereza mawili ya Songea na Kitai, kati ya magereza sita mkoani humo, aliwataka walioachiwa huru kuwa mfano bora kwenye jamii.

Mndeme ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama, aliwataka kutumia mafunzo waliyopata wakiwa gerezani kuzalisha mali,ikiwemo shughuli za kilimo kama njia pekee ya kujikomboa na umaskini.

Pia, Mndeme alimuomba Kamishina wa Magereza nchini, kuliongezea Gereza la Kitai idadi ya wafungwa kwa kuwa ni miongoni mwa magereza ya kimkakati nchini yaliyopewa jukumu la kuzalisha chakula.

Alisema kuachiwa kwa wafungwa kwenye gereza hilo, kumepunguza nguvu kazi ya kilimo.

Wakati wakuu hao wa mikoa wakisema hayo, Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Agrey Mwanri aliwataka wafungwa waliopata msamaha kwenye mkoa wake, kufanya kazi kwa bidii na jamii inayowazunguka na kuachana na vitendo viovu.

Mkoani Songwe, wafungwa 96 ni miongoni mwa wafungwa waliopata msahama wa Rais Magufuli, alioutoa juzi kwenye maadhimisho ya miaka 58 ya Uhuru jijini Mwanza.

Mmoja wa wafungwa waliopata msamaha huo katika Gereza la Mbozi, Victoria Adam alimshukuru Rais Magufuli akisema gereza lilikuwa darasa kwake, ametoka akiwa na ujuzi na sasa anakwenda kuwa raia mwema.

Mfungwa mwingine, Fred Daud alisema anajutia kosa lake na sasa anaahidi kuwa raia mwema na atakwenda kufanya kazi kwa bidii uraiani.

Alisema gereza ni sehemu ya urekebishaji tabia na yeye amerejirekebisha.

Aliwashauri vijana wote wafanye kazi halali, ambazo hazitawaletea matatizo kwa kuwa kazi halali zipo nyingi. Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Nicodemus Mwangela alitembelea baadhi ya magereza yaliyoachia wafungwa na kuwashauri kuwa raia wema na kuwatia moyo waliobaki kubadilika tabia .

Kamishna Msaidizi wa Magereza, Laizack Mfaume Mwaseba alisema amekuwa akipokea malalamiko ya ucheleweshaji wa nakala za hukumu kutoka kwa wafungwa na amekuwa akiwasiliana na mahakimu ili waweze kuzitoa nakala hizo, kwa kuwa ucheleweshaji huo unawanyima wafungwa haki ya kukata rufaa.

Juzi kwenye Sherehe za Miaka 58 ya Uhuru wa Tanzania Bara mkoani Mwanza, Rais Magufuli alitoa msamaha wa kihistoria kwa wafungwa 5,533 nchini.

Mikoa na idadi ya wafungwa na mahabusu waliosamehewa ni: Kagera (713), Dodoma (385), Morogoro (365), Mara (260), Mbeya (259), Kigoma (252), Tanga (245), Geita (230), Rukwa (214), Arusha (208) Dar es Salaam(293) na Manyara 207. Mikoa mingine ni Tabora (207), Mwanza (190), Ruvuma (181), Singida (139), Simiyu (136), Lindi (299), Pwani (128), Iringa (110), Songwe (96), Katavi (74), Shinyanga (74) na Njombe 70.

Imeandikwa na Nashon Kennedy,Mwanza, Anastazia Anyimike,Dodoma, Evance Ng’ingo,Dar, Muhidin Amri, Songea na Lucas Raphael, Tabora.

MASHIRIKA mbalimbali ya kimataifa ya usafiri ...

foto
Mwandishi: Waandishi Wetu

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi